May 21, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ukomo wa urais uheshimiwe

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere

Spread the love

MJADALA juu ya nyongeza ya muda wa Rais John Magufuli, kuendelea kubaki madarakani, baada ya kipindi chake cha urais kumalizika, umepamba moto.

Ndani ya Bunge la Jamhuri, baadhi ya wabunge wamezungumza bila woga, kile wanachoita, “atake asitake,” ni lazima Rais Magufuli aongezewe muda wa kubaki madarakani.

Mjadala huu umeibuka, wakati viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wamepiga marufuku kwa wanachama wake wenye mtazamo huo, wakieleza mjadala huo hauhitajiki na hauna afya kwa chama chenyewe na taifa.

Kwamba, Rais Magufuli hataongeza hata siku moja mara baada ya kipindi chake cha miaka kumi kumalizika.

Rais Magufuli mwenyewe, mara kadhaa amenukuliwa akisema, ataheshimu Katiba ya nchi na hatoongeza hata siku moja ya kubaki madarakani.

Hata hivyo, hadi sasa, hakuna anayejua ajenda ya wanaotaka Rais Magufuli aongozewe muda, wanalengo gani.

Sote tunafahamu ukomo wa urais, ni miongoni mwa tunu muhimu zilizosaidia taifa hili kuwa imara na lenye amani na utulivu.

Tunayo mifano mingi ya baadhi ya nchi zisizoheshimu misingi hiyo zinavyoyumba kwa kukosa amani, kutokana na watu wachache kusukumwa na ulafi wa madaraka.

Hakuna anayeweza kutushawishi, sababu za kuondoa kifungu kinachoweka ukomo wa urais.

Tangu mwaka 1992, Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ameonya kuwa mjadala huu wa kuondoa ukomo wa rais, usitishwe mara moja.

Kutokana na muktadha huo, suala la ukomo wa urais, lina umuhimu mkubwa kama taifa.

Ni lazima tulienzi kama tunu ya taifa. Jambo hili limekwishafanyiwa maamuzi. Tusifanye makosa ya kuliondoa kwenye katiba.

error: Content is protected !!