January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ukiukwaji haki za binadamu wakithiri

Jaji Mstaafu Amir Maneto (kushoto) akizindua ripoti ya haki za binadamu ya mwaka 2014. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Helen Kijo Bisimba.

Spread the love

RIPOTI ya Haki za Binadamu ya mwaka 2014, imezinduliwa leo jijini Dar es Salaam, ikionesha kuwepo kwa ukiukwaji mkubwa wa haki ya kuishi za Watanzania. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Ripoti hiyo imetayarishwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa kushirikiana na Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC) na kuzinduliwa na Jaji mstaafu, Amir Manento.

Taarifa ya ripoti imegawanyika katika sura 10. Kila sura ikiwa na taarifa za kina za ukiukwaji wa haki za binadamu.

Inaonesha matukio hayo katika nyanja za haki za kiraia; haki za kisiasa; haki za kiuchumi; Haki za kijamii; haki za kitamaduni na haki za kijumla au kimakundi.

Maneto ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu, amesema “matokeo ya ukatili na mauaji katika nchi yetu yameota mizizi na toka ripoti hii ianze kuandikwa mwaka 2002, taarifa za mauaji zimeibuliwa kwa kasi kuliko ilivyokuwa hapo awali”.

“Watu kujichukulia sheria mikononi ambapo mshukiwa yeyote wa uhalifu kama wizi, amekuwa akichomwa moto hadharani. Mauaji ya vikongwe, watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), mauaji yatokanayo na imani za kishirikina, ajali zinazozuilika na mauaji ya askari wa Jeshi la Polisi yanatia doa nchi yetu,” ameeleza Maneto.

Mbali na mauji hayo, pia yapo mauaji yanayofanywa na vyombo vya dola dhidi ya raia. Mauaji hayo yanafanyika huku Ibara ya 14 ya Katiba ya Tanzania ikitoa haki ya kuishi.

Takwimu za ripoti hiyo zinaonesha hadi June 2014, kuwepo kwa vifo 320 vinavyohusisha mauji ya kishirikina; mauji ya watu 473 yaliyotokana na watu kujichukulia sheria mkononi; mauaji ya watu 3 wenye ulemavu wa ngozi na vifo vya askari polisi vitatu.

Aidha, wanawake na watoto wameendelea kupata changamoto katika uvunjifu wa haki zao. Mwaka 2014, zaidi ya wasichana 1,000 walifanyiwa ukeketaji wilayani Tarime na Serengeti. Matukio ya ubakaji pia yameendelea kuwa mengi ambapo kumeripotiwa zaidi ya matukio 2, 878 kwa mwaka 2014.

Kwa upande wa Zanzibar, ripoti hiyo imeonesha kuwa, mwaka 2014 vilitokea vifo 88, ambavyo vilitokana na ajali za barabarani huku matukio ya mimba za utotoni yakiwa ni 21 na ndoa za utotoni matukio 19.

Aidha, Mkurugenzi mtendaji wa LHRC, Dk. Helen Kijo-Bisimba amesema kashfa ya uchotwaji wa mabilioni ya shilingi katika akaunti ya Tegeta Escrow, imekuwa ni mojawapo ya matukio makubwa ya kashfa za rushwa kuwahi kutokea nchini.

Amesema kashfa hiyo ilihusisha watu kutoka kada mbalimbali kuanzia serikali kuu, idara mbalimbali za serikali kama Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA), Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), viongozi wa dini na majaji ambapo walichukua fedha kupitia benki ya Mkombozi.

“Kashfa ya Akaunti ya Escrow imeharibu sana muonekano wa serikali kuu, idara nyingine muhimu za serikali, pia zilihusishwa katika kashfa hii. Kituo cha LHRC kinaihusisha kashfa hii moja kwa moja na mmomonyoko wa maadili nchini,”amesema.

Bisimba ameongeza kuwa “utendaji wa kifisadi na manunuzi kinyume cha sheria yanaathiri utaratibu mzima wa manunuzi ya serikali, lakini pia yanaathiri uchumi wa nchi na wananchi kwa ujumla”.

Ripoti hiyo pia imeonesha takwimu na maelezo ya upatikanaji na usambazi wa huduma za kijamii hususani huduma za afya, elimu na maji.

error: Content is protected !!