Tuesday , 5 December 2023
Home Habari Mchanganyiko Ukimya takwimu za corona: Askofu Niwemugizi arudisha Ibada
Habari MchanganyikoTangulizi

Ukimya takwimu za corona: Askofu Niwemugizi arudisha Ibada

Askofu Severine Niwemugizi, Jimbo Katoliki la Rulenge-Ngara
Spread the love

ASKOFU Severine Niwemugizi, Jimbo Katoliki la Rulenge-Ngara mkoani Kagera ametangaza kurejesha misa jimboni humo kuanzia kesho Jumapili ya tarehe 24 Mei, 2020. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Askofu Niwemugizi alitangaza kusitisha misa na maadhimisho mengine yanayokusanya waumini wengi makanisani ikiwemo sala za jumuiya kwa kipindi cha mwezi mmoja kuanzia tarehe 19 Aprili, 2020.

Uamuzi huo aliuchukua ili kuwalinda waumini wa jimbo lake na maambukizi ya ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona (COVID-19) ambao ulikuwa umeingia nchini.

Leo Jumamosi tarehe 23 Mei, 2020, MwanaHALISI ONLINE limezungumza na kiongozi huyo wa kiroho ambaye amesema, tangu walipozuia ibada na mikusanyiko, taarifa na takwimu za corona zimekuwa hazitolewi na kutoka kwa mamlaka.

“Kwa bahati mbaya, baada ya muda kusitisha ibada, taarifa hazikutoka tena na hivi tunavyozungumza hakuna takwimu kwani huku tuliko (Kagera) tuko gizani.”

“Kwa msingi huo, tukasema hakuna takwimu, hakuna taarifa tunazozitegema, tutarejea ibada kuanzia kesho (Jumapili) huku tukiendelea kuchukua tahadhali,” amesema Askofu Niwemugizi.

Askofu huyo ameagiza tahadhali zichukuliwe kwa makanisa yote kuwepo maji ya kuwawezesha kunawa mikono, kuvaa barakoa na kukaa umbali kati ya mtu na mtu.

“Tunataka kupunguza muda wa ibada ili misa zisiwe ndefu sana na pale itakapowezekana tutaongeza ili wachache waweze kuingia kanisani,” amesema Askofu Niwemugizi.

Kuhusu mikusanyiko amesema, jumuiya ndogondogo nazo zitarejea lakini kwa tahadhali kubwa kuchukuliwa.

Askofu Niwemugizi amewataka waumini wa jimbo hilo, “wawe na utulivu kwa sababu wamekuwa wanasikia mambo mengi kwamba hatutaki wasali lakini ukweli ni kwamba ulikuwa ni kipimo kizuri cha kuona je, wakiwa nyumbani wanaweza kusali.”

“Mungu haabudiwi tu kanisani bali anaweza kuabudiwa nyumbani au kanisani na watambue ibada zinarejea ila wachukue tahadhali,” amesema.

Kiongozi huyo amezungumzia pia kauli ambazo zimekuwa zikitolewa za viongozi wa dini kusimamia viapo vyao na kutowazuia waumini kusali kanisani, amewashanaga wale wote wanaohoji kiapo chake kwani wanaozungumza hivyo, hawajui majukumu ya askofu.

“Kiapo ambacho wanakisema ni kipi hiko, kama anakijua kiapo changu kwa sababu, mtu anazungumza kitu ambacho hajui majukumu ya askofu. Mimi naongozwa na sheria za kanisa katika kusimamia jimbo.

“Labda angesema tusimamie taratibu zenu ni vizuri kuliko kusimamia viapo. Kiapo nilichokiapa ni kumtii Baba Mtakatifu kwa sababu ndiye aliyeniteua kuwa askofu na kama namtii yeye, yeye mwenyewe alisitisha ibada takatifu pale Roma.

“Kama ni kusimamia taratibu zangu za kuendesha ibada, ningesema safi sana kwa sababu nina mamlaka hayo,” amesema Askofu Niwemugizi.

Askofu Niwemugizi anaungana na Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kulutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe mkoani Kagare, Benson Bagonza ambaye ametangaza kuanzia tarehe 31 Mei, 2020 ibada zilizokuwa zimesitishwa zitarejea.

Askofu Benson Kagonza, KKKT Dayosisi ya Karagwe

Askofu Bagonza alisitisha ibada kuanzia tarehe 26 Aprili, 2020 kwa siku 30 ili kuwalinda waumini na maambukizo ya corona.

Hata hivyo, Askofu Bagonza ametoa maelekezo 18 yanayopaswa kuzingatiwa. Maekezo hayo ni;

 1. Kila eneo la ibada pawepo na ndoo ya maji na sabuni, kila muumini anawe mikono aingiapo/awapo/atokapo ibadani.
 2. Waumini wote wavae barakoa wakati wote wa ibada.
 3. Kikosi Kazi cha Dayosisi (KAD-COVID 19 TASK FORCE) kitapeleka baadhi ya vifaa vyote muhimu kila mtaa ili kuboresha viwango vya usafi na barakoa za bei nafuu.
 4. Kikosi Kazi kinaandaa semina maalum kwa watoa nasaha ili kuwahudumia watoa huduma wasikate tamaa katika wajibu wajibu (Caring for Care Providers).
 5. Sakramenti ya Meza ya Bwana (kama ni lazima), ipokelewe mkononi si mdomoni tena. Washiriki wanawe tena kabla ya kushiriki. Waadhimishaji wavae barakoa (mask) wanapoadhimisha na wanapogawa mapaji. Mchungaji ana ruhusa ya kusitisha Sakramenti kama anaona washiriki wamejaa hofu kuliko kiu na uchaji wa  kushiriki mafumbo haya ya kiimani.
 6. Sakramenti ya ubatizo imesitishwa isipokuwa kwa dharula. Hata hivyo, waumini wanaelekezwa kuandikisha majina ya wanaotaka kubatizwa ili kutimiza takwa la kikatiba 3.5.7 (d). Asiyeandikishwa, hawezi kupata huduma endapo litatokea la kutokea.
 7. Ibada za ndoa zilizokwishatangazwa zifungwe kwa maelekezo maalum toka ofisi ya Dean. Ambazo hazijatangazwa zisubirishwe isipokuwa zinazowahusu:-
 8. Waumini walio katika vyombo vya ulinzi wanaolazimika kuitikia amri maalum.
 9. Wagonjwa mahtuti.
 10. Watakaotimiza masharti yanayopatikana ofisi ya Dean.
 11. Mafundisho ya Kipa Imara, Sunday School na jumuia vimesitishwa.
 12. Ibada za mazishi zifanyike kwa ushirikiano na viongozi wa serikali na wataalam wa afya katika eneo husika. Wajibu wa Mchungaji/Mwinjiisti ni sala na ibada, yaliyobaki ni jukumu la serikali na watalaam wa afya. Maelekezo yao yafuatwe.
 13. Salaam za kutakiana amani ibadani zifanyike kwa kupunga mikono au kuinama.
 14. Wanaohesabu sadaka wawe wachache – wasiozidi 4, na wahudumu waliobaki washuhudie tu. Barakoa (mask) na gloves vivaliwe. Maji ya sabuni yawe jirani na kila baada ya muda wanawe tena. Sarafu zisafishwe kwa maji yenye sabuni.
 15. Ibada ziwe fupi (si zaidi ya saa 1), vitongozi na jumuia vitapangwa zamu za kuja ibadani na taratibu hizi ziheshimiwe.
 16. Waendesha mnada wa sadaka na malimbuko wavae gloves na pawepo na maji jirani ili baadhi ya vitu vioshwe kulingana na hali yake.
 17. Wazee zaidi ya miaka 70 na wenye matatizo ya kiafya ya kudumu,wanashauriwa kubaki nyumbani.
 18. Watoto wabaki nyumbani au wakija kanisani wabaki na wazazi wakati wote.
 19. Mazoezi ya kwaya na uimbaji ibadani vimesitishwa.
 20. Wahudumu kanisani – wainjilisti, wahudumu wa zamu, parish workers na wachungaji wapate vifaa vya kujikinga na kutakasa vyombo, vitasa na maeneo yote yanayoguswa na watu wengi.

Makanisa yenye madirisha madogo yasiyoruhusu mzunguko wa mzuri wa hewa (orodha imeambatanishwa), yaanze jitihada za kurekebisha kasoro hii. Ni ruksa kusalia nje endapo mzunguko wa hewa si mzuri.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

RPC Songwe awafunda trafki kuzingatia uadilifu

Spread the loveASKARI wa kikosi cha usalama barabarani mkoani Songwe wametakiwa kuendelea...

Habari Mchanganyiko

Mchimba madini jela maisha kwa kubaka, alihonga Sh 500

Spread the loveMahakama ya wilaya ya Songwe imemtia hatiani na kumhukumu kifungo...

Habari Mchanganyiko

Mlima wa Moto wazindua kongamano la SHILO kumuenzi Rwakatare

Spread the loveKANISA la Mlima wa Moto Mikocheni jijini Dar es Salaam,...

Habari za SiasaTangulizi

Maafa Manyara: Rais Samia akatisha ziara yake Dubai

Spread the loveRAIS wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amekatisha ziara yake...

error: Content is protected !!