June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ukawa yatangaza kituo cha kutoa habari za Uchaguzi

Spread the love

UMOJA wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) leo umezindua rasmi ukumbi maalum wa vikao na utoaji taarifa mbalimbali zinazohusu masuala ya vyama hivyo vinavyounda umoja huo. Anaandika Hamisi Mguta … (endelea).

Akizungumza na waandishi katika ukumbi huo Afisa Habari wa Chama cha Demokrasi na Maendeleo (CHADEMA), Tumaini Makene amesema ukumbi huo utatumika kutoa maelezo mafupi na vikao na waandishi wa habari kuanzia saa sita hadi nane za mchana.

Makene ameutaja Ukumbi huo kuwa ni Kisenga uliopo Millenium Towers Kijitonyama Jijini Dar es Salaam ni ukumbi wa kwanza kwa umoja wa vyama hivyo kuuteua kuwa ukumbi maalum wa kufanyia vikao badala ya kubadilibadili maeneo ya mikutano yao.

Umoja huo unaomuunga mkono mgombea Urais, Edward Lowassa kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), unaundwa na vyama vinne ambavyo ni Chadema yenyewe, Chama cha Wananchi (CUF), National League for Democracy (NLD) na NCCR-Mageuzi.

Makene amesema kuanzia leo ukumbi huo utatumika kufanyia vikao na kila kinachohusisha masuala ya habari kwa vyama vyote vya ukawa ikiwa kama idara ya habari ya Ukawa hadi pale watakapotangaza mabadiliko mengine ya ratiba zao.

Amesema “kuanzia leo na siku zote zinazoendelea ukumbi huu utatumika kufanyia vikao na waandishi wa habari pamoja na kutoa taarifa zinazohusu vyama vya Ukawa.”

Aidha alibainisha kuwa muda wa kutoa taarifa kwa waandishi wa habari au maelezo yeyote utakuwa ni saa 6 hadi saa 8 kila siku.

Hii ni mara ya kwanza kwa chama hicho kikuu cha upinzani pamoja na Ukawa kuwa na kituo cha kutolea taarifa za Uchaguzi kila siku tangu kianze kushiriki uchaguzi mkuu mwaka 1995.

error: Content is protected !!