August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ukawa yapigia chapua MSD

Spread the love

GODWIN Mollel, Msemaji Mkuu wa Kambi ya upinzani-Wizara ya Afya ameitaka serikali iongeze Bajeti ya Wizara ya Afya sambamba na ongezeko la Bajeti ya Taifa ili angalau sekta ya afya iwe na asilimia 11.4 kama ilivyokua katika mwaka unaoisha, anaandika Happiness Lidwino.

Mollel ambaye pia ni Mbunge wa Siha (Chadema) amesema hayo leo bungeni wakati akichangia hoja kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa mwaka wa fedha 2016/17 ambapo ameitaka serikali kuongeza bajeti katika wizara hiyo.

“Wakati bajeti ya Taifa imepanda kwa zaidi ya takribani Trilioni 6.5 (kutoka trilioni 22.4 ya mwaka 2015/16 hadi trilioni 29 ya mwaka 2016/17), bajeti ya Wizara ya Afya imepungua kwa bilioni 18 kwa mwaka wa fedha 2016/17.

Ameongeza kuwa, hii inamanisha kuwa Wizara ya Afya haijapata kipaumbele, maana yake ni kwamba huduma za afya zitakuwa mbovu kuliko mwaka uliopita.”

Mollel katika hotuba yake ameeleza kuwa, upungufu wa madawa katika Bohari ya Dawa (MSD) unaweza kuongezeka kwani serikali imetenga Sh. 65.1 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa dawa, kiasi hicho kinatosha mahitaji ya nchi kwa mwezi mmoja na nusu tu.

“Kwa kukadiria kuwa Tanzania ina watu takribani milioni 49.8 (1) wanaohitaji matibabu, kiasi kilichotengwa kinatosha kutibu watu milioni 5.6 kwa mwaka. Je, watu wengine millioni 44 wanaobaki watatibiwa na nini na wapi?” amehoji.

Amesema, Kambi Rasmi ya Upinzani inaishauri serikali iongeze bajeti ya madawa kutoka asilimia 11 (Sh. 65.1 bilioni) mpaka angalau asilimia 50 ya mahitaji (Sh. 295 bilioni).

Amesema, “ili dawa na vifaa tiba visambazwe, MSD inahitaji kupewa fedha illiyoomba. Mpaka Machi 2016, MSD walikuwa wanaidai serikali shilingi bilioni 131. Serikali imetenga shilingi bilioni 108 kulipa deni la nyuma, hivyo kubakiza deni la shilingi bilioni 23.

“MSD waliomba kutengewa shilingi bilioni 114 kwa ajili ya ugomboaji wa mizigo bandarini (Clearance & Forwarding) na kusambaza madawa na vifaa tiba. Wametengewa shilingi bilioni 35 tu, kiasi hiki kikipungua kwa shilingi bilioni 79.

“Kiasi hiki kilichotengwa kinakidhi mahitaji ya MSD kwa miezi minne tu. Je, serikali inataka dawa na vifaa tiba viozee kwenye bohari na bandarini kwa miezi mingine? Ikiwa MSD itakopa ili kujiendesha kwa mwaka mzima, basi itahitaji kukopa shilingi bilioni 79 hivyo deni lake mpaka Juni 2017 litakuwa shilingi bilioni 102. Tutakuwa tumetengeneza deni jipya tena la kilipa mwakani.”

Ameongeza kuwa, serikali inaendelea kutengeneza deni lingine la Sh. 102 bilion kwenye eneo moja tu ,bandari na usafirishaji , hivyo kwa niaba ya kambi rasmi ya upinzani ameitaka serikali iongeze, bajeti ya MSD angalau kulipia deni lote ambalo baki yake ni shilingi bilioni 23 na hela za usafiri na bandari bilioni 79.

Katika hatua nyingine Mollel ameitaka serikali iongeze fedha kwa ajili ya wagojwa wa Ukimwi kutoka asilimia 11 (Sh. 48 bilioni) mpaka angalau asilimia 50 (Shilingi 218 bilioni).

Aidha, ameishauri serikali kufanya   uwekezaji katika maeneo ambayo yanaweza kuzalisha madawa mfano Lushoto kuna miti ya miquinini (sinchona tree), magome yake yamebeba ndani yake alkaloid quinine ambayo hutengeneza dawa ya quinine ya kutibu malaria.

“…dawa hii ni silaha ya mwisho kutibu malaria vilevile tunaweza kuotesha mimea ya kuzalisha ambayo majani yake hutumika kwaajili ya dawa mseto marufu ALU(Artemisia) na mengine mengi ambazo zinastawi katika nchi za tropikali kuliko mkutegemea sana nje,” amesema.

error: Content is protected !!