August 16, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ukawa yapigania haki za waliobomolewa

Spread the love

KAMBI Rasmi ya Upinzani imeitaka serikali kuhakikisha inalipa fidia waathitika waliobomolewa nyumba zao kwa kadri walivyopoteza mali zao wakati wa bomoabomoa, anaandika Regina Mkonde.

Hayo yamesemwa leo na Pauline Gekul, Waziri Kivuli wa Wizara ya Ofisi ya Makamu wa Rais na Mazingira wakati akitoa hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu makadirio ya mapato na matumizi katika Ofisi ya Makamu wa Rais na Mazingira kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017 bungeni mjini Dodoma.

“Kambi Rasmi ya Upinzani inaamini kabisa kwa njia ya migogoro iliyokuwepo kati ya serikali na wananchi hasa wale waliokuwa wamejenga maeneo ambayo kwa mujibu wa serikali ni hatarishi na kupelekea kubomolewa nyumba zao kumesababishwa na uzembe uliofanywa na serikali,” amesema.

Anaeleza , utolewaji wa elimu ya ujenzi katika mazingira hatari lazima uende sambamba na kuzielewesha taasisi za umma ambazo zinatoa huduma za kijamii kwa wananchi kutokana na kwamba wasingepeleka huduma kwenye maeneo hayo wahanga wasingejenga.

“Kama Mamlaka za Maji na Shirika la Umeme zingekuwa na uelewa mpana kuhusiana na dhana pana ya mazingira kwenye maeneo hatarishi zisingepeleka huduma kwa wananchi na kwamba wasingejenga nyumba zao,” amesema.

Ameongeza kuwa, jambo lingine lililochangia baadhi ya wananchi kujenga katika maeneo hayo ni kitendo cha baadhi ya halmashauri katika maeneo husika kutoa leseni za makazi pamoja na kulipisha wamiliki kodi za majengo.

Kwa upande wa mazingira na shughuli za kiuchumi , Gekul amesema shuguli za kiuchumi zinazoathiri mazingira zimesababishwa na hali ya kutoangaliwa kwa hali halisi inayofaa katika uchimbaji wa madini, kilimo, na ufugaji wa mifugo mingi kwenye sehemu ndogo ya ardhi.

“ Kilimo kinachotumia mitambo mikubwa na kinaufanya udongo kuwa mwepesi kiasi cha kuondolewa na maji ya mvua pamoja na upepo, ufugaji mifugo mingi katika eneo ndopo kutokana na eneo la malisho kuchukuliwa kwa aajili ya shughuli zingine za kiuchumi kumepelekea kuharibu mazingia,” amesema.

Ameongeza “Kwa lugha rahisi ni kuwa uendelevu na kukua kwa uchumi wetu kama nchi kunategemea ni kwa jinsi gani kama nchi tumejipanga vizuri kuhakikisha mazingira kwa kila sekta inakua endelevu, je hilo swala linafuatiliwa?”

Amesema, kabla ya serikali kufikiria kuwa na uchumi wa viwanda ni lazima itazame namna ya kuwekeza kikamilifu katika kuhakikisha kuwa mazingira yanalindwa na pamoja na kuweka mipango mapema ya kuanza kufanya tathimini ya kimazingira kabla ya kutekeleza mradi wowote kwa ajili ya kuwa na uchumi endelevu.

error: Content is protected !!