September 23, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Ukawa wawekwa chini ya ulinzi bungeni

Spread the love

BAADA ya kutolewa nje, wabunge wanawake kutoka vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wamewekwa chini ya ulinzi, anaandika Happiness Lidwino.

Tumaini Makene, Ofisa Habari wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (chadema) ameeeleza kisa hicho kwamba, tukio hilo linatokana na kejeli na dharau za wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa Ukawa ndani ya bunge.

“Wabunge hao mpaka mchana huu wamezungukwa na Askari wa Usalama kwenye Ofisi za Kambi Rasmi ya Upinzani (KUB) ambako walikuwa wanaendelea na kikao,” ameeleza.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa, tukio hilo ni mwendelezo wa sakata lililoanza jana jioni bungeni likimuhusisha Mwita Waitara, Mbunge wa Ukonga aliyetolewa nje ya bunge kwa madai ya kutaka kumfanyia fujo Augustin Holle, Mbunge wa Kasulu Vijijini.

Akizungumzia sintofahamu ya jana Makene ameeleza kwamba kisa hicho kimetokana na kiti cha spika kuyumba.

“Jana mara baada ya Bunge kurejea kipindi cha pili cha jioni, Naibu Spika, Tulia Ackson alionekana kuyumba,” imeeleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo inafafanua kwamba, Tulia alishindwa kulisimamia Bunge kutokana na kuruhusu matusi, lugha za kejeli na upotoshaji kutoka kwa wabunge wa CCM.

Inaeleza Tulia alikuwa akizuia miongozo kutoka kwa wabunge wa Ukawa ambapo walikuwa wakiaka kutoa kutoa taarifa ili baadhi ya mambo yatolewe ufafanuzi.

“Alianza Mbunge wa CCM kutoka Zanzibar akisema kuwa, Wabunge wa Upinzani (Ukawa) wanaharishia mdomoni badala ya nyuma,” imeeleza taarifa hiyo na kuongeza;

“Naibu Spika hakuchukua hatua yoyote kama ambavyo hata akili ya kawaida ingetarajia ifanyike hivyo. Akakaa kimya huku akizuia wabunge wa ukawa kuhoji.”

Taarifa inaeleza kuwa, Mbunge wa Ulanga ambaye ni mtoto wa marehemu Celina Kombani aliendelea lugha za kejeli na kupotosha.

“Akasema Ukawa wamerudi bungeni kuchangia baada ya yeye kumshauri shemeji yake Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa KUB ili aruhusu. Kwa hiyo wako pale bungeni kwa sababu yake.

“Akaendelea kudai kuwa sifa ya Wabunge wanawake wa Chadema kupata Ubunge ni kila mtu lazima aitwe Baby kabla ya kupata Ubunge Viti Maalum. Huku wanaume wakifanya vitendo vya kishoga.”

Jenista Mhagama, Mbunge wa Peramiho alidai kuwa, wabunge wa upinzani nao walikuwa wakitoa matusi jambo ambalo lilizidisha kelele ambapo Spika Tulia alimtaka mwandishi wa Hansard afute maneno machafu yote.

“Akafuata Mbunge mwingine wa CCM kutoka Kigoma, Kasulu akasema yeye ana ushahidi kwamba, Tundu Lissu ana jalada la ugonjwa Hospitali ya Milembe!

“Ndipo wabubunge wa Ukawa baada ya kunyimwa nafasi ya kuzungumza wakasimama na kuanza kupiga kelele,” imeeleza taarifa hiyo.

Na kwamba, baada ya kuona kiti kinazidi kuyumba, ama kwa makusudi au kwa kujua kinachofanya, ndipo Waitara akalazimika kusimama akimtaka yule Mbunge wa CCM afute kauli zake hizo za upotoshaji. Ndipo akafuta.

“Akafuta lakini tena akasema Mbunge wa Kibamba John Mnyika anaumwa na anajua yuko Hospitali ya Mhimbili anatibiwa.

“Kitendo hicho cha yule mbunge kuendelea kutoa lugha za kejeli, kupotosha na kuzungumza mambo ambayo hawezi kuthibitisha huku kiti kikiwa kimya, kikamfanya Waitara asogee kwake ili kuwa karibu naye.”

Taarifa inaeleza, baada ya kuona hivyo Naibu Spika akaagiza askari wamtoe nje.

“Hicho kilichotokea jana jioni, ndiyo mwendelezo wake wa asubuhi hii ambapo wabunge wanawake wa Ukawa wametolewa bungeni baada ya kutaka ufafanuzi na hatua dhidi ya hizo kauli za udhalilishaji zilizotolewa jana, mbele ya Naibu Spika ambaye naye ni Mbunge wa Viti Maalum,. Imesema taarifa hiyo na kuongeza.

error: Content is protected !!