July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

UKAWA wataka Tume Huru ya Uchaguzi

UKAWA wataka Tume Huru ya Uchaguzi

Viongozi wa UKAWA

Spread the love

MUUNGANO wa kutetea Katiba ya Wananchi (UKAWA), umepanga kuhakikisha Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inafanyiwa marekebisho makubwa, MwanaHALISI Online linaweza kuripoti.

Habari kutoka ndani ya kikao cha usuluhishi cha kujadili mgogoro uliolikumba Bunge Maalum la Katiba, ambacho kiliitishwa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi zinasema, UKAWA unawekeza nguvu kuishinikiza serikali ifanye marekebisho ya katiba ya sasa ikiwa Katiba Mpya haitapatikana.

“Katika kikao kile, UKAWA wameweka mezani malengo makuu mawili: Kwanza, wanataka kuwapo maafikiano yatakayokwamua Bunge Maalum la Katiba na hatimaye kupatikana Katiba Mpya,” ameeleza mtoa taarifa ndani ya kikao cha usuluhishi.

“Lakini pili wamesema, ikiwa maafikiano yameshindikana kwenye utafutaji wa Katiba Mpya, basi nguvu zielekezwe katika kufanyiwa marekebisho makubwa katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano.”

Kupatikana kwa habari hizi kumekuja wiki moja tangu kuvuja taarifa kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM), kiko mbioni kulegeza msimamo wake wa kung’ang’ania muundo wa Muungano wa serikali mbili.

Taarifa zinanukuu vyanzo vya ndani ya chama hicho kwamba, CCM imelazimika kuachana na mradi wake wa serikali mbili kwa hofu ya kukataliwa na wananchi katika uchaguzi mkuu wa mwaka kesho.

Tayari madhehebu ya dini ya kikristo nchini yameweka msimamo wa kutetea Rasimu ya Katiba Mpya ambayo katika muundo wa Muungano imependekeza uwe wa serikali tatu.

Kwa mujibu wa waraka wa UKAWA ulio mikononi mwa viongozi wakuu wa chama tawala na Msajili Mutungi, inapendekezwa kuwa “suala la muundo wa Muungano limezua mjadala na kuibua tofauti za kimtazamo na kiitikadi, wananchi wapewe fursa ya kupiga kura ya maoni kuamua uwepo wa serikali mbili au tatu.”

“Ni muhimu kukapigwa kura ya maoni kuhusu muundo wa Muungano. Hii itaufanya mjadala katika Sura ya Kwanza na Sura ya Sita ya Rasimu kufanyika bila mikwaruzo,” unaeleza waraka huo.

UKAWA wanasema, wakati hilo likisubiriwa, “Bunge la Jamhuri ya Muungano lifanye marekenbisho kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano kwa lengo la kuundwa upya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ili kuweka utaratibu wa kikatiba wa kukabidhiana madaraka mara baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu kutangazwa.”

Aidha, UKAWA wanaeleza, “Bunge la Jamhuri lifanye marekebisho makubwa ya Sheria ya Uchaguzi ili kuweka utaratibu unaofanana wa kuendesha na kusimamia chaguzi zote katika nchi.”

Viongozi wa UKAWA na CCM walikutana wiki iliyopita jijini Dar es Salam kujadili mustakabali wa Bunge Maalum la Katiba. Wanatarajiwa kukutana naye wiki hii.

 

error: Content is protected !!