May 9, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Ukawa wapigania wachimbaji wadogowadogo

Wachimbaji wadogo wadogo wa madini katika mgodi wa Mwadui

Spread the love

 

KAMATI ya kushughulikia mgogoro kati ya wananchi wa Nyamongo na Kampuni ya ACCACIA iliyoundwa na Sospeter Muhongo, Waziri wa Nishati na Madini imetakiwa kuharakisha utoaji wa taarifa ili kunusuru mauaji na majanga yanayowakabili wananchi hao, anaandika Regina Mkonde.    

Hayo yamesemwa leo Bungeni mjini Dodoma na  John Mnyika, Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani  Bungeni, Wizara ya Nishati na Madini wakati akitoa maoni juu ya mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2015/2016 na makadirio na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017.

Kambi Rasmi ya Upinzani inazo taarifa kuhusu Kamati ya Kupitia Matatizo yote yanayowakabili wananchi wa Nyamongo na Kampuni ya ACCACIA iliyoundwa na Mheshimiwa Waziri. Kambi Rasmi ya Upinzani inataka taarifa hiyo iharakishwe ili kunusuru majanga yasiendelee kwani tayari mauaji yanaendelea, ambapo kijana mmoja alipigwa risasi na askari hivi karibuni,” amesema Mnyika.

Amesema matokeo ya mgogoro huo ulioanza tangu mwaka 1994 ni wananchi kuuawa kila mara kwa kisingizio cha kuingia mgodini na kwamba hadi sasa watu zaidi ya 400 wameuawa huku wengine akibaki na ulemavu wa kudumu bila ya mgogoro huo kutafutiwa suluhisho.

“Wilaya ya Tarime ina mgodi wa North Mara ambao sasa unaitwa ACCACIA, ulianza rasmi mwaka 1994 lakini ulikuta wananchi katika eneo hilo la Nyamongo wakiwa wanachimba madini eneo la Nyarugusu na Nyabirama.

“Baada ya wawekezaji kupewa leseni, Dar es Salaam walitwaa eneo hilo bila kuwaachia  wananchi wa Tarime hata eneo la mita tano kuchimba,” amesema Mnyika.

Amesema licha ya mauwaji ya kikatili yanayofanywa, kitendo cha  ulipuaji wa miamba pia kimekuwa chanzo cha wananchi kukumbwa na athari za kiafya kutokana na vumbi kali, kupatwa kwa mistuko ya moyo na nyumba zao kuharibika kwa kuweka nyufa.

“Mgodi wa Nyamongo ni tofauti na migodi mingine uko, katikati ya makazi ya watu, hivyo wananchi walitakiwa kuhamishwa kwa kulipwa fidia ili kupisha shughuli za uchimbaji kama inavyosema Sheria ya madini ya mwaka 2010.

“Lakini hadi sasa watu wanaishi mita takriban mbili kutoka mgodini kinyume cha sheria inayosema wawe umbali wa mita 200 kutoka eneo la mgodi,” amesema.

Pia, Mnyika ameitaka serikali kupitia mkataba wa kufanya utafiti wa kampuni ya madini ya M/S HENAN AFRO ASI-GEO ENGINEERING (T) Co. LTD uliotakiwa kuisha mwezi wa Mei ambao Mkuu wa Wilaya alitoa kibali bila taratibu cha kuwaongezea muda wa utafiti huku ikifahamika kuwa utafiti huo umeharibu miundombinu ya barabara na mazingira.

“Aidha huko huko Musama Vijijini, Jimbo la Butiama kuna mgodi ambao upo katika kijiji cha Nyamikoma, Kata ya Kyanyari kuna Kampuni ya madini ya M/S HENAN AFRO ASI-GEO ENGINEERING (T) Co. LTD ambayo sasa ni takribani miaka 8 wanafanya utafiti na muda wa utafiti ulitakiwa umalizike mwaka huu mwezi wa Mei,” amesema na kuongezeka;

“Lakini Mkuu wa wilaya alitoa kibali bila ya utaratibu cha kuwaongezea muda wa utafiti kwa barua yake ya tarehe 27/4/2017 yenye Kumb. Na. AB. 128/270/01/A/66 kwenda kwa Afisa Tarafa wa Tarafa ya Makongoro. Utafiti huo umeharibu sana miundombinu ya barabara na mazingira.”

Mnyika amesema kilio hicho kipo pia katika mgodi wa Busekela Mkoa wa Mara, Wilaya ya Musoma Vijijini unaomilikiwa na Kampuni ya Dolphine Mines, lakini wachimbaji wanaozunguka mgodi huo wanasumbuliwa ingawa mgodi huo unajulikana ni wa wachimbaji wadogo.

Na kwamba serikali inashirikiana na Kampuni hiyo ya Dolphine kuwanyanyasa wachimbaji wadogo.

error: Content is protected !!