August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ukawa wapanga kummaliza Lipumba

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema Taifa

Spread the love

UMOJA wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umeeleza mikakati yake ili kuhakikisha Prof. Ibrahim Lipumba anafikia kifo chake cha kisiasa, anaandika Charles William.

Hatua zitakachochukuliwa ni pamoja na kutumia wanasheria wa vyama vyote vinavyounda umoja huo, kufungua kesi ili kumuondoa Ofisi Kuu za CUF, Buguruni jijini Dar es Salaam na hatimaye kuhitimisha zama zake katika siasa za Tanzania.

Vyama vinavyounda umoja huo ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha NCCR-Mageuzi na NLD.

Akitoa tamko la umoja huo mbele ya waandishi wa habari leo katika Hoteli ya Courtyard jijini Dar es Salaam, Freeman Mbowe, mwenyekiti mwenza wa Ukawa amesema, hatua hiyo itasaidia kuuweka umoja huo katika hali salama kwani Lipumba anatumiwa ili kuvuruga upinzani hapa nchini.

23 Septemba mwaka huu, Jaji Francis Mutungi, Msajili wa Vyama Vya Siasa alitangaza kumtambua Prof. Lipumba kuwa mwenyekiti halali wa Chama cha Wananchi (CUF), jambo lililozua mvutano huku chama hicho kikitangaza kumvua uanachama tarehe 27 Septemba, mwaka huu.

“Alichokifanya Lipumba mwaka jana, akiwa jemedari anayeongoza chama chake lakini akaamua kukisaliti chama na Ukawa tena katikati ya mapambano ni uhaini na katika nchi yoyote, iwe ya kidemokrasia au ya kidikteta, uhaini ni kosa ambalo adhabu yake ni kifo.

Sisi siyo mahakama au majaji. Sisi ni wanasiasa na kwa alichokifanya, tunamuhukumu kifo cha kisiasa,” amesema Freeman Mbowe, mwenyekiti wa Chadema kwa niaba ya viongozi wenzake wa Ukawa.

Mbowe alikuwa ameambatana na wenyeviti wenza wa Ukawa, James Mbatia (NCCR Mageuzi), Julius Mtatiro (CUF), Oscar Emmanuel (NLD) pamoja na makatibu wakuu wa vyama hivyo akiwemo Maalim Seif Sharrif Hamad (CUF), Dk. Vincent Mashinji (Chadema) na wengine.

Mbowe emeeleza kuwa viongozi wa Ukawa wamefanya kikao na kukubaliana kuwatumia wanasheria wa vyama hivyo kulishughulikia suala la Lipumba na kwamba wataanza kuchukua hatua mapema wiki ijayo.

“Tumekubaliana wanasheria wetu waanze kuchukua hatua, huu ni wakati muhimu wa kushikamana kuliko wakati wowote ule kwani huyu bwana anatumiwa na serikali ya CCM kwa kazi maalum. Hana lengo la kuivuruga CUF tu bali pia kuvuruga ushirikiano wa Ukawa,” amesema.

Kwa upande wake Mtatiro ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF Taifa amesema hoja za msajili kumrudisha Lipumba madarakani hazina mashiko yoyote kisheria na ndiyo maana chama hicho kimempuuza.

“Duniani kote mtu akishaandika barua ya kujiuzulu anakuwa amejiuzulu tayari, ndiyo maana Katiba ya CUF Ibara ya 117 (1) inasema; Kiongozi yoyote anaweza kujiuzulu wakati wowote….suala la kujiuzulu ni uamuzi na utashi wa mtu binafsi.

Ibara ya 117 (2) ya Katiba ya CUF, inazungumzia mamlaka iliyomchagua kiongozi kuidhinisha kujiuzulu kwake. Hiki ndicho tulichokifanya kwa kuitisha mkutano mkuu uliopiga kura za kuridhia kujiuzulu kwa Prof. Lipumba. Katiba ya CUF haielezi kuwa tulitakiwa kujibu barua yake,” amesema.

Mtatiro amesema CUF ilichukua hatua za kisheria zinazothibitisha kujiuzulu kwa Prof. Lipumba ikiwemo kuteua Kamati ya Uongozi Taifa chini ya Twaha Taslima na kueleza kuwa hata Msajili wa Vyama Vya Siasa aliidhinisha uamuzi huo na kuliweka jina la Taslima kama kiongozi wa CUF.

“Mpaka sasa tunavyozungumza, tovuti ya ofisi ya msajili bado imemuweka Taslima katika orodha ya viongozi wa CUF taifa, hii ina maana kuwa hata yeye alitambua kujiuzulu kwake na alikubaliana na hatua zilizochukuliwa na CUF,” amesema Mtatiro.

error: Content is protected !!