July 28, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Ukawa wamwinda Prof. Lipumba

Spread the love

WAKATI Prof. Ibrahim Lipumba akipiga kambi katika Ofisi Kuu ya chama hicho iliyopo Buguruni jijini Dar es Salaam, Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wajiandaa kumng’oa, anaandika Faki Sosi.

Taarifa zaidi kutoka kwenye umoja huo zinazeleza kuwa, kumekuwepo na mjadala kuhusu namna ya kuuokoa umoja huo ambao kwa sasa unatikiswa na Prof. Lipumba baada ya kurejea kwenye nafasi hiyo kupitia barua ya Jaji Francis Mutungi, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini.

Viongozi hao leo watakutana kujalidili namna ya kuuokoa umoja huo na kwamba, kupasuka kwa CUF kwa kiwango kikubwa kunatishia usalama wa umoja huo ambao umetoa matokeo mazuri kwenye Uchaguzi Mkuu wa tarehe 25 Oktoba mwaka jana.

“Mjadala utafanyika kwa kuwa, uhai wa CUF ndio uhai wa Ukawa,” kimeeleza chanzo chetu na kuongeza;
“Sio jambo rahisi kukubali Ukawa upasuke kutokana na mtu mmoja ambaye ni Prof. Lipumba, hapa lazima juhudi zifanyike.”

Mbele ya waandishi wa habari jana Mbowe alisema, Chadema inatambua mgogoro unaoendelea ndani ya CUF, unaomhusisha aliyekuwa Prof. Lipumba.
Freeman Mbowe jana amesema, Ukawa mpaka sasa haumtambua Prof. Lipumba kama mwenyekiti wa chama hicho wala mwenyekiti mwenza wa Ukawa kama ilivyokuwa awali.

Alisema, kwa kiwango kikubwa mgogoro huo umechangiwa na Jaji Mutungi kutokana na barua ama msisitizo wake wa kumtambua Prof. Lipumba kama mwenyekiti wa chama hicho licha ya kujiuzulu Agosti 2015.

“Jaji Mutungi anaivuruga CUF kwa kujaribu kumrudisha madarakani Prof. Lipumba, ambaye alijiuzulu madarakani katika mazingira yanayoashiria kununuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa lengo la kusaliti vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

“Chadema hatumtambui Prof. Lipumba kama Mwenyekiti wa CUF Taifa au Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, tunamtambua kama adui wa demokrasia na msaliti wa harakati za kudai haki katika nchi yetu.”

Jumanne tarehe 27 Septemba, 2016, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la Chama cha Wananchi (CUF), katika kikao cha dharura kilichofanyika Makao Makuu ya CUF, mjini Zanzibar lilimfukuza uanachama wa chama hicho Prof. Lipumba.

“Baraza Kuu linaweka bayana kwa wanachama wa CUF, Watanzania na mamlaka zote nchini kwamba kuanzia leo, Prof. Ibrahim Lipumba hana haki ya kujihusisha kwa namna yoyote ile na shughuli zozote za chama,” ilieleza taarifa ya CUF.

Aidha taarifa hiyo ilidokeza kuwa, uamuzi huo umechukuliwa baada ya baraza hilo kuridhika na mashtaka dhidi ya Prof. Lipumba kuongoza na kusimamia kikundi cha wahuni kuvamia Ofisi Kuu ya Chama, Buguruni, Dar es Salaam tarehe 24 Septemba, 2016 mwaka huu.

“Baraza kuu limetumia uwezo wake, kwa mujibu wa Ibara ya 10 (1) (c) na kwa kura zote 43 za wajumbe wake waliohudhuria kumfukuza uanachama Prof. Ibrahim Lipumba,” ilieleza taarifa hiyo.

error: Content is protected !!