September 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Ukawa wamwandama Rais Magufuli

Spread the love

RAIS John Magufuli anaandamwa, sasa anatakiwa kuwachukulia hatua wakurugenzi, watendaji na makatibu tawala wa mikoa waliosababisha kuwepo kwa watumishi hewa, anaandika Aisha Amran.

Wabunge na viongozi wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wamekuwa wakimtaka Rais Magufuli kuchukua hatua dhidi ya wale wanaofuja fedha za umma.

Safari hii Ruth Mollel, Waziri Kivuli na Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni-Ofisi ya Rais (Utumishi) amesema, endapo Rais Magufuli atashindwa kuwachukulia hatua watumishi hao, atakuwa hajatimiza wajibu wake.

Amesema, sababu inayochangia kuwepo kwa watumishi hewa ni udhaifu wa Tume ya Utumishi wa Umma kutohakiki mfumo wa rasilimali watu pia kukoseka kwa vitendea kazi ili watekeleze jukumu la kuhakiki watumishi wa umma na kisha kutoa taarifa kwa mamlaka husika.

Amesema “watumishi hewa ni tatizo la kutengenezwa kwa makusudi kwani mabilioni yanayopotea kila mwaka kutokana na malipo ya watumishi hewa yanakwenda kwenye mifuko binafsi ya viongozi na watendaji.”

Amesema, licha ya kelele na jitihada zote na taarifa rasmi za kila mwaka za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesaba za Serikali (CAG) kuonesha ukubwa na upana wa tatizo, hakuna kiongozi wala mtendaji wa idara ya serikali au taasisi ambaye amewajibishwa.

“Wakurugenzi watendaji wa Halmashauri za Serikali za Mitaa ndio waajiri wa watumishi katika halmashauri zao. Kwa sababu hiyo, Wakuu wa Mikoa na Wakurugenzi wa Halmashauri wanahusika moja kwa moja na uwepo wa watumishi hewa katika mikoa na katika halmashauri za serikali za mitaa.

“Hawa ndio ambao wamepewa jukumu na Rais Magufuli la kuwabaini watumishi hewa katika maeneo yao na kutoa taarifa,” amesema Mollel na kuongeza;

“Tunasubiri kuona hatua zitakazochukulia na Rais Magufuli dhidi ya wakuu wa mikoa na wakurugenzi wa halmashauri ambao kwa makusudi au kwa uzembe wao wamesababisha kuwepo kwa watumishi hewa katika mikoa na halmashauri zao.”

error: Content is protected !!