January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ukawa wamlipua Magufuli bungeni

Waziri wa Ujenzi Dr. John Magufuli akionnyesha michoro ya FLYOVER ambayo imekamilika kwaajili ya kufanyiwa kazi

Spread the love

VYAMA vinavyounda kundi la Umoja wa Katiba (Ukawa) vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi, vimemshambulia Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magofuli kuwa, amekuwa akiainisha miradi mingi ambayo utekelezaji wake haukamiliki kutokana na kupewa fedha ndogo na Serikali. Anaandika Edson Kamukara … (endelea).

Akisoma maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani, Waziri Kivuli wa Ujenzi, Felix Mkosamali aliainisha uamuzi wa Dk. Magufuli wa kununua kivuko cha Dar- Bagamoyo kwa takribani Sh. 4 bilioni, kinachobeba abiria 300 na kinatumia saa tatu kutoka Dar kwenda Bagamoyo, akisema ni upotevu wa fedha.

Mkosamali amesema inatia aibu kuona baadhi ya wabunge wakijitutumia kumpongeza Magufuli kwa utendaji kazi mzuri kwa kila wizara anayopita pasipo kuainisha udhaifu wa maamuzi yake ambayo yameligharimu taifa.

“Ni jambo la ajabu kununua kivuko cha kizamani au chakavu chenye spidi ndogo. Azam Bakhresa ana Meli inayotoka Dar kwenda Zanzibar kwa muda wa dakika 90 tu na inabeba abiria 500 na kwa taarifa tulizonazo, inauzwa kati ya Sh. bilioni 4 hadi 5.

“Kambi rasmi ya upinzni inaomba Bunge lako kuunda Tume kuchunguza ununuzi wa kivuko hiki kibovu na cha kizamani, kilichonunuliwa kwa bei kubwa huku kwa siku kikiweza kwenda Dar es Salaam na kurudi Bagamoyo mara moja tu,”amesema.

Kwa mujibu wa Mkosamali, kivuko hicho kimekosa abiria kwani wananchi wanaona bora kupanda daladala kuliko kivuko kinachotumia saa tatu.

Hata katika mchango wake wa jumla kwa bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2015/16, Mkosamali aligusia tena suala la kivuko akisema, miradi hiyo inapelekwa katika baadhi ya maeneo ya viongozi wakuu kwa upendeleo na kuacha mikoa mingine yenye mahitaji makubwa.

Madeni ya wakandarasi

Mkosamali amesema, katika mawasilisho ya Magufuli aliliambia Bunge kwamba kulikuwa na kikosi kazi cha kuhakiki madeni ambayo wizara mbalimbali zinadaiwa na wazabuni.

“Kambi upinzani inamtaka waziri alieleze Bunge kwamba, kile kikosi kazi kilichoundwa na wizara ya fedha ili kuhakiki uhalali wa madeni ya wizara yake, kimebaini inadaiwa kiasi gani na wakandarasi pamoja na wazabuni wengine?

Amefafanua kuwa wizara hiyo, imekuwa ikitengewa fedha nyingi za miradi ya maendeleo katika bajeti kuliko wizara zingine.

“Katika mwaka wa fedha wa 2014/2015, wizara ya ujenzi imetengewa jumla ya Sh.bilioni 662.2 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo. Hadi kufikia Januari, 2014 madeni ya makandarasi na washauri yalikua ni Sh.bilioni 663.9.

“Wizara ya Ujenzi mpaka sasa inadaiwa zaidi ya billion 800 na hakuna majibu juu ya ulipwaji wa madei hayo. Licha ya uwasilishwaji wa bajeti ya wizara hii kuwa na kelele na mbwembwe nyingi ukweli ni kwamba madeni ya wizara yanazidi fedha za maendeleo tunazaopitisha na Bunge lako,”amesema.

Mkosamali ameongeza, “hata kwa mwaka huu wa fedha, bajaeti ya maendeleo ni billion 890.6 kwa wizara na taasisi zilizo chini ya wizara huku madeni yakiwa zaidi ya bilioni 800.Hivyo hakuna uhalisia kati ya fedha za maendeleo zinazoombwa na madeni husika”.

Ameongeza kuwa, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Wakandarasi (CRB) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Contractors Association of Tanzania (CAT), Mhandisi Consolata Ngimbwa, alitoa kilio kwenye mkutano wa mashauriano na maonyesho uliofanyika 14 Mei,2015 kwenye ukumbi wa Mlimani City.

“Kwa uchungu mkubwa Mhandisi huyo aliueleza umma kwamba wakandarasi watatu wamekufa kutokana na msongo wa kudaiwa na watu waliokuwa wanatoa huduma katika kampuni zao, hii ni kutokana na Serikali kutowalipa madeni yao pale wanapomaliza kazi,”amenukuu Mkosamali.

Kuhusu miradi ya barabara, Mkosamali amesema, kila inapofika mwaka wa uchaguzi CCM imekuwa ikiahidi kujenga barabara kwa lengo la kupata kura tu, lakini haitimizi ujenzi wa barabara walizoahidi.

Nao baadhi ya wabunge waliochangia, Piter Msigwa, James Mbatia, John Cheyo, Abass Mtemvu na wengine, walizungumzia kwa kirefu kuhusu msonagamano jijini Dar es Salaam na kuitaka serikali ichukue hatua madhubuti za kumaliza tatizo hilo.

Katika hitimisho la hoja yake, waziri Magufuli alikiri hali ya msongamano kuwa tete na kuanisha mipango ya serikali ya upanuzi wa barabara na ujenzi wa madaraja na barabara za juu lakini akaonya kwamba wizara yake pekee haiwezi kumaliza tatizo hilo.

Pia kuhusu madeni ya wakandarasi, Magufuli amewathibitishia wabunge kwamba wakandarasi wote na hasa wa ndani watalipwa madeni yao yote kama ambavyo Rais Jakaya Kikwete ameahidi.

error: Content is protected !!