June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ukawa wamgomea Magufuli, Shein, Ulinzi mpaka bungeni

Spread the love

UMOJA wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umesema mipango yao ya kutomruhusu Rais Dk. John Magufuli kulihutubia Bunge akiwa na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, imefanikiwa. Anaandika Dany Tibason, Dodoma … (endelea).

Uamuzi huo umekuja baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kudharau barua yao ambayo ilielezea msimamo wao kuhusu mgogoro wa kikatiba na kisiasa unaotokana na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Mwenyekiti wa Umoja huo, Freeman Mbowe, amesema walimua kuzuia Rais Magufuli asihutubie Bunge kwa vile Dk. Shein, muda wake wa kuwa rais ulikwisha tangu Novemba 2 mwaka huu kwa hiyo hakustahili kuhudhuria Bunge hilo.

Amesema kuwa wameamua kufanya vile wakiamini kuwa ilikuwa sehemu muafaka ya kufikisha kilio chao kutokana na wageni mbalimbali waliohudhuria mkutano ule, wakitokea katika nchi za jumuiya ya kimataifa.

“Tulishangaa kumuona Dk. Shein, Pandu Amiri Kificho na Makamu wa Pili wa Rais wakiwa ndani ya Bunge wakati kikatiba hawana uhalali,” amesema Mbowe.

Amesema, baada ya kitendo kile hivi sasa umoja wa vyama hivyo, unatarajia kukutana ili kupeana mikakati ya kuendeleza mapambano ya ndani na nje ya nchi ya kudai haki.

“Uchaguzi wa Zanzibar hauwezi kutenganishwa kikatiba au kisiasa na uchaguzi mkuu wa Jamhuri ya muungano,” amesema Mbowe.

Mbowe amesema Ukawa hawako tayari kuinajisi Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuruhusu viongozi wasio halali kuingia bungeni.

Aidha, Mbowe amesema walitaka shughuli ya ufunguzi rasmi wa Bunge isitishwe kwa sasa na kuahirishwa hadi hapo Rais halali aliyechaguliwa na wananchi wa Zanzibar, Seif Sharrif Hamad, atakapotangazwa rasmi na kuapishwa.

Naye Mwenyekiti Mwenza, James Mbatia, amesema haijawahi kutokea katika historia ya Bunge tangu nchi hiyo ilipopata uhuru kwa vyombo vya dola kuingia ndani ya bunge na kuwatoa wabunge kwa nguvu.

“Wakati sisi tunatafuta majadiliano mezani ilikumaliza mgogoro huu wenzetu Chama Cha Mapinduzi (CCM), wameamua kutumia majeshi kukandamiza demokrasia,” amesema Mbatia.

Mbatia amesema kuwa hawatakaa kimya bali wataendelea kupigania matakwa ya wananchi hususan kwa upande wa Zanzibara.

“Kuna mambo mengi yanafanywa hovyo na CCM na wapinzani wamekuwa wakivumilia kwa sababu ya kumpenda mama Tanzania lakini hivi sasa wasijaribu kuharibu amani, utulivu na mshikamano uliopo,” amesema.

Mbatia, amesema kwa kawaida mtu anapodhulumiwa haki yake kila mara matokeo yake anachoka kwa hiyo kuna siku ataifuta haki yake hata kwa kusababisha kumwaga damu.

Ulinzi unatisha

Kabla ya kuanza shughuli hizo, muda wa asubuhi wakazi wa wa mji huo walikumbwa na taharuki baada mji huo kujaa askari kila kona huku wakiwa wamesheheni silaha.

Miongoni mwa maeneo hayo ni pamoja na Jengo la Bunge, ambako ulinzi uliimarishwa kwa kulizunguka jengo lote, uliwafanya baadhi ya wananchi kuingiwa na wasiwasi.

Wasiwasi wa wananchi hao ulizidi zaidi baada ya polisi hao kujitokeza kwa wingi hata katika maeneo ambayo wananchi walikuwa wakiendelea na shughuli zao zakujizalishia kiapato.

Vitisho ambavyo walikuwa wakivifanya polisi hao ni ama vile kuyacha magari ya maji ya washawasha karibu na maeneo yenye makundi ya watu.

Maeneo ambayo yalionekana magari hayo ni pamoja na karibu na uwanja wa ndege na nje ya viwanja vya Bunge, lililokuwa likitumika kwa maegesho ya magari na zaidi kulikuwa na magari ya wabunge pamoja na yawapembe wao.

Pia kulikuwa na magari aina la Landrover zilisheheni askari waliyokuwa na silaha, mabomu ya machozi na mbwa wakijipitisha pitisha katika maeneo mbalimbali ya mji huo.

Aidha, kuna maeneo ambayo huwa kwa siku za kawaida yamekuwa yakitumika kama maegesho ya magari lakini kwa juzi na jana polisi wameyapiga marufuku huku wakiwa wameegesha magari yao.

Maendeo hayo yalionekana kuwekwa vibao vilivyokuwa vimeandikwa ‘No Parking’ jambo ambalo limewashangaza baadhi ya watu waliyokuwa wamezoea kuyatumia maeneo hayo.

Wakati huohuo, Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu amesema Umoja wa Katiba ya Wanachi (Ukawa ) wamesikitishwa na kitendo cha serikali ya CCM kuonesha wazi jinsi walivyobaka na kuikanyaga demokrasia nchini.

Alitoa kauli hiyo aipokuwa akizungumza na MwanaHALISI Online muda mfupi baada ya kutoka bungeni baada ya kufukuzwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai baada ya wabunge wa umoja huo kupinga kitendo cha kuruhusiwa kwa Rais wa Zanzibar kuwa sehemu ya Bunge.

Lissu amesema imeonesha wazi kuwa serikali ya CCM ilivyo kuwa ikitumia mabavu ya kuvunja sheria waziwazi sambamba na kuvunja kanuni za bunge jambo ambalo ni hatari kwa afya ya nchi.

Akizungumzia kutoka kwao nje ya ukumbi wa Bunge amesema serikali ya CCM kwa kutumia kiti cha Spika walionekana kupanga mbinu chafu za kuwazima wabunge wa Ukawa ili wasiweze kufikisha hoja zao mbele za wananchi kupitia bunge hilo.

“Unaweza kuona kwamba serikali ya CCM inavyoweza kuvitumia vibaya vyombo vya dola, kwa utaratibu jinsi ulivyo ili kuruhusu watu waingie katika ukumbi wa bunge ni lazima kutengua kanuni ili watu waeze kuingia lakini kutokana na uovyo na ujinga mkubwa wa serikali ya CCM, ambayo haizingatii sheria na katiba imeweza kuleta askari wengi pamoja na majeshi kwa ajili ya kukabiliana na upinzani.

“Jambo kubwa na baya zaidi na la ajabu ni pale ambapo askali waliovaa magwanda ya polisi na jeshi wakiwa na silaha za moto walivyoweza kuingia katika ukumbi wa bunge kwa misingi ya kutaka kukabiliana na wabunge wa upinzani.

“Jambo hapa ni kwamba hata wao wanajua kuwa Dk. Shein siyo rais halali wa Zanziba lakini kwa ubishi wao wanalazimisha kufanya hivyo na kutokana na hali hiyo ndiyo maana serikali imekuwa ikitumia vyombo vya dola kwa ajili ya kuthibiti wabunge wa Upinzania ambao wametumwa na Umma wasitoe mawazo yao,” amesema Lissu.

Mbali na hilo amesema pamoja na kuwa wamezuiliwa kuendelea na bunge, kwa ajili ya kuwasilisha hoja zao kwa watanzania lakini watatumia mbinu nyingi za kufikisha ujumbe kwa jamii kwani kwa sasa kuna kila mikakati ya kuhakikisha wanataka kuuzima upinzani.

Akizungumzia kuhusu kanuni za bunge kwa sasa amesema kama ilivyo katiba ya sasa ilivyo na makosa kibao ndivyo na kanuni za bunge zinavyotakiwa kurekebishwa kwani kuna makosa mengi zaidi.

Kwa upande wao wabunge wa Zanzibar wamesema ni dhambi kubwa kwa Dk. Ali Mohamed Shein kuenedelea kung’ang’ania kukaa madarakani wakati muda wake umeisha jambo ambalo linaonesha wazi kuwa ni matumizi mabaya ya madaraka na dola yake.

“Inasikisha zaidi kuona jinsi Rais wa Zanzibar alivyokuwa siyo muungwana anajua kabisa kwamba hakushinda uchaguzi, lakini ikumbukwe wakati wa kuvunja baraza la wawakirishi wabunge wa CCM walimkataa Maalim Seif Shariff Hamad kama makamu wa kwanza wa rais asiingie katika bunge.

“Lakini kwa uungwana wa kiongozi huyo aliondoka wala hakuhudhuria kikao hicho lakini jambo la kushangaza huyu Dk. Shein amekomaa sasa inafikia hatua anazomewa bila kuwa na aibu sasa huo ni uongozi gani na anamuongoza nani,” amesema.

“Tunamuuliza Rais Magufuli, ni nani akapeleka vifaru na kuongeza askari wengi katika nchi za Zanzibar na ni kwa sababu gani.

“Kwa sasa hali ya Zanzibar si shwali kwani kila jambo sasa limelala kwani hata watalii hawaji kama ilivyokuwa mwanzo, mbali na hilo kuna hali ya sitofahamu ni kwani nguvu nyingi ya vyombo vya dola inaelekezwa Zanzibar,” amesema mmoja wa wabunge wa Zanzibar.

error: Content is protected !!