August 16, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ukawa waiangushia jumba bovu CCM

Spread the love

VYAMA vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) leo bungeni vimeeleza kuwa, chanzo kikubwa cha migogoro kwa wananchi ni Chama Cha Mapinduzi (CCM), anaandika Regina Mkonde.

Na kwamba, migogoro ya ardhi inayoendelea pia asilimia kubwa ya wananchi kuishi bila nyumba na makazi bora kumesababishwa na kutotekelezwa kwa Ilani ya Serikali ya CCM.

Hayo yamesemwa leo Bungeni mjini Dodoma na Wilfred Lwakatare, Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wakati wa hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017.

“Kwa hali ya mazingira yalivyo hivi sasa hususani unapozungumzia taswira inayolizunguka suala la usimamiaji, uratibu na upangaji mipango inayohusu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ndani ya nchi yetu, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni bila kumung’unya maneno inao uthubutu wa kutamka wazi kuwa…

“Migogoro inayoendelea inayohusu ardhi na asilimia kubwa ya watanzania kuendelea kuishi bila nyumba na makazi yaliyo bora na yenye kuheshimika ni kushindwa kutekelezeka kivitendo kwa sera na ilani ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi,” amesema Lwakatare.

Lwakatare amesema, sehemu kubwa ya ardhi imeendelea kuporwa na kuwekwa kwenye miliki ya watu wachache na miongoni mwa hao wakiwa ni wamiliki wa kigeni kitendo kilichosababishwa na mfumo wa kinyonyaji uliolelewa na CCM.

“Chini ya Mfumo komavu uliojaa ghiliba, ufisadi, rushwa, uonevu, ubinafsi na unyonyaji uliolelewa na kuzidi kulindwa na Serikali ya CCM na Taasisi zake haviwezi kutoa mrejesho chanya wala kuondolewa na Mheshimiwa Lukuvi pekee au watu wachache wenye nia thabiti na utashi wa kuleta mabadiliko hata kama wangelikuwa na nia njema ya kufanya hivyo,” amesema na kuongeza;

“Kwenye hotuba ya Halima Mdee aliyekuwa msemaji Mkuu wa Wizara hii iliyohitimisha Bunge la kumi iliyofanyiwa utafiti kwa mapana na uwazi, ilionesha kuwa migogopro ya ardhi iliendelea kutamalaki lakini pia ilionekana dhahiri kuielemea serikali ya CCM.”

Amesema, katika hotuba hiyo ilionyesha ufisadi mkubwa uliokuwa ukiendelea ndani ya sekta ya mambo ya ardhi na makazi, na kwamba migogoro na matatizo hayo yameshindwa kupatiwa ufumbuzi huku mengine mapya yakiendelea kuibuka.

Amesema kuwa, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatoa ushauri kwa mamlaka za usimamizi, watumiaji wa ardhi, taasisi pamoja na makundi ya wadau mbalimbali yanayowakilisha watumiaji wa ardhi kukaa na kuibeba agenda moja ya kukubali kuunganisha mawazo ya namna ya kujipanga upya ili kuondoa changamoto hizo.

“Ni vema wadau, watumiaji wa ardhi na taaisi wafikiri kwa umakini wa hali ya juu na kuweka mipango na sera mahususi za Kitaifa zenye kujaa na kutawaliwa na dhana sahihi za fikra za uzalendo na Utaifa ili kuondoa migogoro ya ardhi katika nchi yetu,” amesema.

Lwakatare amesema kufanyika hivyo kutasaidia kujenga dira sahihi ya mipango bora, mizuri, endelevu na ya muda mrefu ya matumizi bora ya ardhi iliyopo kwa kizazi cha sasa na cha baadae.

“Ardhi tuliyotunukiwa kama watanzania na Mwenyezi Mungu ni hii tuliyonayo mkononi na wala haitazaliana, na wakati wa kuipanga ni sasa na wala tusiendelee kuogelea kwenye makosa ya wale waliotutangulia,” amesema.

Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani imeishauri serikali kufanya mapinduzi makubwa ya kimfumo yanayoweza kutoa dira sahihi ya utengenezaji wa mipango mizuri na inayotekelezeka ya upangaji mzuri wa mtumizi ya ardhi ya nchi yetu.

error: Content is protected !!