June 17, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Ukawa: Tutailiza CCM

Spread the love

 

UMOJA wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umejipanga kukiliza tena Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika kinyang’anyiro cha kumpata Meya wa Manispaa ya Kinondoni na Ubungo, anaandika Shabani Matutu.

Hayo yamebainishwa leo na Boniface Jacob, aliyekuwa Meya wa Kinondoni, mbele ya waandishi wa habari ambapo amesisitiza kwamba, Ukawa itashinda uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni kutokana na wingi wa wajumbe wao.

Amesema, wanatambua kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kina fitina na hujuma nyingi lakini wao hawana wasiwasi kwani wamejipanga vizuri kuzitwaa halmashauri hizo.

“Tuna idadi ya kutosha ya wajumbe watakaopiga kura katika sehemu zote mbili hivyo hatuna wasiwasi ingawa tunatambua kutakuwepo kwa hujuma kutoka CCM ambazo hazitasaidia kutokana na umoja tulionao,” ameeleza.

Amewataja wajumbe watakaoshiriki kwenye uchaguzi huo kwa upande wa Kinondoni ni 36 ambapo CCM ina wajumbe 16 ukilinganisha na Ukawa ambao wana wajumbe 23.

“Wajumbe hao 16 wa CCM ni pamoja na wajumbe wa viti maalumu wakiwemo Naibu Spika Tulia Ackson, Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje, na Profesa Makame Mbarawa, Waziri wa Ujenzi,” amesema.

Meya huyo amefafanua kuwa, upande wa Ubungo, Ukawa wananafasi kubwa ya ushindi kwani kati ya wajumbe 20, Ukawa ina wajumbe 12 na CCM ina wajumbe 4 pekee.

Boniface amesema anajivunia kipindi cha miezi saba ya uongozi wake kama Meya wa Manispaa ya Kinondoni kwani wamefanikiwa kukusanya mapato ya ndani ya Halmashauri hiyo zaidi ya bilioni 67 kutoka bilioni 45 zilizokuwa zikikusanywa chini ya CCM.

Amesema kipindi chake cha uongozi licha ya kuongeza mapato hayo lakini pia ameweza kutenga bilioni 110 ambazo zilizopelekwa katika miradi ya maendeleo ikilinganishwa na hapo awali ambapo zilikuwa zikitengwa bilioni 65 pekee.

error: Content is protected !!