January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

UKAWA: Mbele kwa mbele

Viongozi wa Umoja wa Wadai Katiba ya Wananchi (UKAWA) wakijadili jambo bungeni

Spread the love

MUUNGANO wa vyama thabiti vya upinzani nchini, umevuna maelfu ya wenyeviti na wajumbe wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji katika uchaguzi uliyofanyika 14 Desemba 2014.

Haya ni matokeo yenye kuashiria ishara njema ya kufanya vizuri katika uchaguzi mkuu, unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2015.

Matokeo haya, ni tofauti na yale ya uchaguzi wa mwaka 2009, ambapo Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilipata asilimia 91.72 ya viti, huku wapinzani wakigawana asilimia 8.28.

Safari hii, wagombea wa upinzani wanaunda Umoja wa Kutetea Katiba ya Wananchi (UKAWA),  wamekubalika zaidi, ukilinganisha na wale wa CCM.

Ushirikiano wa vyama hivyo, ndiyo umekitikisa chama kilichopo ikulu kwa zaidi ya miaka 53.

Safari ya anguko la CCM, limeanza taratibu. Limeanzia katika vitongoji, vijiji na mitaa. Yawezekana wenye chama chao hawajaliona hili. Ndiyo sababu, hawangalii idadi kubwa ya viti walivyopoteza, bali wanaangalia walivyobakisha.

Ni wazi kuwa katika uchaguzi huu, UKAWA wangefanya vizuri zaidi kama CCM wasingefanya hila. Kama vyombo vya dola, visingejigeuza chama cha siasa.

Ni muhimu vyombo vya dola hususani, jeshi la polisi na usalama wa taifa, vikabaki waangaliaji wa usalama wa raia na mali zao. Basi! Vyama viachwe kunadisha sera zao.

Ni ukweli usiopingika kuwa, kulegalega kwa mfanyabiashara mmoja mmoja, hutoa fursa ya kujijenga kwa mfanyabiashara mwingine.

Ndivyo UKAWA ulivyojijenga kwa kutumia ombwe la uongozi lililoletwa na CCM. Wameonyesha wako makini zaidi kulinganisha na walioko madarakani.

Ni muhimu ushirikiano huu ukalindwa, mithili ya mboni ya jicho.

Mwandishi wa Makala hii ni Ally Maneno anapatikana kwa kupitia 0754-356 333, 0716-356 333.

error: Content is protected !!