July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

UKAWA: Lowassa mtu safi, wamkaribisha rasmi

Wenyeviti Wenza wa UKAWA, kutoka kushoto ni Freeman Mbowe (Chadema), Prof. Ibrahim Lipumba (CUF), James Mbatia (NCCR-Mageuzi) na Emmanuel Makaidi (NLD).

Spread the love

UMOJA wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), umemkaribisha Edward Lowassa, Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa jimbo la Monduli kujiunga na umoja huo. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Rai ya kumtaka Lowassa kujiunga na UKAWA imetolewa leo Makao Makuu ya CUF, jijini Dar es Salaam katika mkutano uliohudhuriwa na Wenyeviti wenza wa UKAWA, Freeman Mbowe (Chadema), Emmanuel Makaidi (NLD), Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) na James Mbatia (NCCR – Mageuzi).

Mbali na kumkaribisha Lowassa, UKAWA wamesema mgombea urais kwa tiketi ya umoja huo atatangazwa wiki ijayo.

Akizungumza katika mkutano huo Mbatia amesema, “Tunachukua fursa hii kipekee kumwalika Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa jimbo la Monduli, Mheshimiwa Edward Lowassa ajiunge na UKAWA na tuko tayari kushirikiana naye katika kuhakikisha kuwa tunaiondoa CCM madarakani katika uchaguzi mkuu ujao.”

“Tunaamini Mheshimiwa Lowassa ana uwezo wa kuhamasisha umma kuikataa CCM yenye kusimamia mifumo isiyotenda haki. Ni mchapa kazi makini na mfuatiliaji wa karibu wa utendaji katika majukumu anayokabidhiwa,” amesema Mbatia.

Mbatia amesema hatua ya Lowassa kukaribishwa UKAWA imekuja baada ya Watanzania kushuhudia hadaa, udhalilishaji, upendeleo na ukandamizaji katika mchakato wa kupata mgombea urais kwa tiketi ya CCM. Pia kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa taratibu, kanuni na katiba ya chama hicho.

Pia, katika kujenga mshikamano ndani na nje ya vyama hivyo kuelekea na baada ya uchaguzi mkuu katika kuleta mabadiliko yatakayo toa katiba bora na kufikia maendeleo yatakayojenga demokrasia ya kweli na kuachana na uonevu, udhalilishaji, fitna na majungu yanayoendeshwa na CCM.

Akizungumza kuhusu harakati zilizokuwa zikiendeshwa kwamba “Lowassa ni fisadi na hasafishiki” Lipumba amesema, “…masuala ya ufisadi ni masuala ya mfumo. Lowassa alitoka madarakani mwaka 2008. Lakini mpaka sasa ufisadi bado umeendelea kukua kwa kasi licha ya Lowassa kutokuwa serikalini.”

“Mpaka sasa hakuna mashtaka mahakamani dhidi ya Lowassa. Tunawakaribisha Watanznia wote kujiunga na UKAWA kupitia chama chochote. Na zoezi hili ni lazima lifuate taratibu zetu ndani ya vyama,” amesisitiza Lipumba.

error: Content is protected !!