August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ukawa kuidhibiti NEC, Lipumba uchaguzi Dimani

Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa (Wakwanza) na Maalim Seif Sharif Hamad, Katibu Mkuu wa chama cha wananchi CUF.

Spread the love

VYAMA vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), vimejipanga kudhibiti hila za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Prof. Ibrahim Lipumba kukihujumu Chama Cha Wananchi – CUF katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Dimani, Zanzibar, anaandika Pendo Omary.

NEC kupitia Ramadhani Kailima ambaye ni mkurugenzi wake imetoa maelekezo kuwa mgombea akayesimamishwa na CUF katika uchaguzi huo ni sharti aungwe mkono na katibu mkuu na mwenyekiti wa chama hicho – Maalim Seif Sharif na Prof. Lipumba jambo ambalo ni gumu kutekelezeka.

Tayari Nasoro Ahmed Mazrui Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar amesema, hawawezi kushiriki katika uchaguzi huo kwa kufuata tamko lililotolewa na Kailima ambapo tarehe 8 mwezi huu alisema “fomu za wagombea wa CUF katika uchaguzi wa Dimani zitapaswa kusainiwa na pande mbili zilizo na mgogoro wa uongozi.”

Mgogoro unaoendelea ndani ya CUF ni juu ya Prof. Lipumba aliyejiuzulu uenyekiti wa chama hicho Agosti 2015 lakini Juni 2016 akatangaza kutengua uamuzi wake na kuirejea nafasi hiyo huku uongozi wa CUF chini ya Maalim Seif ukipinga na hatimaye kumvua uanachama lakini ameendelea kutambulika na Msajili wa Vyama vya Siasa.

“Tutashiriki katika uchaguzi kwa kufuata sheria na katiba ya CUF na si tamko la NEC kwani kwa mujibu wa Katiba yetu, mgombea anateuliwa na Baraza Kuu la chama na fomu yake inayopelekwa NEC inawekwa sahihi na katibu wa wilaya husika.

“Tayari tumepata majina ya wagombea, kesho Baraza Kuu litapitisha jina moja lakini Ukawa bado ina nafasi ya kutoa ushauri kuhusu kusimamisha mgombea hata kama atatoka chama kingine washirika hamna ubaya,” amesema Mazrui.

Taarifa zaidi zimeeleza kuwa ili kukabiliana na hila za NEC na Lipumba ambapo huenda mgombea wa CUF akaondolewa katika uchaguzi huo kwa kisingizio kuwa hajaridhiwa na upande wa pili wa mgogoro, Chadema inasuburi maelekezo kutoka CUF ili kusimamisha mgombea ili kuhakikisha CCM haipiti bila kupingwa.

Mariam Msabaha, mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar ameiambia MwanaHALISI Online kuwa wao ni washirika wa Ukawa na watahakikisha wanaisaidia CUF inapata ushindi katika uchaguzi wa Dimani.

“Tumekuwa na majadiliano ya muda mrefu kuhusu namna ya kuvuka vihunzi vilivyowekwa na NEC ikiwezekana kusimamisha mgombea kama CUF watatutaka tufanye hivyo ingawa kwa sasa tumekubaliana CUF waendelee na mchakato wa kutafuta mgombea wao,” amesema.

Uchaguzi huo Mdogo wa Jimbo la Dimani unafanyika kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Hafidh Ali Twahir (CCM), aliyefariki dunia tarehe 11 Novemba mwaka huu katika Hospitali ya Rufaa mkoani Dodoma.

error: Content is protected !!