August 4, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Ukatili watikisa maendeleo Tarime 

Spread the love

VITENDO vya ukatili vinavyofanyika mkoani Mara, vimetajwa kusababisha shughuli mbalimbali za maendeleo kukwama, anaandika Moses Mseti. 

Ni kutokana na wanawake kutelekezwa na kunyimwa haki na waume zao jambo ambalo limekuwa likilalamikiwa na wadau wa maendeleo. 

Hayo yameelezwa jana na Yassin Ally, Mkurugenzi wa Shirika la Kutetea Haki za Wanawake (Kivulini) wakati wa mafunzo ya siku moja kwa wazee wa mila kutoka kabila la Kikurya, yaliyohusu kulinda haki za mwanamke.

Ally amesema kuwa mkoa wa Mara unaongoza kwa vitendo vya ukatili vinavyofanywa kwa  watoto wa kike na wanawake, kitendo ambacho kimesababisha shughuli nyingi za maendeleo kurudi nyuma ikiwemo elimu.

Amesema kuwa, Mkoa wa Mara unaongoza kwa asilimia 60 kitaifa katika vitendo vya ukatali, kutokana na mila na desturi ikiwemo ya kukeketa watoto wa kike.

Ally amesema kuwa, mkoa huo umekuwa ukitukuza mila nyingi, ikiwemo ile ya ya saiga (rika) kwa wanaume waliofanyiwa jado mwaka mmoja, kuweka utaratibu wao na miongozo yao katika maisha yao.

“Saiga (rika) sio mila ya Kikurya na wao wameiga kutoka nje, lakini hali hii imesababisha watu kufanya uhalifu mkubwa, licha ya shughuli za maendeleo zinazoelezwa kufanywa na saiga, hivyo nilazima kutokomeza vitendo hivi,” amesema Ally.

Hata hivyo, amesema shirika lake limefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupunguza kwa kiasi kikubwa vitendo vya ukatili kwa wanawake katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa ikilinganishwa na wali.

Nashony Marwa, Diwani wa Kata ya Nganyange amesema kuwa, saiga (rika) imekuwa ikirudisha nyuma shughuli za maendeleo kwenye kata hiyo na kwamba, wamejipanga kuelimisha jamii ili kuacha na mila hizo.

Bululwe Makange, Mzee wa Kimila amesema kuwa, mwanasaiga (rika moja) anapokiuka masharti yao, hulala chini huku mke wake akiwa amelala kitandani pia atalazimika kula ugali wa mtama na mboga bila chumvi.

“Saiga akitaka kurudi kama atakuwa ametekeleza masharti ni lazima atengeneze pombe ya kienyeji na kuwachinjia ng`ombe ama mbuzi na kama asipofuanya hivyo, wenzake tunamlani na kutengwa kwenye shughuli za maendeleo,” amesema Makange.

Mafunzo hayo pia yaliwashirikisha watendaji wa kata, Kitengo cha Dawati la Jinsi cha Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Tarime mkoani Mara pamoja na madiwani wa wilaya hiyo.

 

error: Content is protected !!