July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ukata wakwamisha rufaa za Mdee, wenzake Chadema

Spread the love

 

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema, kimeshindwa kuitisha kikao cha baraza lake kuu, kwa ajili ya kusikiliza rufaa ya Halima Mdee na wenzake 18, ya kupinga kufukuzwa ndani ya chama hicho kutokana na kutokuwa na fedha. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Kauli hiyo imetolewa jana Alhamisi, tarehe 15 Julai 2021 na Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, Tundu Lissu, katika mjadala uliofanyika kwenye mtandao wa Club House, baada ya kuulizwa na Mwanahabari wa Tanzania, Absalom Kibanda, kwa nini wanachelewa kutoa uamuzi wa rufaa hizo.

Katika mjadala huo, Kibanda alisema kitendo cha Chadema kuchelewa kutoa maamuzi ya rufaa hizo zilizowasilishwa ndani ya chama hicho, Desemba 2020 na wanachama hao, kinawanyima haki.

“…haki ikichelewa ni kuiminya, ni kweli sisi hatutakuwa wa kwanza kuahirisha kesi katika nchi hii. Sisi tunaweza sema hatukuwa na hela za kuitisha baraza kuu kwa ajili tu ya kusikiliza rufaa ya hawa wanachama wetu wa zamani,” amesema Lissu.

Lissu amesema, Chadema ikiwa tayari itaitisha kikao cha baraza hilo, kwani ni utaratibu wake wa kufanya jambo hilo kila mwaka.

“Baraza linakaa kwa mwaka mara moja, kufanya ajenda za mwaka mzima. Tutaitisha baraza kuu sababu ni sehemu ya ratiba ya baraza ya kila mwaka, Chadema tunaitisha kupitisha mambo mengi ya chama ikiwemo kusikiliza rufaa zao,”amesema Lissu.

Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti Chadema

Mbali na Mdee, wengine waliokata rufaa kupinga kutimuliwa Chadema ni, waliokuwa viongozi wa Bawacha, Hawa Mwaifunga (Makamu Mwenyekiti). Grace Tendega (Katibu Mkuu). Jesca Kishoa (Naibu Katibu Mkuu) na Agnesta Lambart (Katibu Mwenezi).

Wengine ni, waliokuwa wajumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Ester Bulaya na Esther Matiko, pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mtwara, Tunza Malapo.

Pamoja na Cecilia Pareso, Asia Mwadin Mohamed, Felister Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Siyao, Salome Makamba, Anatropita Theonest na Conchesta Lwamlaza.

Wanasiasa hao walifukuzwa Chadema tarhe 27 Novemba 2020, siku mbili baada ya kuapishwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai, kuwa wabunge viti maalumu, tarehe 24 Novemba 2020, katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma.

Wabunge hao walitimuliwa kwa kosa la usaliti, kufuatia hatua yao ya kukubali ubunge viti maalumu, kinyume na msimamo wa Chadema, wa kutopelekea wawakilishi bungeni wakipinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Chadema kilipinga matokeo ya uchaguzi huo kwa madai kwamba mchakato wake haukuwa huru na wa haki. Hata hivyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imekanusha madai hayo ikisema ilisimamia uchaguzi kwa huo kwa mujibu wa sheria.

Katika matokeo ya uchaguzi huo yaliyotangazwa na NEC, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilifanikiwa kushinda kiti cha urais pamoja na kuzoa viti vya ubunge zaidi ya 300, huku vyama vya upinzani vikiambulia viti sita vya ubunge wa jimbo na wabunge viti maalumu 19.

error: Content is protected !!