August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ujumbe wa Chadema Ujerumani kurejea kesho

Spread the love

ZIARA ya siku 6 ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), nchini Ujerumani inamalizika leo, hivyo ujumbe wa viongozi hao unaoongozwa na Dk. Vincent Mashinji, Katibu Mkuu wa chama hicho, unatarajia kurejea nchini siku ya kesho, anaandika Charles William.

Jumla ya viongozi 10 wa Chadema wakiwemo wabunge watano, wapo nchini Ujerumani tangu tarehe 18 Septemba mwaka huu katika ziara ya kikazi ambapo Ijumaa ya kesho tarehe 23 Septemba, 2016 watarejea hapa nchini.

Anatropia Theonest, mmoja kati ya viongozi wa Chadema waliopo nchini Ujerumani, ameieleza MwanaHALISI online kwa kifupi kuwa, “tutarejea Tanzania siku ya kesho.”

Waliopo kwenye msafara huo ni pamoja na John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu (Bara), Prof. Mwesiga Baregu, Mjumbe wa Kamati Kuu, Tundu Lissu, Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, John Mrema, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki na Mambo ya Nje, Benson Kigaila, Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama.

Sambamba na Lissu kushiriki ziara ya Chadema nchini Ujerumani lakini pia wadhamini wake katika kesi ya uchochezi inayomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, waliieleza mahakama hiyo siku ya jana kuwa Lissu yupo nchini humo kwa matibabu.

Wengine katika ziara hiyo ni Zeudi Mvano, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Zanzibar), Ruth Molel, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Pwani, Cecilia Paresso, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Arusha na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Ilala, Anatropia Theonest.

Viongozi hao waliitembelea Wizara ya Mambo ya Nje ya Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani, na kufanya mazungumzo na wizara hiyo lakini pia walifika katika ofisi za Wizara ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo ya nchi hiyo na kufanya mazungumzo na wizara hiyo.

Katika hatua nyingine, viongozi hao wamekutana na kufanya mazungumzo na wabunge wa Bunge la Shirikisho la Ujerumani na kisha kukutana na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini humo ili kubadilishana uzoefu wa masuala mbalimbali.

 

error: Content is protected !!