Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Ujumbe mzito wa kifo cha Masogange
Habari za SiasaMichezoTangulizi

Ujumbe mzito wa kifo cha Masogange

Mwili wa Agnes Gerrald 'Masogange' ukiagwa Leaders, Dar es Salaam
Spread the love

JULIUS Mtatiro, Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF ameandika ujumbe mzito wenye kufikirisha wengi juu ya msiba wa Agnes Gerrald “Masogange.’

Mtatiro ameandika ujumbe huo kwenye ukurasa wake wa Facebook, akieleza maisha ya mrembo huyo huku akiwataja baadhi ya watu ambao walimtumia vibaya binti huyo na kumwacha anafariki bila kula matunda yake.

Soma kwa kina ujumbe huo mzito wa Mtatiro:-

KWAHERI MASOGANGE … HATUKUKUTENDEA HAKI!

Ndugu zangu, uvumilivu umenishinda na nikaona lazima niandike jambo. Ni kawaida yetu kwenye taifa letu kuandika kurasa nyingi za wasifu wa wanasiasa, watumishi wa umma “waliotukuka”, matajiri na watu tunaodhani waligusa maisha ya jamii kwa njia sahihi kila wanapofariki.

Ni kawaida yetu pia kuwahukumu marehemu wengine, bila kuwajua, wakifa tunaishia kutangaza yale tuliyodhani ni maovu yao bila kujiuliza tuliweka mchango gani kwao.

Wapo watu wengine hufa, tukadhani hawana maana, ni wadhambi, hawana mchango kwenye jamii na hawapaswi kuigwa hata kidogo. Kumbe vifo vyao ni kioo kikubwa cha maisha yetu, ni funzo kubwa na ni tafakari halisi ya sisi ni nani.

Tangu dada yetu Agnes Gerald (Agnes Masogange) afariki, nimeona kwenye mitandao mingi watu wakimzungumzia vile watakavyo. Hiyo ni kawaida. Sehemu kubwa ya wanaomzungumzia wanaeleza namna ambavyo hakuishi maisha mema na hakuwa kioo cha jamii.

Mimi sikuwahi kukutana na Agnes zaidi ya kumuona mitandaoni, mara ya kwanza kupitia video ya mwanamuziki “Bele 9”, tangu hapo nilimuona kama msichana mwenye vituko na visa vingi, tangu kuchezesha viungo vyake bila nguo hadi kuhusishwa na tuhuma za madawa ya kulevya.

Katika safari yote hiyo binafsi sikuwahi kumhukumu, maana nilijua chanzo cha yote hayo ni kukosa elimu bora (ya darasani), elimu bora ya uraia na elimu bora ya maadili. Chanzo cha kukosa vitu hivyo ni familia yake, ndugu zake, marafiki zake, serikali yake na wote tuliomzunguka.

Kwa kipaji cha Agnes, tangu kinachomozwa kwenye wimbo wa Bele 9, umbo lake na haiba yake – kama tungelikuwa na taifa lenye maandalizi na vijana walioandaliwa, Agnes tumuagaye na kuelekea kumzika labda angelikufa akiwa Agnes mshindi wa tuzo ya Oscar kwenye Muziki, Uigizaji, Uhamasishaji Jamii, Uburudishaji n.k.

Lakini tunaenda kumzika Agnes na vipaji vyake sahihi ambavyo aliwahi kuvichomoza, vikageuzwa kuwa faida kwa wengine kwa njia nyingine, vikaharibiwa, akavishwa taswira ya picha chafu mitandaoni na madawa ya kulevya.

Naamini, kipaji cha Agnes kilipochomoza tu, wajanja walimuwahi, wengine wakiwa watu wakubwa tu, wengine wakiwa na nyadhifa kubwa tu, wengine wakiwa na elimu kubwa tu, wengine wakiwa na fedha nyingi tu na wengine wakiwa na vipaji vikubwa zaidi.

Dada yetu huyu najua alikimbiliwa na kutumiwa na sisi sisi, kila mmoja wetu akimtumia kwa maslahi yake.

Agnes aliwahi kukutwa na kemikali ambazo haziruhusiwi kusafirishwa, alikamatiwa Afrika Kusini, baadaye aliachiwa. Zile kemikali zilikuwa ni za nani? Kwa alimpa Agnes? Je tulimfuatilia (maana naambiwa yuko hapa Tanzania) na ni mtu mkubwa tu, ana hela nyingi tu na ana elimu ya kutosha! Taifa zima likamhukumu Agnes, tukamuita muuza madawa; mtu mwenye mamlaka (mmiliki wa kemikali hizo) hadi leo anatembea barabarani akitamba, Agnes yuko kwenye jeneza na jamii ikihukumu matendo yake!

Kuna wakati video ya Agnes ilionekana mitandaoni akiwa anacheza na nguo za ndani tu. Aliyekuwa anarekodi video ile alikuwa anampa maelekezo “…bebi sogea hivi, cheza hivi, fanya vile…” Agnes anatekeleza!

Video ile ikazua gumzo, bila shaka aliyeilikisha mitandaoni kwa sababu zozote zile ni huyu mwanaume ambaye anaweza kuwa mpenzi wa wakati huo wa Agnes. Kwa kutojali na kutotambua umuhimu wa vijana wetu (serikali/taifa), hatukuwahi kusikia mwanaume huyo amehojiwa, hatukuwahi kusikia akihukumiwa na hatukuwahi kuona Agnes akilipwa fidia ya udhalilishaji ule uliomuonesha kama msichana mdhambi. Sana sana ambaye alitukanwa na kuhukumiwa na taifa ni Agnes, huyo mwanaume yuko “SALAMA!” na huenda anaendelea kurekodi wasichana wengine.

Tumo kwenye taifa ambalo halijui kulinda vijana wake kwa kutatua mizizi na vyanzo vya matatizo yao. Tumo kwenye taifa ambalo, vijana wanakamatwa kwa tuhuma za kutumia madawa ya kulevya huku wasambazaji na wenye mitaji ya uingizaji wa madawa hayo wakiwa ni wafadhili wakubwa wa vyama vyetu na kutusaidia kuingia serikalini. Sisi ni wapumbavu sana!

Upumbavu wetu ndiyo unafanya vijana wetu wanakufa na vipaji vyao huku sisi kama taifa tukiendelea kushindwa kuwanyanyua na kuwasaidia, sana sana tukiingilia vipaji vyao, tunavitumia kwa maslahi yetu, waje kuimba kwenye matamasha na wawe wanachama wa vyama vyetu, na huko tunawatumia tutakavyo, mwisho wa siku hawatambuliki.

Ndiyo maana kwa hawa wasanii wetu, ni wachache mno ndiyo wana mafanikio, wengi wamo kwenye sanaa kuwanufaisha watu wengine. Angalia wachezaji wetu, wengi hustaafu michezo yao wakiwa hawajui watakula nini. Sababu ya yote haya ni taifa letu kutokuwa na mpango unaotekelezeka wa kuwasaidia vijana kuinuka kutoka chini ni kung’arisha vipaji vyao.

Kifo cha Masogange kimeniumiza kwa sababu kinajenga taswira za maisha ya ndani ya vijana wengi wa taifa letu, taswira ya kutwishwa mizigo mizito wakiwa wadogo, kuharibiwa, kutelekezwa, kujitafutia maisha, kuonesha vipaji vyao na vipaji hivyo kutumiwa na watu wengine kwa manufaa ya watu hao huku vijana wetu wakibaki na taswira hasi na kuonekana ni wavunja maadili.

Namheshimu Binti Agnes kwa sababu naamini hakupaswa kufa akiwa Masogange huyu atafsiriwaye na watu wenye mitizano hasi. Naamini Agnes alinyimwa fursa na usimamizi wa kila mtu (familia, marafiki, ndugu na taifa).

Nimemuona Baba ya Agnes akisema alikosana na mwanaye tangu alipopata ujauzito na kuacha shule akiwa kidato cha 2. Baba ya Masogange alijua kuwa “…mtoto wako akipata mimba shuleni suluhisho ni kumfukuza nyumbani”, ndivyo mababa wengi wa zamani waliamini na ndivyo hata baadhi ya viongozi wakubwa wa sasa wanaamini. (Yupo kiongozi amesema mwanafunzi akipata mimba asisomeshwe tena).

Pamoja na kuishia kidato cha pili na kutelekezwa na familia yake naambiwa ya kuwa, hata baba ya mwanaye alimtelekeza. Masogange akaanza kupambana kivyake.

Video ya Bele 9 ikamtambulisha kwa watanzania, alirudi na kusimama kwa msaada wa watu wema lakini tokea hapo akakosa usimamizi na menejimenti.

Kama kipaji cha Diamond kisingepata usimamizi, Diamond angelikuwa anaomba dua kupata nauli ya daladala, yeye mwenyewe Diamond mara kadhaa amesema kuna watu wamemnyanyua sana.

Lakini Agnes najua kuna watu wamemdidimiza sana, wamemuumiza sana, wamemtumia sana na wamempa matatizo makubwa sana – wengine kati ya watu waliomuumiza watakuwa msibani kwake wakishughulikia usafiri, chakula, matangazo….wengine watafika kuchangia maziko yake lakini walimuumiza sana na ama walifurahi sana wakati walidhani anazama alipokuwa hai. Ni kawaida yetu!

Wako watu wanaamini “wewe binafsi ndiye wa kulaumiwa kwa maisha yako”, ni kweli kabisa, lakini wanasaikolojia wanajua “wewe ni wewe hivi sasa kwa sababu ya jinsi ulivyoathiriwa na mazingira uliyomo.” Watu ulionao, familia uliyonayo, ndugu zako, taifa lako, marafiki zako n.k ni vyanzo vikubwa vya kukufanya wewe uwe nani.

Dada yetu Masogange ni matokeo ya yote niliyoyataja hapo juu. Yeye ni tunda letu, ni dada yetu, mtoto wetu, mwenzetu.

Agnes ni taswira yetu halisi. Kama tunadhani yu mdhambi, basi sisi ni wadhambi mara 100. Kama tunadhani hafai, basi sisi hatufai mara 100 – yeye ni zao letu sisi, ni zao la mazingira yetu, zao la mipango yetu kwa vijana wetu, zao la roho zetu.

Wakati tunamzika Agnes tukumbuke maisha aliyokuwa anaishi ndiyo wanaishi vijana wetu wengi kwenye taifa letu, mapito aliyopitia hadi mwisho ndiyo safari ya maisha ya vijana wetu wengi, tabu, mateso, usumbufu, shida, kutengwa, kutwezwa, kudhalilishwa, kuumizwa, kutumiwa na kulaumiwa kwa yote hayo – ndiyo maisha wanayopitia vijana wetu wengi na hasa wasichana wa taifa hili.

Nimemsikia baba ya Agnes akisema mwaka jana na hadi mwaka huu binti yake alimweleza kuwa anajipanga kumfanyia mambo makubwa. Agnes akamsisitiza baba yake kuwa siku hizi (yeye Agnes) amebadilika mno, ameachana na maisha ya hovyo na ana shabaha ya kulinda nidhamu na kutafuta mafanikio.

Kwa mtizamo wangu, Agnes amekufa kifo cha amani na matumaini makubwa kwake na kwa Mungu wake. Halafu naamini Agnes alikuwa mdhambi kama sisi woote, na labda sisi wengine tumewahi kufanya dhambi kubwa kumshinda, yeye anahukumiwa sana kwa sababu alikuwa maarufu kiasi chake, alikuwa socialite, video queen na msanii.

Wasanii wetu (hasa wa kike) wajifunze kupitia maisha ya Agnes, wajipange, wajenge nidhamu, wachague marafiki wenye faida, wakuze sanaa zao ndani ya menejimenti imara, wasikubali kutumiwa na watu wenye fedha, wanasiasa wenye mamlaka yoyote na hasa wanaume.

Familia zetu, ndugu, jamaa, marafiki, taifa zima..sote tujifunze na tusikimbie majukumu yetu, tusitose wajibu wetu.

Nawapa nukuu hii kutoka Yohana.8:7-9
“Nao walipozidi kumhoji, alijiinua, akawaambia, Yeye asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe. Akainama tena, akaandika kwa kidole chake katika nchi. Nao waliposikia, wakashitakiwa na dhamiri zao, wakatoka mmoja mmoja, wakianzia tangu wazee hata wa mwisho wao; akabaki Yesu peke yake, na yule mwanamke amesimama katikati. ”

Nawakumbusha ya kwamba, wale wanaodhani Agnes alikuwa mwovu wajichunguze mara 7 zaidi, watagundua wao ni wadhambi kuliko marehemu. Agnes ni tunda letu, na kama kuna makwazo aliipa jamii yetu basi hayo ni malezi yetu.

Binti huyu amemaliza safari yake, ametuachia mafunzo makubwa sana. Taswira yake ya ndani ya yeye na Mungu wake inaweza kuwa utukufu mkuu ambao binadamu hatuna jicho la kuuona. Kifo chake kimenigusa mno ndiyo maana nimempa heshima hii.

Mungu wa Mbinguni ampokee, amsamehe dhambi zake! Sisi tuliobaki tunajua wajibu wetu, tumsitiri, na kama hapo kabla ulisambaza picha zisizo na maadili, kama umemaliza kusoma andiko hili, zifute, maana Yesu angelikuuliza “Yeye asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe”.

Mtatiro J,
(+255787536759, juliusmtatiro@yahoo.com),
22/04/2018.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Michezo

Tusua mkwanja na mechi za Ijumaa leo

Spread the love  LEO hii mechi zinaendelea kote na wewe kama unataka...

BiasharaHabari za Siasa

Mavunde aagiza Perseus kuharakisha fidia Sengerema

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameipongeza Kampuni ya Perseus kwa...

Habari za Siasa

Kigogo Chadema awanyooshea vidole vigogo serikalini kuhusu ripoti ya CAG

Spread the love  MWANACHAMA wa Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob, amedai...

Habari za Siasa

Wabunge waikalia kooni TAKUKURU Bungeni

Spread the love  BAADHI ya wabunge wamelia na changamoto za utendaji wa...

error: Content is protected !!