Tuesday , 5 December 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Ujerumani kushirikiana na Tanzania kuboresha makumbusho ya Majimaji
Habari za Siasa

Ujerumani kushirikiana na Tanzania kuboresha makumbusho ya Majimaji

Spread the love

 

Serikali ya Ujerumani imeahidi kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuboresha Makumbusho ya Majimaji ili  kuhifadhi kumbukumbu sahihi kwa ajili ya wakati huu na kwa  vizazi vijavyo. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).

Ahadi hiyo imetolewa na Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani, Dk. Frank-Walter Steinmeier alipotembelea Makumbusho ya Vita vya Maji Maji  Songea Mkoani Ruvuma.

Dk. Steinmeier amesema Ujerumani ipo tayari kufanya uchambuzi na mchakato wa historia ya vita vya Maji Maji kwakuwa kilichotokea zamani hakipaswi kusahaulika.

“Ili kuweka kumbukumbu sawa kwa sasa na kwa wakati ujao, Ujerumani tunaahidi kushirikiana na Tanzania kuboresha makumbusho hii,” alisisitiza Rais Steinmeier.

Dk. Steinmeier alisema Ujerumani inatamani kufanya uchambuzi na mchakato wa historia ya ‘Vita vya Maji Maji’ na kuongeza kuwa mchakato huo utahusisha vijana, wanafunzi wa shule na vyuo vikuu, wasomi na wataalamu wa hifadhi na sehemu za kumbukumbu.

“Mwaka 2024, Ujerumani ina mpango wa kufanya maonesho kwa kushirikiana na Makumbusho ya Taifa ya Tanzania, maonesho hayo yatajulikana kwa jina la  “Historia ya Tanzania”, alisema Steinmeier.

Awali Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Dkt. Damas Ndumbaro alisema historia ya Tanzania na Ujerumani ina sura mbili tofauti. Alifafanua kuwa sura ya kwanza ni kuhusu vita waliyopigana babu zetu na sura ya pili ni yale mazuri yaliyofanywa na Serikali ya Ujerumani Kama vile kujenga shule, hospitali na kutoa huduma nyingine za kijamii.

“Muhimu zaidi ni kukumbuka na kusahau yaliyopita na kuendelea kudumisha uhusiano mzuri uliopo na kusonga mbele kwa kuleta maendeleo kati ya mataifa yetu mawili, lakini pia katika mji wetu wa Songea ,” alisema Dk. Ndumbaro

Dk. Ndumbaro aliongeza kuwa Songea wanatamani kuona makumbusho ya kisasa ya ushirikiano kati ya Ujerumani na Tanzania yakijengwa Songea, “pia tunatamani Ujerumani itusaidie kuboresha chuo cha VETA Songea ili kuwawezesha vijana wetu kupata mafunzo mbalimbali,” alisema Dk. Ndumbaro.

Waziri Ndumbaro pamoja na mambo mengine, ameiomba Serikali ya Ujerumani kushirikiana na Mji wa Songea kwa kuwawezesha kutembeleana, kushirikiana na kuendeleza utani kati ya Wangoni na Wajerumani.

Rais Stenmeier mbali na kutembelea Makumbusho ya Vita vya Maji Maji pia ametembelea Shule ya Msingi ya Majimaji.

Makumbusho ya Vita vya Maji Maji ni makumbusho pekee nchini Tanzania inayoonesha historia kubwa ya Vita vya Maji Maji katika harakati za ukombozi dhidi ya ukoloni wa Wajerumani.

Rais Stenmeier amehitimisha ziara yake ya Kikazi ya siku tatu nchini leo tarehe 01 Novemba 2023.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Baba yake Ole Sabaya ashinda Uenyekiti CCM – Arusha

Spread the loveLoy Thomas Sabaya ambaye ni Baba wa aliyekuwa Mkuu wa...

Habari za Siasa

Serikali yaagiza uchunguzi chanzo maporomoko Hanang

Spread the loveSERIKALI imeagiza uchunguzi ufanyike ili kubaini chanzo cha maporomoko ya...

Habari za SiasaTangulizi

Maafa Manyara: Rais Samia akatisha ziara yake Dubai

Spread the loveRAIS wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amekatisha ziara yake...

Habari za SiasaTangulizi

Wataalaam wa miamba watua Hanang

Spread the loveWaziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na...

error: Content is protected !!