MRADI wa reli ya kisasa ya umeme (SGR) kipande cha kutoka Morogoro, Dodoma na Makutupora, unatarajiwa kukamilika Januari mwaka 2024. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma (endelea).
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa ndani ya Jiji Dodoma.
Mkuu huyo wa mkoa ametembelea mradi wa Reli ya kisasa ya umeme (SGR ) na Mji wa Serikali Mtumba (Magufuli City) na kueleza kuwa ameridhishwa na ujenzi wa mradi huo ambao mpaka sasa kwa mujibu wa mkandarasi umefikia asilimia 95.7 kukamilika.
Amesema mradi huo utaongeza kasi ya maendeleo na fursa za kiuchumi ikiwa ni pamoja na kupendezesha mandhari ya jiji la Dodoma ambapo pia ni fursa ya utalii hivyo amewataka wananchi kuchangamkia fursa za kiuchumi
Aidha, amewaagiza wasimamizi wa mradi ambao ni Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuendelea kutoa elimu kwa wananchi wanaozunguka maeneo ya mradi huo kuchukua tahadhari ikiwemo ya usalama wa mifugo na watu katika eneo la miradi kwa kuhakikisha wanapita maeneo husika ambayo yamewekwa kwa ajili ya matumizi yao ikiwemo vivuko kwa ajili ya usalama.
Akiwa katika Mji wa Serikali Senyamule amekagua maendeleo ya ujenzi wa majengo ya wizara na ameonyesha kuridhishwa na kasi ya maendeleo ya miradi hiyo.
Hata hivyo, amewaagiza wakandarasi wa miradi hiyo kuongeza kasi ya ujenzi kwa kuzingatia ubora wa majengo hayo ili kufikia Januari 2024 iwe imekamilika huku akiendelea kusisitiza suala la kupanda miti ili kutunza mazingira.
“Tumekuja leo kutembelea na kuona maendeleo ya miradi ambayo pia ni kivutio cha utalii ndani ya Jiji letu ambayo yapo katika hatua tofauti tofauti, kuna yaliyofikia asilimia 75 hadi 78 na kuna ya asilimia 99.9, kuna ya asilimia 53 ambapo ya asilimia 75-78 yalitakiwa yawe yamekamilika.
“Nitoe wito kwa wakandarasi waliopata fursa za kujenga, hakikisheni mnatimiza wajibu wenu, punguzeni sababu nyingi kwani tuna amini changamoto zipo ila tatueni kwa haraka ili kukamilisha majengo haya kwa wakati husika,” ameeleza Senyamule.
Kwa upande wake, Meneja wa Ujenzi (TBA), Mhandisi Manasseh Shekalaghe amemuhakikishia mkuu wa mkoa kuwa watasimamia wakandarasi kwa ukaribu zaidi ili ikifika Januari watumishi wote waweze kuhamia Mtumba.
Leave a comment