October 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ujenzi Daraja la Ifume, Tarura Tanganyika yapewa siku 30

Spread the love

 

MTENDAJI Mkuu wa Mamlaka ya Barabara Vijijini na Mijini (Tarura), Mhandisi Victor Seff ametoa mwezi mmoja kwa Tarura Wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi kukamilisha ukarabati wa daraja la Ifume. Anaripoti Mwandishi Wetu, Katavi … (endelea).

Mhandisi Seff ametoa maagizo hayo leo Jumatano, tarehe 17 Mei 2022 wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya miradi ya barabara katika Mkoa wa Katavi.

“Daraja hili ni muhimu sana kwa wakazi wa hapa kwa shughuli za kiuchumi, hivyo ni lazima mhakikishe kazi hii inakamilika kwa haraka ili wananchi wa Kalamsenga na Itunya waweze kusafirisha mazao yao bila kupata usumbufu unaojitokeza kwa sasa,“ amesema Mhandisi Seff.

Amesema Tarura makao makuu itatoa fedha ambazo alielekeza zitumike katika ukarabati wa daraja hilo na aliagiza tathimini ifanyike haraka na maombi ya fedha hizo yatumwe ili yafanyiwe kazi kwa haraka.

Pia, amewaagiza Tarura wilaya kuhakinisha wanatoa kwa haraka magogo na uchafu wote ulioletwa na mvua na kusababisha kuziba kwa daraja hilo ili fedha zikija ukarabati ufanyike ndani ya muda wa mwezi mmoja aliotoa.

Kwa upande wake, Diwani wa Kapalamsenga, Jefu Lameki amesema anaushukuru uongozi wa Tarura kwa kusikia kilio chao kwani wamekuwa wakipata adha kubwa kutokana na kuharibika kwa daraja hilo.

Amesema wanachi watashiriki kikamilifu kuondoa magogo na uchafu katika daraja.

Aidha, Mhandisi Sef amekagua ukarabati wa barabara ya Kapalamsenga – Ifume kuelekea bandari ya Kareme, Tanganyika yenye urefu wa Kilomita 12.1 na kuridhishwa na kazi inavyoendelea, ambapo mpaka sasa ukarabati umefikia asilimia 90.

“Barabara hii itasaidia sana katika shughuli za usafirishaji wa mazao na pembejeo za kilimo na ni sehemu ya barabara ya kutokea bandari ya Karema hivyo ni barabara muhimu sana,” amesema Mhandisi Seff

error: Content is protected !!