MBUNGE wa Makete mkoani Njombe (CCM), Festo Sanga, amehoji kauli ya Serikali kuhusu kukithiri vitendo vya ujambazi katika majiji nchini. Anaripoti Nasra Bakari, DMC…(endelea).
Sanga amehoji hayo leo Alhamisi tarehe 27 Mei 2021, bungeni jijini Dodoma, kwenye kipindi cha maswali ya papo kwa papo, kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
“Swali langu limejikita kwenye usalama, siku za karibuni nchini kumekuwa na changamoto ya wimbi la ujambazi, lililokuwa linaendelea hasa mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Mbeya, Mwanza na Arusha,” amesema Sanga na kuongeza:
“ Kitu ambacho kimekuwa kikihatarisha usalama wa wananchi wetu na wafanyabishara, ipi kauli ya Serikali dhidi ya vitendo hivi viovu vinavyoendelea?”
Akijibu swali hilo, Waziri Majaliwa, amesema Serikali kupitia vyombo vya ulinzi na usalama, inaendelea na juhudi za kudhibiti vitendo hivyo vya uhalifu.
“Jeshi la Polisi linafanya kazi nzuri sana, siku mbili tatu nimesikia kazi nzuri waliyoifanya Dar es Salaam kudhibiti majambazi. Nataka niwahakikishie Serikali inaendelea na kazi hiyo kuhakikisha ulinzi uanendelea,” amesema Waziri Majaliwa.
Aidha, Waziri Majaliwa alitoa wito kwa Watanzania kushiriki katika ulinzi wa maeneo yao na nchi kwa ujumla, kwa kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola, wanapopata taarifa juu ya viashiria vya matukio ya ujambazi.
“Ni jukumu letu kuhakikisha kuwa, tunashiriki kikamilifu kwenye ulinzi wa nchi na kila Mtanzania anapohisi kuona dalili za upotevu wa amani, ni vyema kutoa tarifa katika vyombo vya ulinzi na usalama kuona hatua zinachukuliwa,” amesema Majaliwa.
Hivi karibuni katika Mkoa wa Dar es Salaam, kwenye maeneo ya External Ubungo na Mabwepande, kulitokea matukio ya ujambazi, hali iliyopelekea Inspekta Jenerali wa Polisi nchini (IGP), Simon Sirro, kuzuru katika maeneo hayo.

Katika ziara hiyo, IGP Sirro alitoa maagizo kwa kampuni binafsi za ulinzi kuacha kuajiri wazee, baada ya kubaini baadhi ya matuio hayo husababishwa na maeneo hayo kulindwa na wazee, walinzi wachache na ukosefu wa silaha za kutosha.
Tarehe 25 Mei 2021, Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Camillius Wambura, alisema jeshi hilo liliwakamata watu zaidi ya 20, kwa tuhuma za uhalifu, ikiwemo ujambazi, mauaji na uvunjaji.
Leave a comment