July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Uhusiano wa lishe na magonjwa sugu

Aina ya maumbo ya epo na peasi

Spread the love

MAGONJWA sugu yasiyo ya kuambukiza yana mahusiaano makubwa na mtindo wa maisha na ulaji usiofaa.

Zamani magonjwa haya yalikua yanaonekana kama ni magonwa ya watu wenye umri mkubwa lakini sasa yanaathiri hata watu wenye umri mdogo, hii inatokana na mtindo wa maisha na ulaji ambao umebadilika sana.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), mitindo ya maisha isiyo bora ndio chanzo kikuu cha ongezeko la magonjwa haya.

Magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza ni pamoja na Kisukari, Shinikizo kubwa la Damu, Magonjwa ya Moyo, Magonjwa ya Figo na Saratani. Magonjwa haya yamekua yakiongezeka kwa kasi hasa katika nchi yetu na nchi zinazoendele.

Maendeleo ya kiuchumi ambayo ni pamoja na kuongezeka kwa kipato ambacho huwapa watu uwezo wa kumudu gharama za nyenzo mbalimbali za kurahisisha kazi za kutumia nguvu ikiwa ni pamoja na magari, vifaa vya kutendea kazi, kompyuta, runinga ni miongoni mwa mambo yanayochangia kuongezeka kwa magonjwa haya.

Kunapokuwa na matumizi makubwa ya nyezo za kufanyia kazi au kutokufanya mazoezi ya mwili, huwafanya watu kulimbikiza nishati lishe mwilini ambazo husababisha ongezeko la uzito wa mwili na hivyo kuchangia kuongeza kwa uwezekano wa kupata magonjwa hayo.

Mambo mengine yanayochangia magonjwa haya ni kuongezeka kwa watu wanaohamia mijini na mabadiliko ya tabia ya ulaji. Mabadiliko ya tabia na mtindo wa ulaji yamefanya jamii kubadilisha namna ya ulaji na aina ya vyakula vinavyoliwa.

Mabadiliko haya huifanya jamii kuachana na utaratibu wa kutumia vyakula vya asili, kutopika chakula kwa njia za asili, kutumia kwa wingi vyakula venye mafuta mengi, sukari na chumvi nyingi pamoja na nafaka ambazo zimekobolewa. Matokeo ya mabadiliko haya ni ongezeko la magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza ambayo huathiri ubora wa maisha.

Tathmini ya hali ya lishe ya mtu ni muhimu sana ili kuwezesha kugundua mapema dalili zozote za matatizo ya kiafya au ulaji usiofaa unaoweza kuongeza uwezekano wa mtu kupata maradhi.

Ni muhimu sana kufanya tathmini ya hali ya lishe mara kwa mara, ili kutoa ushauri wa jinsi ya kufanya marekebisho mapema ili kuzuia au kuweka msingi wa hatua za kukabiliana na tatitizo lolote.

Tathmini ya hali ya lishe inajumuisha mbinu mbalimbali kama kuchukua historia ya ulaji na maradhi, na kutumia vipimo vya maabara na maumbile. Vipimo vya maabara na maumbile hutofautiana kulingana na umri, jinsi na hali ya mtu (kama mjamzito).

Tafsiri ya vipimo huzingatia viashiria maalum na viwango vilivyowekwa na WHO. Vipimo na njia hizi huweza kutumika kutoa tahadhari kuhusu uwezekano wa magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza.

Tathmini ya hali ya lishe, tafsiri na hatua za kuchukua

Njia mbalimbali hutumika katika kutathmini hali ya lishe kama tulivyoona kwenye makala iliyopita iliyoonyesha namna ya kutengeneza mlo kamili.

Njia ya kwanza ni kuchukua histori ya ya ulaji na maradhi. Tathmini hii ni muhimu sana katika kugundua mtindo wa maisha na tabia ya ulaji wa mtu na kama ana tatizo lolote la kiafya ambalo linaathiri ulaji wake.

Kuchukua historia ya ulaji kunajumuisha kupata taarifa muhimu kuhusu aina ya vyakula anavyokula mtu, idadi ya milo kwa siku, vyakula anavyopendelea au asivyopendelea kula na hata mtindo wa maisha anaoishi.

Katika kuchukua historia ya maradhi itasaidia kujua kama kuna maradhi yoyote katika njia ya chakula yanayaoathiri ulaji au yanayoongeza mahitaji ya virutubisho.

Njia nyingine ni ya vipimo vya umbile la mwili, hapa upimaji wa uwiano wa uzito na urefu au Body Mass Index (BMI).

demu

Uzito wa mtu katika kilogramu hugawanywa na urefu wa mtu katika mita kipeuo cha pili BMI = Uzito(Kilogramu)/urefu (Mita)2

Uwiano unaopatikana huelezea hali ya lishe ya mtu na kama yupo katika hatari ya kupata magojwa sugu yasiyo ya kuambukiza. Kwa mfano kama uwiano utaonyesha kama una unene uliokithiri au kiribatumbo (utapiamlo) ina maana kiasi cha chakula anachokula ni kingi au kinatoa nishati lishe nyingi kulingana na mahitaji ya mwili na ziada huhifadhiwa mwili kama mafuta na kuwa katika hatari ya kupata magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza.

[pullquote]

Tafsiri ya BMI:

Uzito pungufu:       < 18.5

Uzito wa Kawaida: 18.5 – 24.9

Uzito uliozidi: 25 – 29.9

Uzito uliokithiri:      ≥ 30

[/pullquote]

Kipimo kingine ni mzunguko wa kiuno, kipimo hiki pia huonyesha kama mtu ana uzito uliozidi na kumuweka katika uwezekano mkubwa wa kupata magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza.

Kipimo hiki pia husaidia kuonyesha kiasi cha mafuta yaliyohifadhiwa tumboni. Mafuta yanapokuwa yamehifadhiwa mengi sehemu ambazo ni karibu na moyo ni hatari zaidi kuliko yanapohifadhiwa sehemu nyingine za mwili.

Kipimo kingine ni uwiano wa mzunguko wa nyonga na kiuno (waist to hip ratio). Uwiano huu nao hutuelezea namna mafuta yalivyohifadhiwa mwilini. Mafuta yanayohifadhiwa sehemu za juu za mwili (kifuani na tumboni) yanaashiria hatari zaidi kiafya ukilinganisha na mafuta yanayohifadhiwa mahali pengine mwilini.

Tafiti zinaonyesha kwamba mtu akiwa na umbile la duara kwenye sehemu za kifua na tumbo (apple shape) humuweka katika hatari zaidi za magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza ukiliganisha na mtu mwenye umbile la duara chini ya tumbo (pear shape).

Umbile la duara linafanana na tunda la Tufaha (Epo) na umbile la tunda la peasi

Mtu akiwa na umbile kama apple ina maana kuwa mafuta mengi yamehifadhiwa kifuani na tumboni. Aina hii ya hifadhi ya mafuta inamuweka mtu katika hatari ya kupata maradhi kama magonjwa ya moyo, kisukari na shinikizo kubwa la damu.

Mtu mwenye umbile kama la peasi inamaana mafuta yake mwilini yamehifadhiwa kuanzia kwenye nyonga, mapaja na makalio. Mara nyingi mtu huyu huwa na umbile dogo kifuani na tumboni na pia kiuno huwa chembamba, lakini mnene kuanzia kwenye nyonga kwenda chini.

Mtu huyu hayupo kwenye hatari ya kupata magonjwa sugu ukilinganisha na yule mwenye umbo la epo.

Kwa hiyo, kipimo cha uwiano wa mzunguko wa kiuno na nyonga hutumika kugundua kama mtu amehifadhi mafuta kifuani (apple) au chini ya kiuno (pear).

Taarifa zote hizi za historia ya ulaji na maradhi na vipimo vya mwili husaidia kuonyesha viashiria vya magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza na kuchukua hatua mapema kuhusu ulaji unaofaa na mtindo bora wa maisha.

Makala haya imeandikwa na Afisa Tabibu na Lishe, Juma Nziajose, anapatikana no: 0718 962336

error: Content is protected !!