August 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Uhuru wa habari uliopo una kasoro – Wakili Marenga

Waandishi wa Habari

Spread the love

 

WAKILI wa Kujitegemea, James Marenga amesema vyombo vya habari nchini Tanzania kwa sasa vinaweza kukosoa tofauti na miaka mitano ama sita iliyopita. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Hata hivyo Marenga amesema tatizo lililopo ni kwamba kukosoa huko hakulindwi kisheria.
Ametoa kauli hiyo leo Jumanne tarehe 2 Agosti, 2022, akizungumza na kituo cha Televisheni cha Azam katika Kipindi cha Morning Trumpet.

Wakili Marenga amesema, kwa sasa vyombo vya habari nchini vinaandika na hata kukukosoa lakini pale mwandishi ama chombo cha habari kinapowindwa, sheria zilizopo zinaweza kutumika dhidi yake.

“Kwa sasa vyombo vya habari vinaandika kwa uhuru, vinakosoa lakini kilichopo, kama mwandishi ama chombo cha habari kinawindwa, sheria hizi hizi zinatumika kuumiza chombo ama mwandishi.

“Mwandishi anaweza kufungwa kwa sheria zile zile ama chombo cha habari kinaweza kuondolewa sokoni kwa sheria hizo hizo, ndio maana tunasema uhuru wa habari lazima ulindwe kisheria,” amesema Wakili Marenga ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA-TAN).

Amesema, kuwepo kwa sheria hizo za habari, kwa kiwango kikubwa kumesababisha kushuka kwa habari za uchunguzi, na kwamba baadhi ya wanahabari wamepoteza vifaa vyao kutokana na polisi kuvitwaa kwa ajili ya upekuzi.

“Sheria hii imewapa mamlaka makubwa polisi, wanapoamua kukufuatilia na hata kuchukua vifaa vyako, wanaweza kufanya hivyo kwa sheria hii. Kwa nchi kama ya Ghana lazima polisi awe na kibali, lakini hapa kwetu hiyo haipo,” amesema.

Pia Wakili Marenga amesema, miongoni mwa mambo yanayokwaza tasnia ya habari ni pamoja na sheria kuelekeza usajili wa magazeti kila mwaka.

Amesema, kwa magazeti ingetosha kusajiliwa mara moja na sio kila mwaka kama inavyoelekezwa na sheria ya sasa.

“Unakuwa ni usumbufu na kupoteza pesa, yaani ukimaliza mwaka unaanza kukusanya documents (nakala) ambazo ulizipeleka awali unapeleka tena, tena unatakiwa kulipa. Hili jambo tunasema hapana, tunapaswa kusajili mara moja basi,” amesema.

error: Content is protected !!