April 11, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Uhuru wa habari: THRDC yamwangukia Rais Samia

Onesmo Olengurumwa, Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu

Spread the love

 

MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), umemuomba Rais Samia Suluhu Hassan, kufanyia kazi uamuzi uliotolewa na mahakama za kitaifa na kimataifa, kuhusu vyombo vya Habari vilivyofungiwa na serikali. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Ombi hilo limetolewa leo Alhamisi tarehe 8 Aprili 2021, na Mratibu wa Kitaifa wa THRDC, Onesmo Olengurumwa akimpongeza Rais Samia kwa kuagiza kuachiwa huru vyombo vya habari vilivyofungwa na serikali.

Olengurumwa amesema, ili Rais Samia atengeneze mazingira bora ya kazi za vyombo vya habari na wanahabari nchini, inabidi serikali yake ifanyie kazi uamuzi wa mahakama hizo, kuhusu kesi zinazohusu tasnia ya habari.

Samia Suluhu Hassan, Rais wa Tanzania

Mratibu huyo wa THRDC ametaja uamuzi huo ulitolewa na Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ), katika kesi ya mtandao huo, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Tanzania (LHRC) na Baraza la Habari Tanzania (MCT), dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika kesi hiyo Namba 2/2017, EACJ iliamuru Serikali ya Tanzania kuviondoa vifungu vya Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari ya mwaka 2016, vinavyokiuka Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Mahakama hiyo ilitoa uamuzi kwamba vifungu namba 7 (3) (a), (b), (c), (f), (g), (h), (i) and (j), 13,14,19,20, 21, 35, 36, 37, 38, 39, 40, 50, 52, 53, 54,58 na 59, vya Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016, vinakiuka Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki hivyo serikali ya Tanzania inapaswa kuviondoa kwenye sheria hiyo,” ameomba Olengurumwa.

Olengurumwa ametaja uamuzi mwingine ni wa Mahakama Kuu ya Tanzania katika kesi ya Victoria Media Services Ltd dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Waziri wa Habari (2017).

Pamoja na Uamuzi wa Makakama Kuu katika kesi ya Hali Halisi Publishers Ltd dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali uliyotolewa na Mahakama Kuu ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Na pia Kesi ya Hali Halisi Publishers Ltd dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (2017), iliyotolewa na EACJ.

Katika uamuzi wa kesi hizo zilizofunguliwa na Hali Halisi zikipinga gazeti lake kufungiwa na serikali, mahakama hizo ziliamuru gazeti linalochapishwa na kampuni hiyo – MwanaHALISI – lifunguliwe mara moja.

“Tukiwa miongoni mwa wadau wa habari nchini Tanzania, tunaamini kuwa, agizo la Rais Samia lililenga kufunguliwa kwa vyombo vyote vilivyufungiwa yakiwemo magazeti.

“Hivyo, tunaiomba serikali ifanye mazungumzo na vyombo hivyo na kuvifungulia ili viweze kuendelea kulitumikia taifa,” amesema Olengurumwa.

Jumanne iliyopita ya tarehe 6 Aprili 2021, akiwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua, Rais Samia aligusia suala la kugunguliwa kwa vyombo vya habari vilivyofungiwa.

Vyombo vilivyofungiwa, kunyimwa leseni au kufutiwa ni; MwanaHALISI, Mseto, Mawio, Tanzania Daima na Televisheni ya Mtandaoni ya Kwanza TV.

Rais Samia alisema wizara ya habari inapaswa kusimamia vyombo vya habari vya ndani, “nasikia kuna vijivyombo vya habari mmevifungia fungia, sijui viji- TV vya mikononi vile, vifungulieni lakini wafuate sheria na miongozo ya serikali.”

“Vifungulieni tusiwape mdomo wa kusema tunabinya uhuru wa vyombo vya habari, lakini mhakikishe kila mliyempa ruhusu ya kuendesha chombo cha serikali anafuata sheria za serikali na kanuni ziwe wazi, kosa hili adhabu yake ni hii na mnakwenda kwa adhabu mlizoziweka kwenye kanuni.”

Rais Samia alisema, “tusifungie tu kibabe. Wafungulieni lakini tuhakikishe wanafuata kanuni na miongozo ya serikali.”

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alisema “Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ameelekeza Televisheni za Mtandaoni (Online TV) tu ndio zifunguliwe na sio vyombo vya habari vingine yakiwemo magazeti vilivyofungiwa kwa mujibu wa Sheria.”

error: Content is protected !!