May 6, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Uhuru Kenyatta sasa rasmi Ikulu ya Kenya

Uhuru Kenyatta, Rais mteule wa Kenya

Spread the love

WAFULA Chebukati, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi nchini Kenya (IEBC), amemtangaza Rais Uhuru Kenyatta wa chama cha Jubilee kuwa mshindi wa nafasi ya Urais nchini Kenya, akimbwaga mpinzani wake wa karibu Raila Odinga, kutoka Muungano wa NASA, anaandika Charles William.

Katika matokeo yaliyotolewa leo usiku, IEBC imetangaza kuwa Uhuru amepata kura 8,203,290 sawa na asilimia 54.27 huku Odinga akipata kura 6,762,224 sawa na asilimia 44.74. Hivyo, Kenyatta ataliongoza Taifa la Kenya kwa muhula wa pili.

Akitoa neno la shukrani baada ya kutangazwa mshindi, Uhuru amesema ataendelea kufanya kazi za maendeleo alizozianza katika muhula wake wa kwanza huku akiipongeza IEBC kwa kazi nzuri ya kusimamia uchaguzi.

“Nawashukuru washindani wenzangu, sisi si maadui. Nategemea ushirikiano kutoka kwao kwani sisi wote ni raia wa nchi inayoitwa Kenya. Nipo tayari kujadiliana na kubadilishana mawazo na viongozi wa upinzani ili kuliendeleza Taifa letu,” amesema Kenyatta.

Matokeo hayo yametangazwa, ikiwa ni siku tatu baada ya uchaguzi kufanyika tarehe 8 Agosti, 2017. Awali kulikuwa na mvutano baina ya tume ya uchaguzi na viongozi wa muungano wa NASA ambao walidai kuwa matokeo yaliyokuwa yakitangazwa hayakuwa sahihi.

NASA ilieleza kuwa matokeo halali ni yale yatakayopatikana katika fomu ya matokeo namba 34A na si vinginevyo, hata hivyo mapema leo Odinga alifika eneo la Bomas na kukutana na maofisa wa tume ya uchaguzi, kujadili kile walichodai kuwa ni dosari katika majumuisho ya kura.

Muda mchache kabla ya matokeo kutangazwa Odinga alionekana akiondoka katika eneo la Bomas huku taarifa zikieleza kuwa, hajakubaliana na matokeo hayo.

error: Content is protected !!