June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Uholanzi, Uturuki ‘waingia’ vitani

Baadhi ya wasomi Waarmenia waliokamatwa wakauawa usiku wa tarehe 24 Aprili 1915

Spread the love

 

BUNGE nchini Uholanzi, limepitisha muswaada unaoelekeza serikali ya nchi hiyo, kuyatambua mauaji ya Waarmenia, yaliyofanyika wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia, kama mauaji ya kimbari. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Lakini Uturuki, kupitia wizara yake ya mambo ya nje, imeikosoa hatua ya  Uholanzi na kulitaja tukio hilo kuwa ni batili na lisilokubalika.

Kwa mujibu wa Serikali ya Uturuki, muswada uliopitishwa na Bunge la nchi hiyo, ni uamuzi unaolenga kuiandika upya historia kwa mtazamo wa malengo ya kisiasa na hivyo hauwezi kukubalika.

Mauaji ya Waarmenia 1.5 milioni yaliyofanywa na vikosi vya usalama vya Uturuki chini ya utawala wa Ottoman kati ya mwaka 1915 na 1917, yanatambuliwa rasmi kama mauaji ya kimbari na nchi kadhaa zikiwemo Ufaransa na Urusi.

Maangamizi ya Waarmenia yalitekelezwa kwa sera mbovu na kandamizi za dola ya Osmani ya kukomesha Waarmenia wote walioishi ndani ya eneo la dola hilo, ambalo sasa ni Uturuki.

Kati ya watu milioni 1 na 1.5, wanakadiriwa kufariki mwaka Aprili 1915, ambapo watawala Waturuki waliteka wasomi Waarmenian 250 mjini Istanbul.

Mwanamke Mwarmenia akiwalilia watoto wake watano waliouawa.

Miaka 100 baadaye kulifanyika maadhimisho makubwa katika nchi mbalimbalimbali, hasa Etchmiadzin, ambako ni makao makuu ya kiroho ya Waarmenia, ambapo Padri Katoli Karekin II aliwatangaza kwa jumla waliouawa kuwa watakatifu wafiadini.

Maangamizi yalitekelezwa kwa awamu mbili: Kwanza, wanaume wazima waliuawa mara moja au kulazimishwa kufanya kazi za shoka, halafu wanawake, watoto, wazee na wagonjwa waliswagwa na wanajeshi hadi jangwa la Syria ili wafe njiani, baada ya kunyimwa chakula, maji, mbali na kubakwa na kuuawa.

Makabila mengine pia, hasa ya Kikristo, kama vile Waashuru na Wagiriki, waliangamizwa na Waturuki wakati huo.

Mtawanyiko wa Waarmenia duniani unatokana kwa kiasi kikubwa na mauaji hayo.

Maiti za watoto Waarmenia

Vilevile, kutokana na mauaji hayo, Raphael Lemkin (mwaka 1943), alitunga neno genocide akimaanisha kama maangamizi ya halaiki; maangamizi ambayo yanahesabiwa ya kwanza, yakifuatwa na yale makubwa zaidi ya Wayahudi wa Ulaya chini ya Adolf Hitler.

Utawa wa Uturuki, ulioshika nafasi ya dola la Osmani, unazidi kukataa neno genocide kuhusiana na mauaji ya Waarmenia, ingawa wataalamu wengi wa historia wanaliona kuwa sahihi na nchi nyingi zaidi na zaidi zinaitaka nchi hiyo, kukiri kosa na kupatana na Waarmenia.

Milki ya Osmani ilikuwa dola kubwa lililotawala upande wa mashariki wa Mediteranea pamoja na nchi nyingi za Mashariki ya Kati kati ya karne ya 14 na mwaka 1922.

Milki ilianzishwa na Waturuki Waosmani ikachukua nafasi ya ukhalifa wa Waabbasi na Milki ya Bizanti.

Waarmenia waliokamatwa kabla hawajaangamizwa

Mji wake mkuu ulikuwa Konstantinopoli (leo Istanbul) na mtawala wake mkuu alikuwa Sultani wa Waosmani. Imani rasmi ya milki ilikuwa Uislamu hata kama katika maeneo mengi idadi kubwa ya wakazi walikuwa Wakristo.

Tabaka la viongozi wa kisiasa na wa kijeshi walikuwa Waosmani waliokuwa Waturuki pamoja na mchanganyiko wa Waislamu kutoka sehemu zote za milki yao, hasa Balkani.

Taarifa zinasema, milki hiyo, iliyoanza kama eneo dogo la kabila la Kituruki katika Anatolia chini ya chifu Osmani I, iliendelea kupanuka hasa kwa kutwaa sehemu za milki ya Bizanti upande wa Asia na Ulaya ya Kusini-Mashariki.

error: Content is protected !!