July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

‘Uhaba wa vifaa, walimu wa sayansi shida’

Wanafunzi wa shule ya sekondari

Spread the love

WAKATI matokeo ya mitihani ya kidato cha pili yanaonesha kwamba kuna tatizo kubwa la watoto kutoelewa masomo ya sayansi, baadhi ya wakuu wa shule wanasema hawana tatizo hilo, anaripoti Sarafina Lidwino.

Akitangaza matokeo hayo jijini Dar es Salaam juzi, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Mitihani Tanzania (NECTA), Dk. Charles Msonde, aliseme ingawa kiwango cha kufaulu kimeongezeka kwa zaidi ya asilimia tatu, kwa masomo ya sayansi hali ni mbaya.

Dk. Msonde alisema kiwango cha kufaulu kipo chini ya asilimia 50; hivyo kuhimiza wataalamu wa utafiti kuchunguza kiini cha tatizo hilo ili kusaidia serikali katika kurekebisha changamoto zitakazobainishwa.

Kutokana na kauli hiyo, kunaibuka maswali muhimu yanayohitaji majibu fasaha: Liko wapi tatizo? Kwa mfumo wa elimu? Ukosefu wa walimu wa sayansi? Wanafunzi ni watukutu? Au hakuna vifaa vya kufundishia, vikiwemo vya maabara?

MwanaHALISIOnline limezungukia sekondari ya Kambangwa, Wilaya ya Kinondoni, kudadisi jumuiya ya shule hiyo wanavyoona matatizo ni nini.

Mwalimu Mkuu, Madam Ng’wigulu amesema shule pao hakuna tatizo katika uelewa wa wanafunzi kwa masomo ya sayansi.

Alijinasibu kwamba matokeo ya kidato cha pili kwa shule hiyo ni mazuri, kwani ni watoto wawili tu walioharibu rekodi nzuri baada ya kutofanya mtihani.

“Hatujaletewa matokeo yalivyo, lakini nilivoangalia kwenye mtandao, nimeona shule yetu imefaulisha vizuri, kasoro tu wanafunzi wawili ambao hawakufanya mtihani. Watahiniwa shuleni petu walikuwa 138, wote wengine wamefaulu,” alisema.

Wakati mwalimu mkuu akitoa maelezo hayo, walimu wameeleza mlolongo wa matatizo yanayoikabili shule hiyo yakiwemo ukosefu mkubwa wa vitendea kazi – vitabu, vifaa vya maabara na uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi.

Walimu wanasema kwamba wanafunzi wenyewe wanachangia tatizo la uelewa kwa sababu wamejenga utamaduni wa kutozingatia yale wanayofundishwa darasani, badala yake kukimbilia mitandaoni kupata mada.

“Vitu vingine tunavyofundisha darasani ni tofauti na wanachokipata mitandaoni. Mwalimu amepitia kwa utulivu wakati akiandaa somo, hivyo anaingia darasani na kitu alichokielewa vizuri, kinyume na itakavyokuwa kwa wanafunzi kuchukua mambo mitandaoni bila ya kuelekezwa ipasavyo,” alisema mwalimu XX.

Aidha, tatizo jingine kwa wanafunzi ni kuanzia na msingi mbovu tangu shule ya msingi wa kutoshawishika kuyapenda masomo ya sayansi. “Inakuwa tatizo kubwa kuwashikilia wanapoingia sekondari, ni wachache wanaokubali sawasawa,” alisema mwalimu huyo.

“Yaani sio tu kufeli, wanayachukia pia masomo ya sayansi na kuhisi kuwa ni magumu kuliko masomo yoyote, hivyo husababisha kukata tamaa mapema… wanafunzi siku hizi wanapenda sana vitu rahisirahisi; ukimfundisha kwa kuandika notsi (muhutasari) ubaoni hasomi, anataka asome kwenye mitandao. Hili ni tatizo sugu,” ameeleza.

Baadhi ya wanafunzi walisema wanakosa mwamko wa masomo ya sayansi kutokana na misingi mibovu baada ya kutojengwa kihamasa kuyapenda masomo hayo.

Walisema waalimu pia ni kikwazo kwa wanafunzi wengi kwa kuwa wengi wa walimu hawatoi ushirikiano ikiwemo kujibu maswali au kutoa ufafanuzi mpana wa yale waliyofundishwa da rasani.

“Mara nyingine unakuta hukufahamu somo darasani ukimfuata mwalimu akusaidie kuelewa vizuri, anakuzungusha au anakupa ratiba ndefu. Ukichanganya na tatizo la vitendea kazi ndio maana inakuwa shida kwetu kuelewa vizuri,” alisema mwanafunzi wa kidato cha tatu.

Mwanafunzi wa kidato cha nne, VV, alisema: “Kwa mfano sisi shuleni hapa tupo jumla ya wanafunzi 1,368 lakini ukiangalia walimu wa sayansi kwa shule nzima wapo 13 tu. Ukienda labo (maabara) hakuna vifaa vya majaribio, hakuna vitabu.

“Kwa mfano vifaa vya kemia hakuna hata kimoja, sasa hali kama hii mwanafunzi akijumlisha hayo matatizo anaona bora aache somo hilo,” alisema.

Mwanafunzi mwingine wa kidato cha nne alisema uhaba wa walimu wa sayansi unasababisha walimu waliopo kuchoka kwa mzigo mkubwa wa kufundisha watoto wengi.

“Walimu wanakuwa wameshachoka kutokana na uchache wao… fikiria mwalimu anafundisha madarasa zaidi ya manne kwa siku. Wale wanaofundishwa mchana inakuwa shida kuelewa kwa ufasaha,” alisema.

Wanafunzi wanashauri serikali iongeze fedha za bajeti kwa ajili ya kupatikana walimu wenye ujuzi wa masomo yao na kuwapeleka kwenye shule zenye uhaba wa walimu hao.

error: Content is protected !!