April 13, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Uhaba wa madarasa: Wanafunzi wasoma kwa zamu

Spread the love

WANAFUNZI wa shule ya Msingi Mkambarani iliyopo kata ya Mkambarani Halmashauri ya Wilaya na mkoa  wa Morogoro, wanalazimika kusoma kwa kupokezana madarasa kutokana na kukabiliwa na upungufu wa vyumba vya madarasa 17, vyoo 33 huku kukiwa hakuna darasa la shule ya awali. Anaripoti Christina Haule, Morogoro … (endelea).

Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Bernadetha Malisa alisema kuwa shule hiyo ina vyumba sita tu vya madarasa huku madarasa yanayohitajika yakiwa ni 17, pamoja na uhaba wa matundu ya vyoo kwa wanafunzi na walimu.

“Tuna wanafunzi 694, na kwa wanafunzi hao tunatumia vyumba sita vya madarasa huku darasa la awali likiwa halina chumba cha kusomea, hayo madarasa mengine yana mikondo miwili na mingine mitatu lakini yote wanasoma kwenye chumba kimoja,” alisema Mwalimu Malisa.

Akizungumzia uhaba wa vyoo vya wanafunzi alisema ili matundu ya vyoo yatimie yalitakiwa yawe 33 lakini kwa sasa yapo nane ambapo manne ni kwa ajili ya wasichana na manne wavulana, huku walimu wakiwa hawana choo kabisa.

“Kutokana na hali iliyotukuta ya kuanguka choo miaka miwili iliyopita wanafunzi wakakosa pa kupata huduma hiyo tulijitahidi kutafuta wadhamini watakaotusaidia ndipo alijitokeza Diwani Mteule wa sasa ambaye alichangia bati 20 na mifuko ya saruji na kufanikisha ujenzi huo,” alisema.

Alisema kwa sasa wameanza ujenzi wa jengo na matundu matatu ya vyoo vya walimu kutokana na walimu hao kukosa vyoo kabisa shuleni hapo vyoo ambavyo vinajengwa kwa hisani ya Diwani hiyo mteule.

Naye Diwani mteule wa Kata ya Mkambarani, Charles Mboma alisema atahakikisha sekta nyingi ikiwemo ya elimu zinafanya vizuri zaidi katani humo kwa kutumia wataalamu wa fani mbalimbali kufanikisha suala la maendeleo kwenye kata hiyo. 

“Mimi nimejipanga vizuri, ingawa sijaapishwa lakini nimeshaanza kujenga vyoo vya shule ikiwemo shule ya msingi Mkambarani, na walimu pia hawakuwa na vyoo kabisa, tumeshaanza kujenga vyoo vitatu, vya walimu wa kike viwili na wakiume kimoja” alisema Mboma.

Kwa upande wake Afisa elimu kata ya Mkambarani, Irene Mtui alisema kuwa wameshaongea na jamii na kwamba wamekubali kufanya maendeleo katika shule hiyo, ambapo watajenga vyoo na wataanza kunyanyua madarasa kwa kila mwananchi kuanzia umri wa miaka 18 kuchanga kiasi cha shilingi elfu tatu.

error: Content is protected !!