August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ugonjwa wa ajabu Lindi ni homa ya Mgunda

Spread the love

WAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu amesema kuwa upimaji wa sampuli za wagonjwa waliokuwa wakiugua Ugonjwa Usiojulikana katika Wilaya ya Ruangwa katika Mkoa wa Lindi umethibitisha mlipuko huu kuwa ni ugonjwa wa Leptospirosis, Field Fever kwa lugha ya Kiswahili inajulikana kama Homa ya Mgunda. Anaripoti Mwandishi wetu… (endelea).

Katika taarifa iliyotolewa leo tarehe 18 Julai, 2022 na Wizara ya Afya, imebainika kuwa Homa ya Mgunda ni miongoni mwa magonjwa yanayoambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu na unasababishwa na Bakteria aina ya Leptospira interrogans.

“Ugonjwa huu umekuwepo katika maeneo ya kitropiki ambayo ni yenye hali ya joto katika mabara ya Amerika ya Kaskazini, Amerika ya Kusini, Afrika, Asia na Australia. Wanyama aina za panya, kindi, mbweha, kulungu, swala, na wanyamapori wengine wameripotiwa kupata maambukizi ya vimelea hivi na kuwa chanzo cha maambukizi kwa binadamu” amesema Waziri Ummy Mwalimu.

Amesema kuwa Ugonjwa wa Homa ya Mgunda huambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu kupitia uchafuzi wa mazingira ikiwemo vyanzo vya maji kutoka katika mkojo wa wanyama wenye maambukizi.

Waziri Ummy amesema mtu anaweza kupata ugonjwa huo kwa kugusa mkojo (au maji maji mengine ya mwili) kutoka kwa wanyama wenye maambukizi; Kugusa maji, udongo, au chakula kilichochafuliwa na mkojo wa wanyama wenye maambukizi au kunywa maji yaliyochafuliwa na vimelea vya bakteria wa ugonjwa huo huku maambukizi ya ugonjwa huu kutoka kwa binadamu mmoja kwenda kwa mwingine hutokea kwa nadra.

Waziri Ummy amewataka wananchi kuchukua hatua zote stahiki za kujikinga na ugonjwa huo ikiwemo kuepuka kugusa maji au vitu vilivyochafuliwa na mkojo wa wanyama na kunywa maji safi na salama ambayo yamechemshwa au kutibiwa pamoja na kuwataka wagonjwa wenye dalili za homa, kuvuja damu, kichwa kuuma na mwili kuchoka kwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili wapate matibabu sahihi

“Wizara inaendelea kuchukua hatua za kukabiliana na ugonjwa huu na kuendelea kutoa taarifa kwa umma kuhusu mwenendo wa ugonjwa huu. Hivyo Serikali inawaasa Wananchi kutokuwa na hofu kwani ugonjwa huu unaendelea kudhibitiwa” amesema Waziri Ummy Mwalimu.

Ugonjwa huo ulithibitishwa kuibuka na Rais Samia Suluhu Hassan wiki iliyopita wakati akizungumza katika mkutano wa maaskofu wa Afrika Mashariki na kati ambapo alieleza kuwa waziri mkuu, Kassim Majaliwa amemueleza kuna ugonjwa wa ajabu umeibuka mkoani humo.

Aidha, wizara ya afya ilitoa taarifa kuwa ugonjwa huo uliwapata watu 13 ambapo kati yao watatu wamepoteza maisha na wawili wamepona.

Ilisema tarehe 7 Julai, 2022 Mganga Mkuu wa mkoa wa Lindi alitoa taarifa kwa wizara hiyo kwamba kuna ugonjwa wa ajabu umeibuka katika wilaya hiyo ya Ruangwa.

error: Content is protected !!