August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

‘Ugonjwa huu si kimeta’

Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Spread the love

SERIKALI imeeleza kwamba, ugonjwa wa ajabu ulioibuka katika Wilaya za Chemba na Kondoa, Dodoma na kuua watu saba, hauna uhusiano na ugonjwa wa kimeta, anaandika Dany Tibason.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto amesema, tafiti za awali zilizofanywa kwa kushirikiana na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma wamebaini kuwa, ugonjwa huo hauna uhusiano wowote na ugonjwa wa kimeta.

Amesema, ilibainika kuwa ugonjwa huo ulianza kujitokeza baada ya wananchi kula nyama ya ng’ombe ambaye alichinjwa baada ya kuvunjwa mguu katika Kijiji cha Mwai Kisabe, Kata ya Kimaha , Chemba mkoani Dodoma.

Hata hivyo Ummy ameisema, wanakijiji wengine hawakuugua licha ya kutumia nyama hiyo hiyo.

“Mpaka kufikia Juni 18 mwaka huu, kuna wagonjwa 21 ambao kati yao saba, wamefariki na watoto wawili hali zao ni mbaya.”

Amesema, wizara yake imeunda kamati maalum kwa kushirikiana na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya kutibu dalili za ugonjwa huu ili kuzuia maambukizi mapya.

Amesema, timu nyingine ya wataalamu kutoka ngazi ya taifa inayoundwa na daktari bingwa kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhumbili (MNH), wataalamu kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali,TAMISEMI na Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) wanatarajiwa kuwasili mkoani humo ili kuongeza nguvu ya uchunguzi zaidi.

Aidha amesema, timu hiyo itasaidiana na wataalamu wa Sekta ya Kilimo na Mifugo kwa kuwa, inadhaniwa ugonjwa huo uenda ukawa umahusishwa na vyakula vyenye sumu kuvu.

“Vipimo vya awali vilivyofanywa ma maabara kuu ya taifa vinaonesha kutokuwepo kwa homa ya Manjano.Hata hivyo maabara kuu inaendelea kufanya vipimo vingine ikiwemo homa ya Liftvalle” amesema Ummy.

Waziri ameongeza kwamba, wizara yake inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa Afya wakiwemo shirika la Afya Duniani (WHO) na Kituo cha Kuthibiti Magonjwa katika kuhakikisha ugonjwa huo unatambuliwa kwa haraka na hivyo kupunguza wingu la wasiwasi lililowajaa wakazi wa Dodoma juu ya ugonjwa huo.

Dk.James Kiologwe Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma amesema, hali ya wagonjwa waliolazwa katika hospitali hiyo inaendelea vizuri isipokuwa watoto wawili ambao hali zao siyo nzuri.

error: Content is protected !!