June 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ugaidi na hoja nzito ya Muungano

Jaji Mkuu wa Serikali ya Zanzibar, Omar Othman Makungu

Spread the love

SI rahisi kuona kama jambo linalobishaniwa na wanasheria, linalohusu Wazanzibari kukamatwa Zanzibar lakini wakashitakiwa Tanzania Bara, linaweza kuwa na mvuto mkubwa.

Linao. Ndio maana kwenye baraza za mjini Zanzibar, linajadiliwa sana; na tofauti na lilivyoanza kwa wasio wasomi, sasa hao wanalijadili kwa hoja nzito.

Kwa lilipofikia, naona litaendelea kujadiliwa hata baada ya kuwa limeshatolewa uamuzi na Mahakama Kuu Zanzibar.

Chini ya Jaji Mkusa Isaac Sepetu, mahakama imesema haina mamlaka ya kuingilia suala lililoko mahakamani Tanzania Bara.

(Kwa mujibu wa Makubaliano ya Muungano wa Tanzania (Article of Unon), na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, nguvu za kisheria za Mahakama Kuu ya Zanzibar na Mahakama Kuu Tanzania, ziko sawa).

Ni suala linalohusu hatua ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano kuwafungulia mashitaka ya jinai Watanzania wa Kizanzibari – kwa kuwa kwao wazaliwa wa Zanzibar – kwenye Mahakama ya Tanzania Bara, ilhali walikamatwa maeneo mbalimbali mjini Zanzibar.

Ilikuwa Julai, Jeshi la Polisi Tanzania, likishirikiana na Usalama wa Taifa (TISS), walipowakamata Wazanzibari wapatao 20, wengi wao wakiripotiwa kukutwa majumbani mwao Zanzibar, nyakati za usiku.

Baada ya mahojiano mafupi, walipelekwa Dar es Salaam – baadhi kwa njia ya anga (helikopta) na wengine bahari (boti) – ambako walifanyiwa mahojiano marefu Makao Makuu ya Polisi.

Walifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na walikosomewa mashitaka. Waendesha mashitaka, walidai mahakamani watu hao walitenda vitendo hivyo maeneo mbalimbali ndani ya Jamhuri ya Muungano, yakiwemo yaliyoko Zanzibar.

Watu hao, wakiwemo wasomi wa sheria za Dini ya Kiislam na elimu za kidunia kama hisabati na teknolojia ya habari na mawasiliano (TEKNOHAMA), ufundi mwingine pamoja na ualimu, wanashitakiwa chini ya Sheria ya Kudhibiti Ugaidi Tanzania, Na. 2 ya Mwaka 2002.

Wiki moja baadae, kulifunguliwa ombi Mahakama Kuu Zanzibar, wanasheria wakitaka mahakama itamke kuwa wateja wao wamekamatwa na kushitakiwa jinai nje ya Zanzibar, kinyume cha sheria.

Jaji Sepetu alikataa ombi hilo kwa kusema mkono wake kisheria hauwezi kufika Tanzania Bara. Anamaana haina mamlaka ya kuhoji kilichotendwa na mahakama Tanzania Bara.

Alisema hajaona sheria iliyovunjwa, kwa kuwa mashitaka yameandaliwa kwa nguvu ya Sheria ya Jamhuri ya Muungano.

Kwa kuzingatia mazingira ya Muungano – zao la kuunganishwa kwa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar – kila upande una mamlaka kwa mahakama yake, lakini inayohusu ushirikiano ni Mahakama ya Rufaa Tanzania.

Kwa mujibu wa uamuzi wa Jaji Sepetu kwenye Mahakama Kuu ya Zanzibar, wawasilishaji ombi, wanaweza kukata rufaa mahakama hiyo.

Kiongozi wa jopo la mawakili, Abdalla Juma, amesema hawakusudii kukata rufaa.

Wiki iliyopita, siku chache baada ya uamuzi, Chama cha Wanasheria wa Zanzibar (ZLS) kilikutana na waandishi wa habari ambapo walibainisha tatizo la msingi kisheria, na kushauri lishughulikiwe.

ZLS wanaamini haikubaliki mwananchi Zanzibar ambaye hifadhi na haki zake zinalindwa na Katiba ya Zanzibar ya 1984, akamatwe Zanzibar na kushitakiwa Tanzania Bara.

Wanasema kama hiyo inakubalika kisheria, basi isingetamkwa kwenye Katiba kuwa mamlaka ya mahakama ya Bara yanaishia pale yanapoanzia mamlaka kama hayo kwa Mahakama ya Zanzibar – juu yao ni Mahakama ya Rufaa.

Ni mtizamo wao kuwa wananchi hao walipaswa, na wanapaswa, kurudishwa Zanzibar na kushitakiwa kwenye Mahakama Kuu Zanzibar, hasa kwa kuwa makosa wanayodaiwa kuyatenda, yamefanyika pia Zanzibar.

Huku wakikazia hoja ya ulazima wa kwanza kuridhiwa kwa sheria ya ugaidi na Baraza la Wawakilishi, wanaona uvunjaji wa wazi wa haki zao za kibinaadamu kwa kuwashitaki kule ambako ndugu zao hawawezi kufika kushughulikia dhamana.

Ipo namna: Aliyeamua ombi ni mwanasheria na wanaolalamika sheria kuvunjwa, ni wanasheria. Hawa ni wasomi.

Hukutana na kujadiliana yanayohusu taaluma yakiwemo mambo yanayogusa maslahi ya nchi. Raia hutarajia kuona matatizo yanatatuliwa kupitia maamuzi yao.

Lakini, maono yao katika suala hili yanatofautiana. Wale walioko nje ya mahakama – wasio majaji – wanaiona dhulma. Wenzao, huyo jaji, haioni.

Ndipo ninapoona suala hili ni zito. Hoja zinazoibuka zinagusa maslahi makubwa ya Muungano na unavyoendeshwa.

Kwamba je, ipo haki kisheria Jamhuri kukamata Mzanzibari awapo Zanzibar na kumshitaki Bara kwa makosa yanayotajwa pia kutendeka Zanzibar?

Naona suala hili linahitaji mjadala mpana wakati Watanzania wanapohangaikia kupata Katiba mpya inayohusu ushirikiano wa kimuungano.

error: Content is protected !!