January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ufisadi watafuna watano TRA

Spread the love

MAOFISA watano waandamizi kwenye Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wamesimamishwa kazi na italazimu kushitakiwa iwapo itathibitika wametumia vibaya madaraka na kusababisha serikali kukosa mapato ya zaidi ya Sh. bilioni 80 kupitia kodi. Anaandika Mwandishi Wetu … (endelea).

Uamuzi huo umetangazwa leo na Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa alipokutana na uongozi wa juu wa Mamlaka ya Bandari nchini (TPA) pamoja na uongozi wa TRA alipofanya ziara ya kushitukiza bandarini Dar es Salaam.

Maofisa watuhumiwa wametajwa kuwa waliruhusu kutoka kwa makontena 349 ya mizigo pasina wenyewe kulipia kodi inayokisiwa kupita Sh. Bilioni 80.

Waziri Mkuu Majaliwa amemtaka Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade na msaidizi wake ambaye ni Naibu Kamishna Mkuu, Lusekelo Mwaseba kutoa ushirikiana kwa wachunguzi wa Jeshi la Polisi wanaofuatilia taarifa za upotevu wa makontena hayo ikiwemo kusimamia kuhakikisha mapato yaliyokosekana yanapatikana na kurudishwa serikalini.

Kwa mujibu wa taarifa yake, maofisa watuhumiwa waliosimamishwa kazi ni Kamishna wa Forodha, Tiagi Masamaki na Mkuu wa Kituo cha Huduma kwa Wateja, Habibu Mponezya.

“Hawa wanasimamishwa kazi. IGP ninaagiza hawa wakamatwe na kusaidia uchunguzi wa Polisi. Hati zao za kusafiria zikamatwe na mali zao zikaguliwe kama zinaendana na utumishi wa umma,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Maofisa wengine walioadhibiwa ni Mkuu wa TEHAMA, Haruni Mpande, Mkuu wa Kitengo cha Bandari Kavu (ICD), Eliachi Mrema na Hamisi Ali Omari ambaye hakutajwa anakofanyia kazi.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema hao watatu wanasimamishwa kazi mpaka itakapojulikana hatima yao baada ya uchunguzi kukakamilika. Wanatakiwa kushirikiana katika uchunguzi unaofanywa na Polisi.

Pia ameagiza watumishi watatu wa TRA – Anangisye Mtafya, Nsajigwa Mwandengele na Robert Nyoni – waliopo Dar, wahamishiwe vituo vya mikoani.

Katika tukio jingine, Waziri Mkuu Majaliwa amemwagiza Katibu Mkuu wa Hazina, Dk. Servacius Likwelile kupeleka wataalamu kutoka Wakala wa Serikali Mtandao (e-Govt) haraka iwezekanavyo ili wakakague mifumo ya taarifa na kubaini namna wizi huo unafanyika.

“Ninataka uchunguzi uanze mara moja, tafuteni njia ambazo zinatumika kama mianya ya wizi kutokea hapa bandarini hadi kwenye ICDs. Nataka hayo makontena yatafutwe hadi yajulikane yaliko, na fedha hiyo ihakikishwe inarudi serikalini,” amesema huku Dk. Likwelile akishuhudia kwa vile alikuwepo kikaoni.

Hata IGP Ernest Mangu, Makatibu Wakuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk. Florens Turuka, Uchukuzi, Dkt. Shaaban Mwinjaka, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar, Kamishna Suleiman Kova, Mkurugenzi wa TPA, Awadh Massawe walihudhuria.

Kamishna Mkuu wa TRA, Bade alikiri kugundulika upotevu wa makontena unaofanyika kati ya Bandarini na ICDs na hasa ICD Ubungo.

Amesema walifanya ukaguzi kwenye ICD moja na kukuta makontena 54 yamepotea kwa njia za wizi. Ukaguzi ulipoendelea, idadi ya makontena yaliyopotezwa kiudanganyifu iliongezeka kufikia 327. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) inashiriki ukaguzi huo.

Ulipita uamuzi kikaoni kwamba mmiliki wa ICD alipishwe Sh. bilioni 12.6 za faini na tayari ameshalipa Sh. Bilioni 2.4 kwa mujibu wa Kamishna wa TRA, Bade.

Bade alipoulizwa na Waziri Mkuu Majaliwa kama anayo majina ya watumishi wanaotuhumiwa kwa wizi huo, alisema anaweza kuyapata kwa wasaidizi wake baadaye.

Ndipo alipokabidhiwa orodha hiyo na Waziri Mkuu hapohapo kikaoni. Orodha ilikuwa na taarifa za makontena 349 potevu yenye namba za magari yaliyobeba mizigo husika.

“Kwa utaratibu huo hatuwezi kufika, labda baadhi ya watu waondolewe kazini,” amesema Waziri Mkuu na kutaja majina ya maofisa wa kusimamishwa kazi na wale alioagiza wahamishwe kituo cha kazi kwenda mikoani.

error: Content is protected !!