July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ufaulu waongezeka matokeo kidato cha sita

Wanafunzi wa kidato cha sita wa Shule ya Sekondari ya Maposeni, Ruvuma, wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kumaliza mtihani

Spread the love

BARAZA  la Mitihani la Tanzania (NECTA), mnamo Julai 15 mwaka huu, lilitangaza matokeo ya mitihani ya kidato cha sita uliofanyika mwaka 2015 katika shule 584, yakiwemo shule 163 yanayomilikia na watu binafsi na shule  421 zinazomilikiwa na serikali. Anaandika Deusdedit Kahangwa … (endelea).

Kwa mujibu wa tangazo hilo la serikali lililotolewa mjini Zanzibar na  Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde, wa mwaka huu ufaulu umeongezeka kwa asilimia 0.61, kwa maana kwamba umeongezeka kutoka asilimia 98.26 ya mwaka jana mpaka asilimia 98.87 mwaka huu.

Kwa mujibu wa Dk Msonde kati ya watahiniwa 40,753 waliofanya mitihani hiyo ya kumaliza kidato cha sita, jumla ya watahiniwa 38,853 wamefaulu, japo kwa madaraja tofauti. “Kati ya wanafunzi hawa waliofaulu, wasichana ni 11,734 wakati  wavulana ni 27,119,” alifafanua. Matokeo yote yanapatikana katika tovuti ya NECTA kwa kutumia anwani pepe ufuatayo: http://necta.go.tz/matokeo/2015/Alevel.htm

Hata hivyo, “watahiniwa 35 walishindwa kufanya mitihani yao baada ya kuugua ghafla,” amesema  Dk. Msonde.

Haya ni matokeo ya kwanza ya kidato cha sita tangu serikali ilipotangaza viwango vipya vya alama za ufaulu katika elimu ya sekondari mnamo Aprili 2014. Kwa mujibu wa mfumo huu mpya, viwango vya ufaulu ni kama ifuatavyo:

Gredi A ina maana ya ufaulu uliojipambanua (distincion or outstanding performance), na inaanzia alama 75 mpaka alama 100. Gredi B+ ina maana ya ufaulu bora sana (excellent performance), na inaanzia alama 60 mpaka alama 74. Gredi B ina maana ya ufaulu mzuri sana (very good perfomance), na inaanzia alama 50 mpaka alama 59.

Gredi C ina maana ya ufaulu mzuri (good performance), na inaanzia alama 40 mpaka alama 49. Gredi D ina maana ya ufaulu wa wastani (low performance), na inaanzia alama 30 mpaka alama 39. Gredi E ina maana ya ufaulu hafifu (very low performance), na inaanzia alama 20 mpaka alama 29. Gredi F ina maana ya ufaulu usioridhisha (unsatisfactory performance), na inaanzia alama 0 mpaka alama 19.

Kuanzia mtihani wa kidato cha nne wa mwka 2014 na mtihani wa kidato cha tano sita wa mwaka 2015 serikali inapanga ufaulu wa mwanafunzi kwa kutumia mfumo wa “wastani wa uzito wa pointi za gredi” husika (Grade Point AverageGPA).

Mfumo wa “Grade Pointi Average” huonyesha wastani wa pointi alizopata mtahiniwa katika masomo aliyofaulu katika mtihani wake. Madaraja katika mfumo wa GPA hupangwa katika utaratibu wa Distinction, Merit, Credit na Pass, ambapo daraja la Distinction ni la ufaulu wa juu zaidi na daraja la Pass ni la ufaulu wa chini.

Mtahiniwa hutunukiwa gredi A, B+, B, C, D, E au F kutegemeana na ufaulu wake katika masomo. Uzito wa alama hizi ni kama ifuatavyo: gredi A pointi 5, gredi B+ pointi 4, gredi B pointi 3, gredi C pointi 2, gredi D pointi 1, gredi E pointi 0.5 na gredi F pointi 0. Katika mpangilio huu, mtahiniwa atahesabiwa kuwa amefaulu somo endapo atapata gredi D ambayo ni sawa na uzito wa pointi 1. 

Ukokotoaji wa jumla ya GPA ya mtahiniwa hufanyika kwa kuzingatia masomo ambayo mtahiniwa amefaulu angalau kwa gredi D na kuendelea. GPA anayopata mtahiniwa hutokana na wastani wa pointi alizopata katika masomo saba aliyofanya vizuri zaidi kwa mtihani wa kidato cha nne au masomo matatu ya tahasusi kwa mtihani wa kidato cha sita.

Aidha, GPA ya mtahiniwa huandikwa katika nafasi moja ya desimali ambamo nafasi ya pili ya desimali hukadiriwa katika makumi yaliyo karibu. Mfano, mtahiniwa mwenye GPA ya pointi 3.14 anakuwa na GPA ambayo ni sawa na pointi 3.1 tu.

Kwa mujibu wa mfumo huu mpya, muundo wa madaraja kwa kutumia GPA katika mitihani ya kidato cha sita ni kama ifuatavyo: Daraja la kwanza (distinction) pointi 3.7 mpaka 5.0; daraja la pili (merit) pointi 3.0 mpaka 3.6; daraja la tatu (credit) pointi 1.7 mpaka 2.9; daraja la nne (pass) pointi 0.7 mpaka 1.6; na daraja la tano (fail) pointi 0.0 mpaka 0.6. 

Na kwa kidato cha nne muundo wa madaraja kwa kutumia GPA ni kama ifuatavyo: Daraja la kwanza (distinction) pointi 3.6 mpaka 5.0; daraja la pili (merit) pointi 2.6 mpaka 3.5; daraja la tatu (credit) pointi 1.6 mpaka 2.5; daraja la nne (pass) pointi 0.3 mpaka 1.5; na daraja la tano (fail) pointi 0.0 mpaka 0.2. 

Huu ndio mfumo uliotumiwa na serikali mwaka huu kupanga matokeo ya kidato cha sita, ikiwa ni mara yake ya kwanza kuutumia tangu ubuniwe mwaka jana.

error: Content is protected !!