June 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ufafanuzi wa Kamishna wa Sensa kutangaza nia ya ubunge

Risiti aliyopewa Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 baada ya kulipia ukumbi wa Idara ya Habari

Spread the love

 

TAARIFA KWA UMMA

UFAFANUZI KUHUSU KAMISHNA WA SENSA KUTANGAZA NIA YA KUGOMBEA UBUNGE KATIKA JIMBO LA KITETO

Kuna taarifa imetolewa na moja ya Magazeti ya Mitandao (Online Newspapers) ikisema kuwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imemgharamia Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 ili kumuwezesha kutangaza nia ya kugombea Ubunge kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika jimbo la Kiteto mkoani Manyara.

Gazeti hilo la kwenye Mtandao limetoa taarifa hiyo tarehe 08 Juni, 2015 likiihusisha Ofisi ya Taifa ya Takwimu kuhusika na ufadhili wa gharama alizotumia Kamishna kama Mtumishi wa Umma wakati akitangaza nia yake ya kugombea Ubunge katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba, 2015.

Ofisi ya Taifa ya Takwimu inakanusha taarifa hiyo kuwa si ya kweli bali ni uzushi mtupu.

Ukweli ni kwamba, NBS haijahusika kwa gharama zozote zinazohusiana na kutangaza nia kwa Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012.

Gharama zote zilizotumika katika mchakato wa kutangaza nia zimetolewa na mhusika mwenyewe ambaye ni Hajjat Amina Mrisho Said, Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012.

Kudhihirisha hilo, risiti iliyotumika kulipia gharama hizo imeandikwa kwa jina la mhusika mwenyewe kama inavyoonekana hapa chini.

Kamishna akiwa mtumishi wa Umma amefikia uamuzi wa kutangaza nia yeye binafsi na wala si kwa kutumwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu. Kamishna amefanya hivyo kwa kutumia haki yake ya Kikatiba ya kuchagua au kuchaguliwa kuwa kiongozi katika nafasi yoyote ya uongozi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha, kwa mujibu wa Waraka wa Utumishi wa Umma Na. 1 wa mwaka 2000 Kuhusu Maadili ya Watumishi wa Umma katika Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa pamoja na mambo mengine, unaweka wazi kuwa, Mtumishi atakayeamua kugombea nafasi yoyote ya kisiasa, atatakiwa kutoa taarifa rasmi kwa mamlaka yake ya ajira. Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 ametekeleza agizo hilo kwa kuzingatia Waraka husika.

Ofisi ya Taifa ya Takwimu inaendelea kusisitiza kuwa, Hajjat Amina Mrisho Said ametangaza nia kwa kutumia gharama zake mwenyewe na siyo Ofisi ya Taifa ya Takwimu kama ilivyoripotiwa na gazeti hilo la kwenye       Mtandao.

Imetolewa na: Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Ofisi ya Taifa ya Takwimu,

Dar es Salaam,

09 Juni, 2015.

error: Content is protected !!