August 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

UDSM waungana kuchangia waliokosa mikopo

Shamira Mshangama, Makamu wa Rais wa Serikali ya wanafunzi – DARUSO

Spread the love

WANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), wameamua kuchangishana ili kuwasaidia wenzao waliokosa mikopo kuendelea na masomo, anaandika Charles William.

Hivi karibuni kumekuwa na mfululizo wa matangazo ya wanafunzi wa UDSM waliokosa mikopo wakiomba msaada wa fedha za ada kutoka kwa wasamaria wema kupitia mitandao ya kijamii huku wengine wakiomba angalau nauli tu ili waweze kurudi nyumbani – mikoani.

Taarifa iliyotolewa na Shamira Mshangama, Makamu wa Rais wa Serikali ya wanafunzi – DARUSO imeeleza kuwa utaratibu maalum wa kuwachangia wanafunzi wa mwaka wa kwanza walioshindwa kufanya usajili kutokana na kukosa ada umeandaliwa na utatangazwa hivi karibuni.

Akizungumza na MwanaHALISI Online mapema leo kuhusu suala hilo amesema;

“Kwa sasa hivi tunataka kuwasaidia angalau hawa waliobaki chuoni huku wakiendelea na masomo kwa miezi miwili sasa lakini hawajalipa ada na wanaomba msaada, wakati huo tukiendelea kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa suala hili kwasababu vijana hao wengi wana sifa za kupata mikopo,” amesema.

Amefafanua kuwa miongoni mwa wanafunzi wa UDSM waliokosa mikopo wapo walemavu, yatima, waliosoma shule za kata, wanaotoka familia duni na wanaosoma masomo yaliyotajwa na serikali kuwa ni miongoni mwa vipaumbele vyake.

“Tutachangishana fedha za kuwalipia ada, wakati huo tukisubiri majibu ya rufaa zao walizokata kwa bodi ya mikopo (appeals) kwani wengi wana sifa za kupata mikopo kutoka serikalini. Hatutakubali wanafunzi hawa waliopo chuoni mpaka sasa hivi wakiendelea na masomo waondoke kwa kukosa ada,” amesema.

Shamira ameeleza kuwa wameandaa utaratibu mzuri wa kukusanya michango kutoka kwa wanafunzi wa chuo hicho, viongozi wa DARUSO na wadau mbalimbali wa maendeleo ndani na nje ya chuo na kwamba wana uhakika wa kukamilisha zoezi hilo mwanzoni mwa wiki ijayo kabla ya likizo ya sikukuu ya Christmas na mwaka mpya.

“Wanafunzi hawa wanatakiwa kulipa ada haraka na kupata vitambulisho vya chuo ili waweze kupata uhalali wa kufanya assignments na tests (majaribio), kwahiyo kabla ya wiki ijayo kuisha tutakuwa tumeshakusanya michango na kabla ya Ijumaa ya wiki ijayo tutakuwa tumeshawalipia ada zao,” amesisitza.

Itakumbukwa kuwa, mapema mwezi Oktoba mwaka huu, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) ilitangaza kutoa mikopo kwa wanafunzi 3,996 kati ya wanafunzi zaidi ya 8,000 wa mwaka wa kwanza wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam jambo linalosababisha wengi washindwe kujisajili na kuendelea na masomo.

Abdul-Razaq Badru, Mkurugenzi wa HESLB amekuwa ikisisitiza kuwa wanafunzi wanaojiona wana sifa za kupata mikopo na wamenyimwa wakate rufaa kwa bodi hiyo.

error: Content is protected !!