BENKI ya NMB imeendelea kufanya kazi kwa karibu na Asasi ya Tawala za Mitaa (ALAT Taifa), ikiwemo kudhamini Mikutano yake Mikuu ya Mwaka kwa takribani miaka 7 mfululizo, na hadi sasa jumla ya Sh. 1.2 bilioni zimeshatumika. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Makamu wa Rais wa Tanzania Dk. Philip Mpango akielezewa mafanikio na mipango iliyopo kati ya Benki ya NMB na ALAT Taifa katika ngazi zote, Afisa Mkuu Wateja Wakubwa na Serikali wa NMB, Alfred Shao, alipotembelea banda la NMB katika viwanja vya AICC Arusha, ulipokua unafanyika Mkutano Mkuu wa 37 wa ALAT Taifa.
Haya yamesemwa na Afisa Mkuu Wateja Wakubwa na Serikali wa NMB, Alfred Shao wakati akiwasilisha mada katika Mkutano wa 37 wa ALAT uliofanyika kwa siku tatu katika ukumbi wa AICC- Arusha ambapo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Philip Mpango alikuwa mgeni rasmi.

Mkutano huo uliokuwa na kauli mbiu inayosema “Miundombinu iliyoboreshwa ni chachu ya utoaji wa huduma bora katika Mamlaka za Serikali za Mitaa” uliwakutanisha zaidi ya watumishi 500 kutoka Halmashauri zote 184 za Majiji, Manispaa, Wilaya na Miji kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
Aidha, Shao alielezea kuwa, Benki ya NMB kama mdau wa maendeleo kupitia Halmashauri zote chini, imekuwa mshirika mkubwa kuboresha miundombinu ya elimu, afya, usafirishaji na mazingira.

Alisema pia NMB inaendelea kushiriki kikamilifu katika kutoa dhamana kwa kandarasi zaidi ya 580 zenye thamani ya Sh 49 bilioni katika hatua zote kuanzia hatua ya kuomba na kutekeleza miundombinu chini ya TARURA.
Alisema kupitia mifumo na mtandao mpana wa NMB umesaidia Serikali katika makusanyo ya mapato ya zaidi ya Sh. 9.8 trilioni kuanzia mwaka 2018.
“Lakini pia, kwenye utunzaji wa mazingira tumezindua kampeni ya upandaji miti milioni moja nchi nzima, ambapo hadi sasa tumepanda miti zaidi ya 550,000.
“NMB imetenga kiasi cha Sh 472 milioni kama zawadi katika kampeni ya Tunza Mti Tukutuze kwa shule za Halmashauri zote Bara na Visiwani kushirikiana na Wizara ya TAMISEMI,” amesema.
Akisisitiza umuhimu wa kuyatunza mazingira kwa ajili ya maendeleo endelevu, Dkt. Mpango alizihamasisha Halmashauri kushiriki kikamilifu na kuwataka kufanya kama NMB walivyofanya kwenye kampeni ya kupanda miti milioni moja ambapo kwa kushirikiana na TAMISEMI wameandaa shindano la shule la upandaji miti lenye zawadi.
Leave a comment