August 4, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Udhamini wa Makonda waingia doa

Spread the love

WANANCHI waliojitokeza katika zoezi la kupima afya zao lililoanza Jumamosi na Jumapili wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, wamelalamikia mpango mbovu wa huduma hiyo, anaandika Aisha Amran.

Wamesema, huduma hiyo imekuwa ya kuchelewa na kwamba, wamechukua namba mapema lakini mpaka jana hawakuwa wamehudumiwa.

Zoezi hilo lililotarajiwa kumalizika jana, limeongezwa siku mbili na sasa litamalizika kesho kutokana na kuwepo kwa idadi kubwa ya watu waliojitokeza.

Upimaji afya huo ulidhaminiwa na Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa lengo la kuhamasisha wananchi kuwa na tabia ya kwenda kupima afya zao mara kwa mara.

Akizungumza na mwanahalisionline, Salumu Moshi, mwananchi aliyekwenda kupata huduma hiyo Mnazimmoja amelalamika kuwa, huduma hazikidhi mahitaji kwasababu watoa huduma ni wachache ukilinganisha na watu waliojitokeza.

“Huduma za hospitali ni gharama sana kwani mpaka umuone dakitari lazima utoa kwanza kiasi cha shilingi 30,000 ambapo kwa hali ya Mtanzania wa chini hawezi kumudu na ndio maana kukitokea huduma kama hizi ambazo hutolewa bure, watu tunakauwa wengi sana,” amesema Moshi.

Moses Michael amesema, endapo hospitali wangepunguza gharama za kupima afya ya mwili, watu wengi wasingejitokeza mpaka watoa huduma kuelemewa.

“Baadhi ya watu walioendelea kujitokeza walirudishwa nyumbani kwa kukosa huduma ya namba ambazo mwazo zilitolewa kwa zaidi ya watu 11,200,” amesema.

Joseph Masanzo, Famasia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam amesema, lengo la huduma hiyo ni kuwahamasisha wananchi kuwa na tabia ya kupima afya zao mara kwa mara.

Amesema, hawakutegemea kama watajitokeza kwa wingi kiasi hicho na kwamba, kutokana na ongezeko la idadi ya watu kinyume na matarajia yao, wameongeza siku mbili zaidi (Jumatatu na Jumanne).

“Mategemeo yetu ni kutoa huduma kwa jumla ya watu 3000 na tuwahudumie kwa siku mbili lakini imekuwa kinyume kwani wamejitokeza zaidi ya idadi tuliyotegemea, mpaka tukaamua kuongeza siku ili kila mtu apate huduma.”

Amesema, awali wananchi hawakuwa na uelewa mzuri hivyo walitoa huduma taratibu.

“Tunashukuru wananchi kujitokeza kwa wingi lakini mpaka leo tumeshahudumia zaidi ya watu 6000 ukilinganisha na idadi tuliyoandikisha na huduma ambazo tunazitoa hapa ni kupima presha, figo, kisukari, virusi vya Ukimwi, tezi dume na mwagonjwa mengine,” amesema Masanzo.

 

error: Content is protected !!