September 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

UDA yazikwa rasmi

Spread the love

BARAZA la Madiwani wa Jiji la Dar es Salaam, wametembelea vyanzo vya mapato na kuamizia mambo nane ya kutekeleza, anaandika Happiness Lidwino.

Katika kikao chao kilichofanyika tarehe 2 Mei mwaka baraza limeazimia kupitia taarifa ya viwanja vilivyopimwa na halmashauri ya jiji, taarifa za mikopo kwa kina mama na vijana, taarifa za ujenzi wa vituo vya mabasi yaendayo mikoani, ujenzi na uboreshaji wa madampo, miradi ya jiji na mingine.

Isaya Mwita Meya wa Jiji hilo akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake amesema kuwa Baraza lilibatilisha uuzwaji wa hisa za Halmashauri ya jiji ambazo ni asilimia 51 zilizo katika Shirika la Usafirishaji Dar es Salaam (UDA) baada ya kugundua mnunuzi wa hisa hizo hakufuata utaratibu.

Mwita amesema Baraza la madiwani lilijiridhisha kuwa, hakuna kumbukumbu zinazoonesha kuwa mwanahisa mwenza kwamaana ya msajili wa hazina kuridhia uuzwaji wa hisa hizo. Pia ziliuzwa bila kuzingatia sheria ya manunuzi.

Pia, hakukufanyika uthaminishaji wa mali za UDA kabla ya kuuzwa hisa zake, nakwamba fedha zilizolipwa kwa halmashauri ya jiji na Kampuni ya Simon Group Ltd kwaajili ya kununuliwa hisa zisirudishwe hadi hapo tathmini ya kina itakapofanyika na kujiridhisha kuwa kampuni hiyo haidaiwi.

Mwita amesema, Baraza pia liliazimia kuundwa kwa kamati ndogo ya uchunguzi wa kina kuhusiana na ubatilishwaji wa uuzwaji wa hisa za halmashauri ya jiji. Kamati hiyo imeundwa na, Halima Mdee Mbunge wa Kawe, Abdallah Mtolea Mbunge wa Temeke na Jumanne Mtinangi ambaye ni Mwanasheria wa jiji.

Baraza pia lilishauri mikopo ya kina mama na vijana iwekwe wazi na kuwepo mfumo utakao tumika kupata idadi ya vikundi hivyo ambapo halmashauri itatumia benki ya DCB kukopeshea ili iwe rahisi kurejesha, Pia Baraza lilishauri kuendelea kutumia kituo cha ubungo huku mchakato wa kujenga kituo kipya ukiendelea.

Mwita amesema kuwa, Baraza pia lilitaka kujua uhalali wa miradi ya jiji ambapo kwa pamoja liliazimia miradi hiyo ianze kufanyiwa uchunguzi ambao tayari umeanza, ikiwa ni pamoja na kupitia miradi ya viwanja vya kigamboni na sehemu nyingine.

Aidha, Meya huyo amesema anapambana ili kuwatafutia wananchi mali zao zinazomilikiwa na vigogo kwa masilahi yao ili azirejeshe kwa wananchi ambapo ameahidi kulitekeleza hilo.

error: Content is protected !!