January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

UDA yachochea umaskini Dar

Mabasi ya UDA

Mabasi ya kampuni ya Usafiri Dar es Salaam (UDA) yakiwa kwenye maegesho yake kabla ya kuanza kazi

Spread the love

SHIRIKA la usafiri Dar es Salaam (UDA), lililokuwa mkombozi wa wanyonge, limegeuka “Jehanam,” imefahamika.

Gharama za usafiri jijini zimeongezeka; uhaba wa mabasi ya abiria umekuwa mkubwa; ustaarabu wa wafanyakazi wa mabasi umepungua na mvua ya matusi kwa wafanyakazi wa daladala imehalalishwa.

Taarifa kutoka vyanzo mbalimbali jijini Dar es Salaam zinasema, tangu UDA ibinafsishwe kwa muwekezaji mwenye utata – kampuni ya Kisena Group – watumiaji wa usafiri wa umma wanaendelea kuteseka.

Habari zinasema, magari yote yaliyokuwa yakiingia Kivukoni kutoka maeneo ya jiji yamezuiwa, badala yake kibali cha kuingia katika eneo la Kivukoni kimekabidhiwa kwa UDA, jambo ambalo linasababisha kuwapo na uhaba mkubwa wa mabasi.

“Mabasi yanayoruhusiwa kuingia Kivukoni, ni UDA tu. Mengine yote yanaishia Mnazi Mmoja. Haya mabasi ya UDA yanayokwenda Kivukoni, yanaanzia safari zake Mnazi Mmoja, kitendo ambacho kinaongeza gharama ya maisha,” ameeleza Mohamed Hassan, mkazi wa Mwananyamala.

Anasema, “Kabla ya UDA kubinafishwa, tulikuwa tunapanda basi moja kutoka Mwananyamala hadi Kivukoni na Mwananyamala hadi Mwenge. Nauli ya basi hilo ilikuwa Sh. 800 kwa safari ya kwenda na kurudi.”

Anasema, “Lakini sasa tunalazimika kutumia Sh. 1600 kwa sababu hakuna gari zinazofika Mwenge wala Kivukoni kutoka Mwananyama. Ukitaka kwenda Kivukoni, kutoka hapa Mwanyamala utalazimika kwenda hadi Mnazi Mmoja, au posta. Kisha utalazimika kusubiri basi ya UDA inayoanzia safari zake Mnazi Mmoja.”

Anahoji, “Kama UDA walipewa kibali cha kwenda Kivukoni kwa nini wanaishia Mnazi Mmoja? Kwa nini wasianzie Kimara; Mbezi; Tegeta, Gongolamboto, Tabata au Mbagara?

MwanaHALISI Online limebaini kuwa waathirika wakubwa wa usafiri jijini, ni wananchi wenye kipato cha chini ambao hulazimika kuamka kati ya saa tisa na saa 10 alfajiri.

Wakazi hawa wanalazimika kutembea kwa miguu muda wa saa mbili hadi tatu kwenda kazini.

“Kipato changu kwa siku ni Sh. 2500. Usafiri wa basi kutoka Mbagala ninakoishi mpaka Kivukoni ninakofanyia shughuli zangu, hunigharimu Sh. 1800 kwa safari ya kwenda na kurudi. Hii ni kwa sababu, ili nifike Kivukoni, sharti nishuke Mnazi Mmoja ndipo nipate gari ya kwenda Kivukoni ambalo ni hili la UDA,” ameeleza Juma Mkumba.

Mbali na tatizo la serikali kumilikisha UDA njia kuu ya kwenda Kivukoni, magari ya shirika hilo yamekuwa yakifanya kazi zake nje ya utaratibu unaotumiwa na magari mengine.

Miongoni mwa taratibu zinazokiukwa, ni kukatisha safari za mabasi hayo.

Mmoja wa madereva wa mabasi ya UDA aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa gazetini amesema, tatizo la “kukatisha ruti” linatokana na hesabu kubwa waliyopangiwa na mmiliki wa shirike hilo.

Amesema, “Tumepangiwa kupeleka Sh. 205,000 kwa kila siku. Hesabu isipotimia unakatwa mshahara. Hivyo ili kukabiliana na tatizo hilo, tunalazimika kukatisha safari hasa zinazotumia muda wa mwingi njiani.”

Afisa elimu wa baraza la watumiaji wa usari wa nchi kavu na majini Nicholaus Kinyiriri, amekiri kuwa UDA imekuwa kero badala ya tiba ya usafiri jijini.

“Ninafahamu malalamiko ya wananchi juu ya UDA. Tatizo la magari kutofika Kivukoni linashughulikiwa. Tunawaomba wananchi watusaidie kutoa taarifa pale wanapomuona dereva anakatisha ruti,” ameeleza Kinyiriri.

Msemaji wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), hakupatikana kujibu swali la mwandishi, ni hatua gani zinachukuliwa kwa UDA kukatisha ruti.

error: Content is protected !!