May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Uchunguzi tukio la Lissu kupigwa risasi waibuka kesi ya Mbowe

Tundu Lissu, Aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki akiwa hospitali ya Nairobi nchini Kenya

Spread the love

 

MPELELEZI wa Makosa ya Jinai, Goodluck Minja, amedai hafahamu kama ripoti ya uchunguzi wa tukio la aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, imeshatolewa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Minja ambaye ni Mpelelezi katika Kituo Kikuu cha Polisi Arusha, ametoa madai hayo leo Jumatatu, tarehe 24 Januari 2022, akitoa ushahidi wake katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Dar es Salaam, mbele ya Jaji Joachim Tiganga.

Ametoa ushahidi wake kwenye kesi ya uhujumu uchumi namba 16/2021, inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na walinzi wake ambao walikuwa makomandoo wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Halfan Bwire Hassan, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Ling’wenya.

Baada ya Wakili wa utetezi, Dickson Matata, kumuuliza kama anafahamu kuhusu kutolewa kwa ripoti ya uchunguzi wa tukio hilo, lililotokea tarehe 7 Septemba 2017, jijini Dodoma.

Mahojiano kati ya Wakili Matata na Minja, kuhusu ripoti ya uchunguzi huo, yalikuwa kama ifuatavyo;

Matata: Wakati unatoa ushahidi wako ulisema wakati unafanya ukamataji wewe ulikuwa ni detective coplo?

Shahidi: Sio sahihi

Matata: Ulikuwa nani?

Shahidi: Nilikuwa detective

Matata: Kwa maana ya kwamba ulikuwa mpelelezi?

Shahidi: Ni mpelelezi

Matata: Utakubalina na mimi kwamba kwa nafasi hiyo ulikuwa unatakiwa pia kufuatilia vyombo vya habari na Bunge ili uweze kupata taarifa nyingi ndani na nje ya nchi?

Shahidi: Kufuatilia habari ni jambo la kawaida kama unataka kufuatilia.

Matata: Kwa hiyo kama ulivyosema ulikuwa unafuatilia, uliwahi kusikia juu ya kuvamiwa na kupigwa risasi kwa mtu anayeitwa Tundu Lissu huko mkoani Dodoma?

Shahidi: Ndiyo nilisikia.

Matata: Na unafahamu kwamba huyo Tundu Lissu ni kiongozi wa Chadema?

Shahidi: Pia nafahamu.

Matata: Na kwamba alipigwa risasi hizo akiwa Dodoma kwenye shughuli zake za kibunge?

Shahidi: Nilisikia hivyo.

Matata: Kama ulifuatilia uliwahi kusikia juu ya uchunguzi wa kupigwa kwake risasi uliowahi kufanyika na ripoti kutolewa?

Shahidi: Tukio limetokea uchunguzi kufanyika ni lazima.

Matata: Ripoti ya uchunguzi ilitolewa?

Shahidi: Sijafuatilia kuona kama uchunguzi umefanyika au haujafanyika.

Matata: Je, kufahamu ripoti imetoka au haijatoka kuhusu uchunguzi huo?

Shahidi: Sifahamu

Lissu, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema- Bara, baada ya kushambuliwa kwa risasi alipata matibabu jijini Nairobi nchini Kenya na nchini Ubelgiji anakoishi hadi sasa.

Shahidi huyo wa 11 wa Jamhuri, anaendelea kutoa ushahidi wake mahakamani hapo, kwa kuulizwa maswali ya dodoso na mawakili wa utetezi.

error: Content is protected !!