October 21, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Uchaguzo mdogo; ACT- Wazalendo, CCM wagawana majimbo

Emmanuel Peter Cherehani, mgombea wa CCM aliyeshinda Ubunge jimbo la Ushetu

Spread the love

VYAMA vya ACT – wazalendo na CCM vimegawana majimbo Konde Visiwani Zanziba na Ushetu mkoani Shinyanga katika uchaguzi mdogo uliofanyika jana tarehe 9 Oktoba mwaka huu. Anaripoti Ulwe Ulwe (endelea).

Hatua hiyo imekuja baada ya Mgombea wa ACT Wazalendo, Mohamed Said Issa kutangazwa mshindi katika uchaguzi mdogo wa Jimbo Konde kwa kupata kura 2391 kati ya kura 3,338 zilizopigwa.

Wakati mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Jimbo la Ushetu, Emmanuel Cherehani ameshinda uchaguzi huo kwa kupata kura 103,357 sawa na asilimia 96.6 ya kura zote zilizopigwa jimboni hapo.

Awali vyama vya siasa 16 vilijitokeza kuchukua fomu ya kugombea jimbo hilo la Ushetu lakini vyama 14 vilikosa sifa na baadhi yao kushindwa kurejesha fomu mpaka muda ulipokwisha huku CCM na ACT Wazalendo vikikidhi vigezo na kugombea.

Kwa mujibu wa Msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la Ushetu, Mwalimu Lino Pius, idadi ya wapiga kura waliojiandikisha ni 165,418 lakini waliopiga kura walikuwa 107188.

Amesema kati ya kura hizo idadi halali ya kura zilizopiga zilikuwa 106,945, idadi ya kura zilizokataliwa zilikuwa kura 243, huku mgombea wa ACT Wazalendo Julius Nkwabi Mabula akipata kura 3588 sawa na asilimia 3.4.

Mohamed Said Issa, mgombea wa ACT Wazalendo aliyeshinda Ubunge jimbo la Konde

Uchaguzi huo katika jimbo la Ushetu umefanyika baada ya aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Elias Kwandikwa kufariki duniani tarehe 3 Agosti mwaka huu.

Aidha, kwa upande wa jimbo la Konde, Msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo Abdallah Said Ahmed amesema Issa amefuatiwa na mgombea wa CCM, Mbarouk Amour Habib aliyepata kura 794 kati ya kura 3,338 zilizopigwa.

Mgombea mwingine katika uchaguzi huo Salama Khamis Omar wa CUF alipata kura 98 na Hamad Khamis Mbarouk (AAFP) akipata kura 55.

Uchaguzi huo katika jimbo la Konde ulifanyika kwa mara ya tatu baada ya Khatib Haji aliyekuwa mbunge wake kufariki duniani tarehe 20 Mei, mwaka huu, hata hivyo katika uchaguzi mdogo wa tarehe 19 Julai, Sheha Mpemba Faki CCM), alishinda lakini ilipofika tarehe 4 Agosti mwaka huu alijiuzulu kutokana na changamoto za kifamilia.

error: Content is protected !!