September 25, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Uchaguzi Zambia wawaibua wanasiasa, wanaharakati Tanzania

Hakainde Hichilema, Rais wa Zambia

Spread the love

 

USHINDI wa aliyekuwa mgombea urais wa upinzani nchini Zambia, Hakainde Hichilema, katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 12 Agosti 2021, umeacha fundisho kwa vyama vya siasa nchini Tanzania. Anaripoti Noela Shila, TURUDACo … (endelea).

Maneno hayo yametolewa katika nyakati tofauti na wanasiasa, wanaharakati pamoja na wananchi wa kawaida, kupitia mtandao wa Twitter, baada ya Tume ya Uchaguzi Zambia (ECZ), kumtangaza Hichilema mshindi, akimbwaga Rais aliyemaliza muda wake, Edgar Lungu.

Jana tarehe 15 Agosti 2021, tume hiyo ilimtangaza Haichilema mshindi wa kiti cha urais, baada ya kupata kura 2,810,777, huku Lungu akishika nafasi ya pili kwa kupata kura 1,814,201.

Katika uchaguzi huo, Hichilema aligombea kupitia Chama cha United Party for National Development (UPND) na Lungu akiwa mgombea wa Chama cha Patriotic Front (PF).

Akizungumzia uchaguzi huo, Mwanaharakati wa haki za binadamu Tanzania, Ananilea Nkya, amesema matokeo ya uchaguzi huyo yanaonesha dhahiri matunda ya jitihada za Rais wa Kwanza wa Taifa hilo, Hayati Keneth Kaunda, za kuimarisha na kulinda misingi ya demokrasia.

“Keneth Kaunda Rais wa Kwanza wa Zambia, Mungu aitunze roho yake mbinguni. Uamuzi wake kuachia demokrasia ichukue mkondo, wakati Wazambia walipomkataa kupitia sanduku huru la kura katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi 1992, naye akaheshimu, alitengeneza Zambia ya leo,” ameandika Nkya.

Fatma Karume

Amos Omary, amesema chama cha upinzani nchini Tanzania kitafanikiwa kutwaa madaraka endapo kutakuwa na katiba mpya pamoja na tume huru ya uchaguzi,.

“Mpaka siku ikipatikana katiba mpya na tume huru ya uchaguzi, tutapata mabadiliko lakini bila hivyo CCM (Chama Cha Mapinduzi) itaongoza milele, save this tweet (hifadhi tweet hii),” ameandika Omary.

Naye aliyekuwa Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Fatma Karume, amesema ili kufikia mafanikio ya Zambia, tume huru ya uchaguzi ni muhimu “tume huru ni muhimu sana.”

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema, ameuzungumzia uchaguzi huo akisema, Hichilema ameingia madarakani baada ya wananchi kuamua kupitia sanduku la kura.

Godbless Lema

“Zambia wameamua kufanya kampeni, kupiga kura na kulinda kura na sasa wana utawala mpya, Rais Hakainde Hichilema,” ameandika Lema katika ukurasa wake wa Twitter.

Kwa upande wake Hance machemba ameandika “siku yaja hata Tanzania nayo itatoka katika utawala wa chama kimoja na wengine kushika madaraka ya nchi.”

Omary Shemdoe, amevishauri vyama vya siasa, vijifunze siasa za Zambia, kama vinataka kuingia madarakani.

“My advice kwa sisi wapinzani tukajifunze kwao, jinsi ya kuitoa CCM madarakani kama wao wanavyofanya,” ameandika Omary.

Tangu Tanganyika na Zanzibar ziungane mwaka 1964 na kuunda Tanzania, Taifa hilo halijawahi kuongozwa na chama cha upinzani, bali limeongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), zaidi ya mitano.

error: Content is protected !!