January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Uchaguzi watawala Bunge la Bajeti

Spread the love

MKUTANO wa 20 wa Bunge la 10, umeanza leo kwa mbwembwe za aina yake, huku joto la uchaguzi mkuu wa mwaka huu, likionekana kutawala mjadala kati ya wabunge wa upinzani na CCM. Anaandika Edson Kamukara … (endelea).

Mvutano mkali ulianza kujitokeza jioni wakati Kiongozi Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, akisoma maoni ya kambi yake kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya fedha katika Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2015/2016.

Chanzo cha mzozo huo baina ya Mbowe, Spika Anne Makinda na wabunge wa upinzani ni baada ya mgawanyo wa muda wa dakika 90 walizokuwa wamepewa kambi ya upinzani kuwasilisha maoni yao kufanyiwa marekebisho bila spika kupewa taarifa.

Kwa mujibu wa kanuni za Bunge, Msemaji mkuu anapewa dakika 90, ambapo Mbowe na wasemaji wawili katika ofisi hiyo, kila mmoja alikuwa na dakika 30 za kuwasilisha sehemu ya hotuba yake; ingawa mabadiliko ya upinzani yalitaka Mbowe atumie dakika 50 na wezake 20, spika akakataa.

Hatua hiyo iliibua mabishano kwa dakika takribani tatu kati ya Spika na wabunge wawili watatu wa Chadema, Tundu Lissu, David  Silinde na Pauline Gekul wakitaka Mbowe aheshimiwe na kutendewa haki.

Malalamiko yao hayakubadili msimamo wa spika, ndipo Lissu akiwa mchangiaji wa tatu wakati wa mjadala wa jumla akaamua kuishabulia Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa imechoka na kufanya mambo ya kufunika kombe.

Lissu alianza kwa kuinukuu katiba ya sasa, akisema hairuhusu hata dakika tano kumuongeza muda rais wala Bunge labda pale ambapo nchi inakuwa kwenye vita na nchi jirani.

“Lakini wachovu hawa wa serikali ya CCM wameshindwa kuipa fedha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kufanya kazi zake za uwazi ili kutengeneza mazingira ya kuongeza muda.

“Hawa wachovu walioshindwa kufanya kura ya maoni ya katiba inayopendekezwa waliyodanganya watu kuwa ingefanyika Aprili 30. Serikali ipi ya kufanya haya…hii iliyochoka,” alihoji na kuongeza;

Ndiyo maana wachovu hawa wa CCM walipigisha hata kura za marehemu, wagonjwa na wale waliokuwa hija nchini Macca wakati wa Bunge la Katiba.

Kauli hiyo, ilimwinua Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge, Jenusta Mhagama, akihoji utaratibu kwa Spika kwamba Lissu anaiita serikali ya CCM chovu wakati imefanya mambo makubwa nchini.

Hata hivyo, pamoja na utetezi huo, Lissu aliendelea kusisitiza kuwa, “serikali hii ni ya wachovu ndio maana imewasafisha hata watuhumiwa wa kashfa ya ukwapuaji wa fedha za escrow na walioua watu kwenye oparesheni tokomeza licha ya Bunge kuazimia wachukuliwe hatua.”

Awali, katika hotuba yake, Mbowe alisema “suala la kuongeza muda kwa serikali ya sasa kwa sababu yoyote ya NEC ni aibu na haitakubalika kwa vyovyote iwavyo. Uchaguzi sio jambo la kuzuka tu bali linajulikana na fedha zake zilishatengwa.”

Kuhusu mpango wa NEC kutaka kugawa majimbo ya uchaguzi, Mbowe amesema ilipaswa utaratibu huo ufanyike mapema na kuweka wazi maeneo yatakayohusika badala ya kushtukizwa sasa wakati vyama vikiwa vimeanza michakato ya ndani ya uteuzi wa wagombea.

“Hivi sasa serikali inaonekana kuwa na matatizo makubwa ya fedha baada ya wahisani kusitisha kutoa fedha za msaada wa bajeti kwa sababu ya ufisadi wa kutisha wa Tegeta Escrow Akaunti.

Pamoja na ukweli kuwa Sheria ya Taifa ya Uchaguzi inahitaji Tume kuboresha Daftari la Kudumu la wapiga kura angalau mara mbili kati ya uchaguzi mkuu na unaofuata; Kwa makusudi Serikali iliamua kuivunja sheria ya kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura,” amesema.

Kuhusu udhaifu wa NEC katika mfumo wa BVR, Mbowe amesema pamoja na zoezi kuanza kwa kusuasua ni wazi kuwa Tume haina watumishi wa kufanya kazi  katika zoezi hili muhimu kwa uhai wa Taifa.

Amesema NEC wameomba kupatiwa kiasi cha Sh. 187.962 bilioni kwa ajili ya uendeshaji wa uchaguzi ambao unapaswa kufanyika Oktoba mwaka huu.

“Kambi rasmi ya upinzani bungeni inataka kupatiwa mchanganuo wa kasma 229914.Uendeshaji wa uchaguzi mkuu kiasi cha Sh.187,962,160,000 hizi ni fedha kwa ajili ya vitu gani na hasa ikizingatiwa kuwa Tume haijatangaza zabuni kwa ajili ya vifaa vya uchaguzi huo,” amehoji.

Nao baadhi ya wabunge wa CCM, Henry Shekifu (Lushoto), Felister Burra (Viti Maalum), Ismail Rage (Tabora Mjini), Chacha Nyangwine (Tarime), Ali Keissy (Nkasi Kaskazini), waliomcharukia Lissu wakidai kuwa serikali ya chama chao imefanya kazi kubwa japo wapinzani hawaoni.

error: Content is protected !!