August 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Uchaguzi wagawa majeshi Zanzibar

Spread the love

Baada ya kuwepo fununu za mgawanyiko ndani ya Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar juu ya usimamizi wa amani katika uchaguzi wa marudio utakaofanyika machi 20 mwaka huu, uongozi wa juu wa vikosi hivyo umekuja juu na kukanusha taarifa hizo. Anandika Josephat Isango

Makamo Mwenyekiti wa Idara Maalum, Ali Abdalla Malimussy, Kamishna wa Zimamoto Zanzibar alikanusha taarifa hizo zilizoenezwa kwenye mitandao ya kijamii wakati akitoa taarifa maalumu mbele ya waandishi wa habari jana Ofisi za Zimamoto Kilimani Mkoa wa Mjini Magharibi. 

Kamishna huyo alisema kuna taarifa za uzushi  zilizosambazwa kwa vipeperushi na mitandaoni zenye lengo la kufitinisha vyombo vya ulinzi na usalama na wananchi wa Zanzibar.

Taarifa hizo zenye ujumbe usemao “Mfumo wako hatuutaki” zinazodaiwa kuandikwa na kusambazwa na baadhi ya vikosi hivyo ambao unamhusisha moja kwa moja Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalumu za SMZ Haji Omar Kheir.

“Kwa kweli jambo hili sisi limetusikitisha sana na tunaamini kwamba limetayarishwa kwa makusudi na kwa lengo maalumu na mtandao wa watu wanaotumiwa na wanasiasa wasioitakia mema nchi yetu “alisema Kamishna.

Alisema taarifa hizo zinazosambazwa sio za kweli na ni za uzushi na zina lengo la kusababisha vurugu kwa kisingizio cha kurejewa kwa uchaguzi wa marejeo ambao tayari baadhi ya viashiria vimesnaza kujitokeza.

Kwa mujibu wa taarifa hizo ambazo zinadai Waziri wa Vikosi ameamrisha kuagiza fomu maalumu za aina ya “Combat” kama zile za kijeshi kwa ajili ya kuwafanyia hujuma tofauti wananchi ikiwemo kuwapiga, kuwaua na kuwanyanganya mali zao wakati wa uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao.

“Tunalishukuru jeshi la polisi kwa kutoa tahadhari na kuanza kuwasaka wahusika kwa kuwachukulia hatua za kisheria” alisema Kamishna huyo wa Zimamoto Zanzibar.

Malimussy alisema taarifa kama hizo za uzushi hazipaswi kunyamaziwa kwa kuwa zinapoachiwa kuendelea kuhatarisha usalama wa nchi hasa katika kipindi hiki ambacho Zanzibar inakabiliwa na uchaguzi.

Kamishna huyo alitumia muda huo kuelezea ununuzi wa sare hizo kuwa hufanywa na idara maalumu na haimhusishi Waziri.

“Sare za vikosi vyote vya SMZ wenye jukumu hilo ni Vikosi wenyewe na sio kama inavyodaiwa ameagiza yeye aina ya sare zinazotakiwa, hapana” aliongeza.

Lakini alisema Zanzibar kuwa na sare za aina ya Combat katika vikosi vya ulinzi na usalama kwani ni jambo la kawaida kwa majeshi duniani kote kuwa na sare za aina hiyo kwa hivyo sio jambo la aibu wala kiroja.

Aidha Kamishna huyo alisema Waziri Kheri hakuwahi kufikiria wala kuagiza kikosi chochote kutekeleza maagizo hayo kuletwa kwa sare hizo kama inavyodaiwa.

Alisema Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalumu za SMZ Haji Omar Kheir yupo kikatiba ndani ya wizara yake na kusambazwa kwa vipeperushi hivyo ni njia moja ya kumfitinisha na watenaji wake.

Vikosi vya SMZ vinashutumiwa kushiriki katika ukiukwaji wa haki za binaadamu kutokana na baadhi ya askari wake kujifunika nyuso zao maarufu kama ‘Mazombi’ huku wakibeba silaha mbalimbali na kutumia magari ya vikosi hivyo kwa kupiga watu ovyo mitaani. Hata hivyo Kamishna huyo hakutaka kapiga suala hilo.

error: Content is protected !!